RC Dar: Watanzania tumieni ‘Saba Saba’ kuteka masoko kimataifa
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Juni 25, 2026 jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea Viwanja vya Sabasaba, wilayani Temeke.
Muktasari:
- Chalamila ametoa wito huo Dar es Salaam leo Juni 25,2026 jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea Viwanja vya Sabasaba, wilayani Temeke, kukagua maandalizi ya maonyesho hayo yanayoadhimisha Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na yanayotarajiwa kuanza rasmi Juni 28, 2026.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewahimiza Watanzania kutumia fursa ya Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, kutangaza bidhaa zao katika masoko ya kimataifa kupitia mifumo ya kidijitali ili kuongeza ushindani na kupanua wigo wa biashara.
Chalamila ametoa wito huo leo Alhamisi, Juni 25, 2026 jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea Viwanja vya Sabasaba, wilayani Temeke, kukagua maandalizi ya maonyesho hayo yanayoadhimisha Jubilei ya Dhahabu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na yanayotarajiwa kuanza rasmi Juni 28, 2026.
Amesema maonyesho hayo yatawakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa biashara kutoka mataifa mbalimbali, hivyo kutoa fursa adhimu kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania kutangaza bidhaa zao na kufikia masoko mapya nje ya nchi.
“Tunataka wafanyabiashara wa Tanzania wafikirie zaidi ya masoko ya ndani. Mustakabali wa uchumi wetu unategemea uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa. Saba Saba inatoa fursa hiyo,” amesema Chalamila.
Amesema maonyesho ya Sabasaba yamekua kutoka ya kawaida ya ndani na kuwa jukwaa muhimu la biashara, uwekezaji na mageuzi ya kiuchumi nchini, hivyo toleo la Jubilei ya dhahabu linaakisi safari ya maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania katika kipindi cha miongo mitano iliyopita na matarajio ya miaka ijayo.
Chalamila amesema ongezeko la ushiriki wa mataifa kutoka Afrika, Asia na Mashariki ya Kati linaonesha kuimarika kwa imani ya kimataifa kwa uchumi wa Tanzania na nafasi yake kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
"Kuna umuhimu wa kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, changamoto iliyopo si uzalishaji pekee bali kuhakikisha bidhaa hizo zinafikia masoko ya kimataifa ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni, ajira na ukuaji wa uchumi wa viwanda," amesema
Katika kuendana na mabadiliko ya teknolojia, Chalamila amewataka wafanyabiashara kutumia zana za masoko ya kidijitali, majukwaa ya biashara mtandaoni na mifumo ya utambuzi wa bidhaa kama vile misimbo pau (barcodes) ili kuongeza mwonekano wa bidhaa zao.
“Dunia inabadilika kwa kasi. Biashara ambayo haiwezi kupatikana mtandaoni inazidi kuwa isiyoonekana kwa wateja watarajiwa. Teknolojia si chaguo tena ni hitaji muhimu,” amesema.
Amesema matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia biashara ndogo na za kati kuvuka vikwazo vya upatikanaji wa masoko na kuunganishwa moja kwa moja na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis amesema zaidi ya washiriki 3,000 na wawakilishi kutoka nchi 23 wanatarajiwa kushiriki katika maonyesho ya mwaka huu, jambo litakaloyafanya kuwa miongoni mwa matoleo makubwa zaidi katika historia ya tukio hilo.
Amesema maonyesho hayo yanafanyika wakati Tanzania ikiendelea na jitihada za kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi, kuimarisha uzalishaji wa viwandani na kuvutia uwekezaji zaidi kwa ajili ya kukuza uchumi wa Taifa.