Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia: Tunzeni chakula hali si nzuri

Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kutumia vizuri chakula, huku wakijihadhari na njaa inayoweza kuikumba dunia kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo mabadiliko ya tabianchi, athari za Uviko-19 na vita kati ya Urusi na Ukraine.

Mkuu huyo wa nchi alitoa tahadhari hiyo jana, wakati wa hotuba yake ya kuzindua tamasha la utamaduni na ngoma za asili za jamii ya Wasukuma, zinazochezwa kipindi cha mavuno maarufu kama Bulabo linaloendelea katika viwanja vya Red Cross, eneo la Kisesa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Alisema kutokana na tishio hilo la njaa na mfumuko wa bei duniani, Serikali inakamilisha mchakato wa kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha katika maghala ya Taifa kwa tahadhari, lengo likiwa ni kuwahakikishia Watanzania uwepo wa chakula.

Huku akiwasihi wakulima kutouza nje ya nchi mavuno yao, Rais Samia alisema kwa kawaida, mfumuko wa bei katika kipindi kama hiki huwa inatarajiwa kuwa asilimia 5, lakini kutokana na athari za Uviko-19, vita vya Urusi na Ukraine na mabadiliko ya tabianchi, mfumuko wa bei duniani umefikia zaidi ya asilimia 10 kinyume cha matarajio.

Kuhusu uhimilivu wa mfumuko wa bei, Amiri Jeshi Mkuu huyo alisema Serikali inafanya jitihada mbalimbali kudhibiti mfumuko wa bei, huku akitaja uamuzi wa kutoa ruzuku kwenye biadhaa ya mafuta na mbolea kama moja ya jitihada hizo.

Pembejeo za kilimo

Rais Samia aliwahimiza wakulima nchini kujisajili katika mfumo wa ruzuku ya pembejeo inayotolewa na Serikali kupitia vyama vya msingi vya ushirika, lengo likiwa ni kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Alisema Serikali pia inaendelea kutekeleza miradi kadhaa ya kufufua na kujenga skimu za umwagiliaji kuwezesha wakulima kutumia ardhi nzuri, mabonde yanayofaa kwa kilimo na wingi wa vyanzo vya maji nchini kulima na kuvuna kwa kipindi chote cha mwaka badala ya kutegemea misimu ya mvua.

Mazingira, mmomonyoko wa maadili

Akiwageukia machifu, watemi, viongozi wa dini na kijamii, Rais Samia ambaye ndiye Chifu Mkuu wa Machifu wote nchini aliwataka viongozi hao wa kimila kutumia nafasi na ushawishi wao ndani ya jamii kuonya, kukemea na kuelekeza vijana kuhusu tamaduni na maadili mema ya Kitanzania.

Alisema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kundi la vijana ndilo linaloongoza kwa wingi wa watu nchini; hivyo ni muhimu kuangaliwa kwa macho mawili kwa kuwalea, kuwaelekeza na kuwaonya dhidi ya mmomonyoko wa maadili ambao wakati mwingine huchochewa na maendeleo ya teknolojia na utandawazi.

Uhifadhi wa mazingira ni eneo lingine ambalo Rais Samia alishauri liwe ajenda ya kudumu kwa kila Mtanzania kupanda miti siyo tu kwa nia ya kutunza na kuhifadhi mazingira, bali pia kulinda uoto wa asili utakaowezesha uwepo wa mvua za kutosha na hatimaye mavuno mazuri.

Utamaduni na utalii

Kuhusu mapato kupitia sekta ya utalii, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka nyingine za Serikali kuendeleza na kuuza nje mila, desturi na tamaduni za makabila zaidi ya 120 nchi kama sehemu ya vivutio vya utalii.
“Tuzilinde na kuziendeleza tamaduni zetu kwa sababu utamaduni ni nyenzo muhimu ya maendeleo inayoweza kutuingizia fedha nyingi za kigeni,’’ aliagiza Rais Samia, huku akiagiza kupitiwa upya na kuboreshwa kwa Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997.
Katika hatua nyingine, Rais Samia aliiagiza Wizara ya Maji kufufua visima vya zamani kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji wakati utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaogharimu zaidi ya Sh69 bilioni ukiendelea.

Mgogoro wa ardhi Magu

Akijibu ombi la Askofu Mkuu Jimbo Kuu Katoliki Mwanza, Renatus Nkwande kuhusu mgogoro wa umiliki wa eneo la utamaduni na hija la Kageye kati ya Kanisa hilo na Halmashauri ya Wilaya ya Magu, kiongozi huyo mkuu wa nchi aliiagiza Wizara ya Ardhi, Nyuma na Maendeleo ya Makazi na Wizara Maliasili na Utalii kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kutatua suala hilo.

Awali akitoa salamu mbele ya Rais Samia, Askofu Nkwande alisema licha ya eneo hilo kujengwa na Kanisa, uongozi wa halmashauri hiyo imelitwaa huku waumini wakizuiwa hata kuingia kufanya ibada katika majengo waliyoyajenga wao wenyewe.

Imeandikwa na Saada Amir, Mgongo Kaitira, Damian Masyenene na Anania Kajuni.