Rais Samia ateua watendaji Tume ya Mipango

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan, leo Mei 29, 2024 jijini Dodoma amewaapisha wajumbe wa Tume ya Mipango. Lengo la Tume hiyo ni kusimamia uchumi, mchakato wa upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, akiwamo Dk Mursali Milanzi, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya Mipango ya Kitaifa.

Kabla ya uteuzi huo, Dk Milanzi alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango ya Kitaifa katika Tume ya Mipango.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Mei 29, 2024 na Zuhura Yunus, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema Rais Samia amemteua Dk Lorah Madete kuwa Naibu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya Ubunifu wa Biashara. Kabla ya uteuzi alikuwa Meneja wa Idara ya Uchumi Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Mwanza.

Mteule mwingine ni Dk Linda Ezekiel anayekuwa Naibu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya Menejimenti ya Utendaji na Tathmini.

Dk Ezekiel alikuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Taasisi ya Ofisi ya Rais ya Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (PDB).

Rais Samia amemteua Alban Kihulla kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA). Kabla ya uteuzi huo alikuwa akikaimu nafasi hiyo.

Pia amemteua Profesa Najat Kassim Mohamed kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC).

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Najat alikuwa Naibu Mkuu wa Chuo (Mipango, Utawala na Fedha), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Mteule mwingine ni Bernadetta Ndunguru anayekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).

Bernadetta ni Mkurugenzi wa Mafunzo mstaafu, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).