Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia atunukiwa tuzo mwanamke kinara 2025

Muktasari:

  • Sababu ya kumpatia tuzo hiyo Rais Samia Suluhu Hassan ni uongozi wake kuwa chachu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayochangia maendeleo ya uzalishaji, ujasiriamali na ustawi wa kijamii kwa wanawake.

Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan ametunukiwa tuzo ya heshima ya mwanamke kinara 2025, huku akishukuru na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa masilahi ya Taifa.

Tuzo hiyo ilitolewa juzi usiku mkoani Mwanza na taasisi ya Mwanamke Kinara iliyoandaa tuzo za wanawake waliofanya vizuri katika sekta mbalimbali Kanda za Ziwa na Magharibi, huku mgeni rasmi akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa.

Akizungumza na Kadogosa kwa njia ya simu baada ya kupokelewa tuzo hiyo, Rais Samia alisema anashukuru kwa waandaaji kwa kuona mchango wake na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya wananchi na masilahi ya Taifa.

"Ninashukuru sana kwa tuzo kutoka kwa wanawake wa mikoa ya kanda ya ziwa na magharibi. Ninawashukuru sana kwa ushirikiano mlionipa, mimi kama mama mmenipa utulivu ndio maana nimeweza kuyafanya niliyoyafanya.

"Tumeweza kuboresha sekta ya maji, umeme na barabara, ahadi yangu ni kuendelea kuwatumikia wananchi na Taifa kwa kadri Mungu atakavyonijalia," alisema Rais Samia.

Katika risala ya waandaaji wa tuzo hizo, walisema sababu ya kumpatia tuzo hiyo Rais Samia ni uongozi wake kuwa  chachu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayochochea shughuli za uzalishaji, ujasiriamali na maendeleo ya kijamii kwa wanawake.

Pia, miradi hiyo imekuwa mkombozi kwa wanawake wengi waliokuwa pembezoni mwa mfumo rasmi wa uchumi.

“Tumeona ni jambo la heshima na faraja kubwa kuenzi uongozi wa Rais wetu kwa kumpatia tuzo hii maalumu. Kupitia dira yake ya maendeleo jumuishi, wanawake wamewezeshwa, wamehamasika na sasa ni kinara wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi,” alisema Khadija Liganga, mwanzilishi na mwandaaji wa tuzo hizo .

Katika hafla hiyo, jumla ya wanawake 16 kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Kagera, Mara, Tabora na Kigoma walitunukiwa tuzo mbalimbali kutokana na mchango wao katika sekta za uongozi, biashara, kilimo, elimu, afya na ustawi wa jamii.

Pia, mwandishi na msimamizi wa gazeti la Mwananchi Kanda ya Ziwa, Saada Amir aliibuka mshindi katika tuzo hizo upande wa mwanamke kinara 2025 katika sekta ya habari.