Prime
Ripoti Maalumu: Watoto wanavyolawitiwa ufukweni Dar es Salaam

Mtoto Johnson (jina sio halisi) akiwa katika barabara ya Mandera eneo la Ubungo mataa
Dar es Salaam. Ukimuangalia usoni amejawa hofu, uchovu na mashaka ya kutojua kesho yake jijini hapa.
Alizaliwa Mbeya eneo la Mafiati mwaka 2009 sasa anaishi kwa kurandaranda katika viunga vya Jiji la Dar es Salaam.
Huyu ni Johnson Joseph (si jina halisi), mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani aliyetoroka nyumbani kwao jijini Mbeya na kufika Dar es Salaam mwaka 2020 kutafuta maisha na kuishia kulawitiwa mara kadhaa katika eneo la Feri wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam alipofikia kwa mara ya kwanza.
Johnson anasema kutengana kwa wazazi wake, naye kupelekwa kuishi kwa bibi ndiyo chanzo cha kutoroka Mbeya.
Anasema alipata wazo la kutoroka baada ya kuanza kuzurura na kufanya kazi ndogondogo katika stendi kuu ya Mbeya.
“Siku tuliyozamia kuja Dar mimi na rafiki yangu tuliwahi alfajiri pale stendi tukapanda kwenye chesisi ya gari, kule tulikutana na watoto wengine kama wawili hivi. Tulivumilia vumbi mpaka tulipofika Ubungo, baada ya abiria kushuka na sisi tulitoka tukakimbilia sehemu ambayo hatuijui,” anasimulia.
Johnson anasema kati ya waliozamia kuja Dar es Salaam, mmoja ilikuwa mara yake ya pili, hivyo akawaambia kuna sehemu wanaweza kupata kazi.
Anaeleza aliwapeleka Feri siku ya pili, ndipo alipoanza kulawitiwa na baadhi ya wavuvi kwa nguvu ili apate eneo la kulala na kula.

Ramani ikionyesha eneo la Feri Wilaya ya Kigamboni. Chanzo na: Google Earth
“Pale Feri tulikutana na wavuvi waliotufundisha kazi ndogondogo lakini usiku wanakuingilia na unakuwa huna nguvu kuwazuia. Watoto wengi wapo pale, baadhi nilitoka nao Mbeya na wengine nimewakuta wanafanyiwa hivyo ili wapewe chakula. Muda mwingine wanapewa sehemu ya kulala au wanakulinda usionewe na wahuni wengine,” anasema.
Johnson akifanya mahojiano na Mwananchi Digital alikuwa ameondoka eneo hilo na sasa anashinda Daraja la Juu la Kijazi, eneo la Ubungo.
Wakati Johnson na watoto wengine wakikumbwa na kadhia hiyo, Ripoti ya Haki za Binadamu nchini ya mwaka 2022 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inaonyesha kuongezeka kwa matukio ya ulawiti mara tano zaidi mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2021.
“Mwaka 2021, LHRC ilirekodi matukio 34 ya unyanyasaji wa kijinsia wa wavulana kwa njia ya kulawiti. 2022 idadi ya matukio iliongezeka hadi 166,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Simulizi ya Johnson ilinilazimisha kukita kambi Feri kuthibitisha vitendo hivyo.
Hatua ya kwanza nilitafuta picha ya mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 14.
Nilieleza amepotea; nikisingizia alitoroka nyumbani Mbagala na nimepata taarifa kuwa yupo maeneo yale ili nipate njia ya kuingia katika eneo hilo linaloogofya kutokana na mtindo wa maisha ya hapo.
Nilipofika Feri nilikutana na mwanamke aliyekaa karibu na ngalawa; baada ya kumsabahi nilimuoyesha picha na kumtajia jina la mtoto yule (si halisi) na kumuuliza kama anamfahamu.
“Kwa jina hilo simfahamu labda awe anatumia jina lingine huku, maana wakifika huku wanabadilishwa majina,” alisema mwanamke huyo wa makamo.
