Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ridhiwani awapiga 'biti' maofisa utumishi nchini

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa. Picha na mpiga picha maalum

Muktasari:

  • Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka maofisa utumishi kutosubiri mpaka ziara za viongozi ndipo waitishe vikao vya watumishi ili kusikiliza kero zao.

Iringa. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka viongozi wa halmashauri hasa maofisa utumishi kujenga tabia ya kuitisha vikao vya watumishi wa umma ili kuwasikiliza badala ya kusubiri ziara za viongozi pekee.

Hatua hiyo imekuja baada ya baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo kuelezea kero zao ikiwamo kutopandishwa madaraja na makato ya mishahara.

Amesema kwa kuwasikiliza watumishi hao, zipo baadhi ya kero na malalamiko ambayo wanaweza kujibu na kutatua bila kufikishwa ngazi za juu ikiwa wataweka utaratibu wa kuwasikiliza.

Akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo jana Jumatano Novemba 22, 2023, Ridhiwani amesema kwa kufanya hivyo wataongeza morali ya kazi na hivyo kusaidia kuharakisha maendeleo ya Taifa.

“Fikiria mfanyakazi ana makato ya miaka minane na wewe ofisa rasilimali watu upo tu? Shida ni nini? msisubiri mpaka waziri au naibu waziri aje ndio muitishe vikao vya watumishi. Tengenezeni utaratibu wa kukutana nao,” amesema Ridhiwani na kuongeza;

“Sitaki kusikia mfanyakazi ameacha kituo chake cha kazi amekwenda Dodoma kwa mambo ambayo ofisi za wakurugenzi na maofisa rasilimali watu mnaweza kushughulikia.”

Amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuwa wabunifu wakati wanapotekeleza majukumu yao ikiwamo kuwahudumia wananchi.

Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kazi na kwamba imeweka baadhi ya mifumo ya kiutendaji inayoweza kuwapima kutoka kwenye halmashauri zao.

“Mfano, Serikali imebuni mfumo wa kujua ufanisi wa kazi kwenye maeneo ya kazi ambao unaonyesha kati ya kero 21 zilizofikishwa kwenye wilaya ya Kilolo, tano zimeshughulikiwa,” amesema.

Ameipongeza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Iringa (IRUWASA) ambayo kati ya kero 53, kero 52 zimeshughulikiwa.

Awali, baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo walilalamika kuwepo kwa kero mbalimbali ikiwamo makato ya mishahara na kutopandishwa madaraja, jambo linalopunguza morali ya kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Peresi Magiri amewataka watumishi wa umma kutumia mkutano huo kutoa kero na malalamiko yao ili yaweze kushughulikiwa.

Mbunge wa Kilolo (CCM), Justine Nyamoga amesema uhaba wa watumishi hasa walimu ni moja kati ya changamoto zinazowakabili Wilaya ya Kilolo kutokana na jografia kuwa ngumu.

“Kuna watumishi ukiwapeleka huko vijijini wanatamani kuhama, kitakachosababisha wabaki huko ni mazingira mazuri,” amesema Nyamoga.

Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati amesema watumishi wa umma ni kundi muhimu kwenye jamii linalochangia kuwepo kwa kasi ya maendeleo.