Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia atunukiwa udaktari wa heshima India

Muktasari:

  • Rais Samia ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (Doctorate Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru kwenye hafla iliyofanyika jijini New Delhi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametunukiwa udaktari wa heshima (PhD) na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru (JNU) India kwa kutambua mchango wake katika kuchochea maendeleo ya watu nchini Tanzania.

Rais Samia yuko India kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine leo Oktoba 10, 2023 ametunukiwa shahada ya pili ya udaktari wa heshima.

Mara ya kwanza alitunukiwa udaktari wa heshima Novemba 30, 2022 na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akitangaza kumtunuku Rais Samia shahada hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru, Santishree Dhulipudi Pandit amesema:

“Kwa mamlaka niliyopewa mimi Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru, ni heshima kwangu kumtunuku udaktari wa heshima (Honoris Causa) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, sasa Dk Samia Suluhu Hassan kwa uhusiano wa Tanzania – India na uhusiano wa India – Afrika,” amesema.

Baada ya kutangaza kumtunuku shahada hiyo, Pandit amemkabidhi Rais Samia cheti, nishani na vazi maalumu kama ishara ya kumtunuku udaktari wa heshima kiongozi huyo ambaye ndiyo mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini Tanzania.

Pandit amesema mwaka 1995, chuo hicho kilimtunuku Mwalimu Julius Nyerere udaktari wa heshima, hivyo, Rais Samia amekuwa kiongozi wa pili wa Tanzania kutunukiwa hehima hiyo na chuo hicho.

“Chuo chetu kimetoa washindi wawili wa tuzo za Nobel na wote ni katika uchumi. Pia, chuo hiki kipo katika nafasi 10 bora ya vyuo vikuu bora duniani katika masomo matano,” amesema makamu mkuu wa chuo.

Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo ya udaktari wa heshima, Rais Samia amekishukuru Chuo cha Jawahalal Nehru kwa kumtunukia shahada hiyo akieleza kwamba hiyo imeongeza kitu katika historia yake.

Amesema siyo mara ya kwanza kwenda India, alikwenda kwa mara ya kwanza mwaka 1998 alipokuwa akisoma katika Chuo cha Teknolojia na Utawala cha Hyderabad, lakini amerudi tena nchini humo akiwa kama Rais wa Tanzania.

“Mmenibadilisha kama familia na kunitunuku shahada ya heshima (honoris causa), sasa nimesimama hapa kama mmoja wa familia ya Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru na siyo kama mgeni wa kawaida. Asanteni sana,” amesema Rais Samia.

Amekishukuru chuo hicho kwa kumpa heshima hiyo na kwamba anaikubali kwa kuwa anathamini uhusiano wa Tanzania na India na pia imeongeza kitu kwenye historia ya maisha yake.

“Shahada hii ya heshima itakuwa daima katika historia yangu kwa kuwa ya kwanza kutolewa kwangu na nchi ya kigeni. Ninayo moja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini hii itakuwa ya kwanza kupewa na chuo cha nje,” amesema Rais Samia.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Subrahmanyam Jaishankar amesema elimu na kujenga uwezo ni moja ya vipaumbele katika uhusiano wa Tanzania na India ambapo zaidi ya Watanzania 5,000 wamepata mafunzo katika taasisi za elimu za India hasa kwenye teknolojia.

Jaishankar amesema wameamua kuanzisha Taasisi ya Teknolojia ya India (IIT) huko Zanzibar na ratiba kwa ajili ya watahiniwa wa kwanza inaandaliwa na mwezi huu wataanza maomo yao.

“Taasisi hii (IIT) ina fursa ya kuwa kituo kikuu cha elimu ya teknolojia kwa bara zima la Afrika. Ni ishara ya ushirikiano wetu na dunia ya kusini na ni farahi kwangu kuwahi kwenda Zanzibar katika shughuli zangu,” amesema.

Waziri huyo ameisisitiza kwamba ziara ya Rais Samia ni ya kwanza kwa kiongozi wa Afrika kuitembelea India tangu Umoja wa Afrika (AU) ilipoingizwa kwenye umoja wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda duniani (G20).