Nilipomdadisi kuhusu usalama wa mdogo wangu endapo atakuwa eneo hilo alisema: “Wanakuja wengine wanalala huku. Wengi wanabakwa kwa sababu wanazidiwa nguvu; unakuta mtu ni mkubwa lakini anamuingilia mtoto mdogo.
Mtoto wako akija huku jiandikie ameharibika kwa sababu michezo hiyo ya kijinga ipo na wanafanyiana wenyewe kwa wenyewe, lakini na watu wazima pia wanawafanyia watoto.” Niliendelea kusogea mbele kando mwa bahari.
Boti nyingi zimeegeshwa na kuna watu waliovaa nguo kuukuu wakichambua nyavu, bila shaka walikuwa wavuvi.
Nilimfuata mmoja wao, nilipojitambulisha na kumuonyesha picha ya niliyekuwa namtafuta aliwaita wenzake na kuwauliza iwapo wamewahi kumuona; wote walisema hawajawahi lakini waliniletea mtoto mdogo waliyemuita ‘Banjuka’ anipeleke upande wa pili kumtafuta.
“Mwanangu huyu dogo (anaonyesha picha niliyowapatia) hapa hatujawahi kumuona ila kuna upande wa pili kule nao wanavua samaki. Ngoja tukupe huyu dogo akupeleke ila ‘umtoe’ -umpatie fedha,” anasema mmoja wao.
Bila ajizi nilikata shauri kuongozana na Banjuka, ambaye kwa mwonekano amekubuhu tabia hatarishi kutokana na kauli za matusi, misemo na hata matendo. Kwa kukadiria umri wake si zaidi ya miaka 16.
Tukiwa tunavuka upande wa pili kwa kutumia pantoni nilimdadisi sehemu gani tunakwenda na kama kuna uhakika wa kumpata mdogo wangu.
“Huku tunakwenda Tanavamba, peke yako huwezi kuingia kwa sababu utajulikana wewe ni wakuja (mgeni), unaweza kumpata,” alijibu kwa lugha na lafudhi ya majivuni huku akionyesha kutojali kitu.
Nilipomuuliza iwapo watoto wa kiume wanalawitiwa Banjuka alisema, “Eeeh! ukiwa mgeni unafanyiwa hivyo kwa sababu unakuwa huna uwezo wa kuwazuia na hakuna mtu wa kukutetea.”
Baada ya kufika Tanavamba tulipita kwenye baadhi ya boti zilizoegeshwa kando mwa bahari kumtafuta, tuliuliza baadhi ya wavuvi na watu wengine waliokuwa wakibarizi eneo lile na wote walieleza hawamfahamu.
Eneo hilo lilikuwa na watoto wadogo (umri wa miaka 11 hadi 16) waliokuwa wanasaidia kuchambua nyavu kabla ya kutumika kwenye uvuvi; wengi wao vichwani wamesokota ‘dread’.
Tulimaliza na kuondoka eneo lile, Banjuka alinitaka nimpatie Sh5,000 ili arudi hata kama hatujampata ninayemtafuta. Nilifanya hivyo.
Dawati la Jinsia
Kamanda wa Polisi Dawati la Jinsia Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Leah Mbunda alipoulizwa na Mwananchi Digital kuhusu uwapo wa vitendo vya ulawiti eneo hilo alisema unafanyika sehemu nyingi kwa sasa na si Feri pekee.
Anasema wanafanya operesheni kadhaa kuzuia matukio hayo.
“Ulawiti kwa sasa unaweza kufanyika sehemu yoyote si Feri na ufukweni pekee, na huko kote tunaendelea kufuatilia.
“Tunapenda kuzuia kabla kosa halijatendeka, katika kuzuia makosa kama hayo ya kulawiti na kubaka hasa kwa watoto, tumejikita kutoa elimu kwa wazazi na walezi ili kuwalinda kwa sababu bado mtoto hawezi kujisimamia,” anasema.
