Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rita yatangaza utaratibu uhakiki wa vyeti

Muktasari:

  • Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) umetaja hatua za kufuata katika uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kupitia mfumo wa eRITA.

Dar es Salaam. Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) umetoa mwongozo wa uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa eRITA.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, waombaji wote wanapaswa kufuata hatua maalumu ili kupata huduma ya uhakiki wa vyeti hivyo.

Rita imeeleza kuwa uhakiki huo hufanyika kwa kutumia mfumo wa eRita pekee, wenye vyeti vya zamani wanapaswa kwanza kuvibadilisha kuwa vya kidijitali kabla ya kuendelea na mchakato wa uhakiki.

“Uhakiki unafanyika kupitia mfumo wa eRITA pekee. Walio na vyeti vya zamani vilivyochapwa kwa typewriter watalazimika kwanza kupata vyeti vya kidijitali kwa kufuata hatua zilizoainishwa, baada ya hapo achague OLD to NEW. Baada ya kukamilisha hatua hiyo na kupata cheti kipya ataendelea na uhakiki,” inaeleza sehemu ya mwongozo huo.

Katika hatua za awali, waombaji wanatakiwa kuingia kwenye tovuti ya Rita, kisha kubonyeza kitufe cha eRITA na kuchagua huduma ya vizazi na vifo.

Baada ya hapo, waombaji wanapaswa kujisajili kwa kubonyeza sehemu ya “Register” na kujaza taarifa zote zinazohitajika kwa ajili ya kufungua akaunti ya maombi.

“Muhimu: Nenosiri (password) liwe na herufi zaidi ya nane ikiwa na mchanganyiko wa herufi kubwa, ndogo, namba na alama mojawapo mfano (&@*#!)," imeeleza taarifa hiyo.

Baada ya usajili, mwombaji anatakiwa kufungua akaunti yake ya barua pepe, kutafuta ujumbe uliotumwa na Rita na kubonyeza sehemu ya “Account activation” ili kuamilisha akaunti hiyo.

Hatua inayofuata ni kuingia tena katika mfumo wa eRITA kupitia sehemu ya “Sign In” na kujaza taarifa zinazotakiwa.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, mwombaji atachagua huduma ya “Birth Services” kwa huduma za kuzaliwa au “Death Services” kwa huduma za vifo kabla ya kuendelea na maombi ya uhakiki.

Katika hatua ya maombi, Rita imeeleza kuwa mwombaji anatakiwa kuchagua “Request Verification” na kujaza taarifa zote kwa usahihi, zikiwamo taarifa za cheti husika.

“Chagua REQUEST VERIFICATION na jaza taarifa zote kwa usahihi ikiwa pamoja na namba ya cheti cha kuzaliwa au kifo (namba hii ipo katika safu (column) namba moja (1) katika cheti),” inaeleza sehemu ya mwongozo huo.

Baada ya kujaza taarifa hizo, mwombaji anatakiwa kuthibitisha taarifa alizoingiza, kuendelea na hatua inayofuata na kufanya malipo kulingana na ankara atakayopewa na mfumo.

“Kupata majibu ya uhakiki: Ingia katika akaunti uliyofungua ya mfumo wa eRITA, chagua huduma ya birth/death Submitted Details. Mfumo ukionyesha neno ‘verified’ itamaanisha cheti chako ni halali. Pakua fomu ya uthibitisho utakayotumia kupata huduma unazohitaji," imefafanua Rita.

Aidha, wakala hiyo imebainisha kuwa waombaji wa huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) watahitaji namba ya ombi inayopatikana kwenye fomu upande wa juu kulia.