Rea yapeleka umeme vijijini asilimia 69, kukamilisha mwakani

Muktasari:
Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) imesema umeongeza huduma ya upatikanaji umeme kutoka asilimia 2 mwaka 2007 hadi kufikia 69.6 Juni mwaka huu.
Dar es Salaam. Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) imesema umeongeza huduma ya upatikanaji umeme kutoka asilimia 2 mwaka 2007 hadi kufikia 69.6 Juni mwaka huu.
Pia imesema inatarajia hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha ujao vijiji vyote 12,345 vitakuwa vimeunganisha umeme kwa awamu ya tatu.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Novemba 30, 2021 na Mkurugenzi Mkuu wa Rea, Mhandisi Hassan Saidy wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu na mafanikio ya Wakala hao katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru.
Amesema malengo yalikuwa kufikia asilimia 50 hivyo wameweza kuvuka lengo walilojiwekea kwa ongezeko la asilimia 19.6.
Amebainisha mpaka sasa wameweza kutekeleza miradi 21, ambapo kati ya hiyo 13 ni ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji, saba kwa njia ya jua huku mmoja wa kutumia tungamo taka (bayogezi).
Pia ameongeza kuwa wameweza kuunganisha umeme kwa taasisi za elimu 7735, vituo vya afya 4002, vituo vya kusukuma maji 3400, maeneo mbalimbali ya biashara 1967 pamoja na nyumba za ibada 5117.
"Pamoja na hayo tumeweza kupanua mifumo ya usambazaji umeme, kuwezesha utekelezaji wa miradi kwenye maeneo ambayo gridi ya Taifa haijafika pamoja na kufunga umeme wa jua kwenye vituo vya afya na maeneo ya kijamii ambayo iko mbali na gridi.
"Tumejipanga kuhakikisha nishati bora inawafikia wananchi wote waishio vijijini, hivyo wakala utaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ili kufika malengo hayo ya Taifa," amesema Saidy.
Naye Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila amesema kwasasa wanaendelea na mradi wa kuunganisha umeme wa jua (sola) katika wilaya ya Kishapu, ambapo mpango ni kuhakikisha kunakuwa na miradi mingi ya sola.