Kamanda Leah anasema katika utoaji elimu kuhusu watoto wa mtaani, wanashirikisha viongozi wa dini ili ndoa zidumu.
“Kwa sababu watoto wengi wanaokuja Dar es Salaam hawana sehemu za kulala, wanakutana na watu wanawapeleka Feri kuwapa kazi ya kuparua samaki ila wanakuwa na mambo yao.
“Baada ya hapo kwa ajili ya kupata malazi watoto hao wanajikuta wanafanyiwa vitendo hivyo, hilo tunapambana nalo,” anasema.
Kuhusu hatua wanazochukua endapo wakibaini vitendo hivyo amesema:
“Inapotokea kitu kama hicho tunarudi katika misingi ya sheria kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa tena haraka, na vielelezo tunakusanya.”
Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), Bakari Kadabi alipoulizwa kuhusu vitendo vya ulawiti kufanywa na baadhi ya wavuvi alisema,
“Nimeshtushwa na taarifa hizo, tunalaani na tutafanya uchunguzi tujue. Hayo ni mambo maovu na yanafanywa na wasio waadilifu, hatuungi mkono.
“Wavuvi ni watu kama wengine, hivyo mmomonyoko wa maadili ni suala mtambuka, isionekane jamii nzima ya wavuvi ndiyo inafanya hivyo. Tutajikita kutoa elimu,” anasema.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Nyamara Elisha anasema hali ilikuwa mbaya zaidi kipindi cha nyuma, japokuwa wamefanya operesheni kadhaa kuzuia ulawiti maeneo ya ufukweni.
“Kuhusu ulawiti kwa watoto Kigamboni, hali ilikuwa mbaya zaidi miaka miwili iliyopita, tulifanya operesheni maalumu tukapunguza kwa sababu tulikataza watoto wasilale ufukweni.
“Kwa kipindi cha hivi karibuni, nimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni (Halima Bulembo), kwa sababu alifanya ziara maeneo yale akatoa katazo. Aliagiza viongozi kuhakikisha watoto wadogo hawafiki maeneo yale kwa kuwa ni hatarishi kwao,” anasema.
Mkurugenzi wa Shirika la Kulinda Watoto la Save the Children, Angela Kauleni anasema matukio ya ulawiti pia yanafanywa nyumbani na shuleni, hivyo jitihada zaidi za kuyazuia zinahitajika.
“Kama shirika la kutetea haki za watoto, tunasikitishwa na matukio ya unyanyasaji yanayotokea nyumbani, shuleni na katika jamii yanayofanywa na wazazi, walimu, walezi na watu wengine ambao wanadhuru watoto kimwili, kingono na kihisia.
“Tunajua kesi zipo nyingi na hizi ambazo zinaripotiwa na vyombo vya habari ni chache tu kati ya hizo,” anasema.
Kauli ya Angela inaungwa mkono na Kamanda Leah anayesema bado kuna changamoto ya kesi nyingi za aina hiyo kutoripotiwa, badala yake familia zinasuluhisha nyumbani na nyingine hazijulikani kabisa.
Waziri mwenye dhamana
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima akiwasilisha mada ya mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye mafunzo ya wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na viongozi wa jumuiya hiyo ngazi ya mikoa na wilaya jijini Dodoma Machi 21 hadi 22, mwaka huu, alisema matukio ya ukatili kwa ujumla yameongezeka mwaka 2022 ikilinganishwa na 2021.
“Mwaka 2022 matukio 12,163 ya ukatili kwa watoto yameripotiwa ukilinganisha na 11,499 mwaka 2021; ubakaji ni 6,335, ulawiti 1,555, mimba za utotoni 1,557, kuzorotesha masomo 808 na mashambulizi 231,” alisema.
Dk Gwajima alisema matukio mengi ya ukatili hufichwa na jamii maeneo ambako hakuna elimu na mifumo thabiti, hivyo manusura hukosa huduma na haki.