Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia aacha kitendawili

Dar/Dodoma. Kitu gani kimetokea Ikulu? Ni anguko la Diwani Athuman au kupanda kwake na kushuka? Vipi wengine walioondolewa? Haya ni miongoni mwa maswali yanayogonga vichwa vya wengi kutokana na uamuzi alioufanya Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya saa 48 ulioacha kitendawili.

Ni ndani ya saa hizo, mkuu huyo wa nchi alimteua Kamishna wa Polisi Diwani kuwa Katibu Mkuu-Ikulu kutoka kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) kisha akatengua uteuzi wake na kumteua Mululi Mahendeka ambaye awali alikuwa ofisa mwandamizi wa Ofisi ya Rais, Ikulu kuwa katibu mkuu Ikulu.

Hatua hiyo imeibua maswali lukuki maeneo kadhaa ikiwemo mitandaoni huku wachambuzi waliozungumza na gazeti hili, wakitofautiana juu ya kinachoweza kuwa kimetokea.

Katika panga pangua hiyo ya Rais Samia aliyoitangaza usiku wa Januari 3, alimteua Said Hussein Masoro kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa kuziba nafasi ya Diwani. Masoro anakuwa mkurugenzi mkuu wa 10 wa idara hiyo nyeti tangu Uhuru.

Pia, Rais Samia alimteua Moses Kusiluka kuwa Katibu Mkuu Kiongozi akichukua nafasi ya Balozi Hussein Katanga ambaye aliteuliwa kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa New York, nchini Marekani.

Balozi Katanga anakwenda kuchukua nafasi ya Profesa Kennedy Gaston ambaye uteuzi wake umetenguliwa na kurejeshwa nchini. Kabla ya uteuzi huo Kusiluka alikuwa Katibu Mkuu Ikulu.

Wakati wateule hao wakiwa hawajaapishwa, Rais Samia anatangaza kutengua uteuzi wa Diwani, hali inayoibua maswali zaidi, miongoni mwa wachambuzi wa siasa waliozungumza na Mwananchi.

Miongoni mwa waliozungumzia hatua hiyo ni Dk Faraja Kristomus, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyesema Rais Samia atakuwa ameshauriwa vinginevyo kuhusu uteuzi wa Diwani, kwamba ungeweza kuathiri utendaji wa wafanyakazi wa Ikulu.

Alisema katibu mkuu wa Ikulu anapaswa kushauriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), kwa hiyo kumweka Ikulu mtu aliyekuwa Mkurugenzi wa TISS kutadhoofisha utendaji ndani ya Ikulu.

“Uwezekano wa yeye (Diwani) kushauriwa na mkurugenzi mpya wa usalama wa taifa (aliyekuwa msaidizi wake) unakuwa ni mdogo kwa sababu yeye ametoka huko. Kwa hiyo, wajuvi watakuwa wamemshauri Rais kwamba hapa angesababisha mgogoro wa kimahusiano na kiutendaji,” alisema.

Vilevile, aliongeza kuwa wafanyakazi wa Ikulu wakigundua katibu mkuu wa Ikulu alikuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, ingewanyima uhuru na amani ya kufanya naye kazi, hivyo ingepunguza ufanisi.

Wakati Dk Kristomus akieleza hayo, Rainery Songea mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, alisema kutenguliwa kwa Diwani ndani ya saa 48 tangu kuteuliwa kunaonyesha kuna shida kwenye upekuzi wa taarifa za wateuliwa (vetting) .

“Inawezekana baada ya kupata taarifa za kutosha, ikaonekana mtu huyu hawezi kufaa kwenye hiyo nafasi, ndiyo maana wakabadilisha, kama itampendeza anaweza kumpa nafasi nyingine baadaye,” alisema Songea.

Alisema Diwani anaweza akawa amefanya vizuri kwingine alikotoka lakini akaonekana hafai katika nafasi hiyo. Pia, inategemea Rais anamwonaje katika kufanya naye kazi.

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk David Mwakapala alisema suala la utenguzi wa kiongozi huyo ni utaratibu wa kiufundi kwenye utawala, na Rais ameona nafasi hiyo haikuwa vizuri na kwa mamlaka aliyonayo ana uwezo wa kufanya utenguzi ili kuboresha kwa namna ambavyo anataka ofisi, nchi na watumishi wake wawe.

“Nafikiri ni suala la kiufundi zaidi, ameangalia namna ambavyo anataka watendaji wake wawe na kuona kuwa yule aliyemuweka hapo ata-fit (atafaa) sehemu nyingine, na nimeangalia utenguzi huo nimeona hajapangiwa majukumu mengine, nawaza labda atampangia majukumu mengine, lakini kwa Rais ni jambo la kawaida ili kuboresha kama alivyosema atapanga safu ya kuendana naye,” alisema msomi huyo.

Kwa upande wake Dk Upendo Biswalo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John alisema Rais ana uwezo wa kujua mwenendo wa kila mtumishi wake na ikiwa atateua na kisha kupewa sifa au maelezo tofauti na watendaji wake kuhusu mtu huyo, ana mamlaka ya kufanya utenguzi kwa namna atavyoona itafaa.

“Ni suala la kufikirisha kwakweli hasa kwa wananchi na watu walio nje ya mfumo wa uteuzi huu wa muda mfupi. Tunajiuliza ni kwamba aliteuliwa kwa bahati mbaya au kuna kasoro gani zilizojitokeza au atampangia majukumu gani ambayo Rais ataona yanafaa, bado tupo kwenye mkanganyiko kwa kweli,” alihoji.


Anakwenda wapi?

Baada ya kuwa amehudumu serikalini kwa nafasi kadhaa kama Katibu Tawala Mkoa wa Kagera (RAS) akitoka kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi Mkuu Takukuru na Usalama wa Taifa, miongoni mwa maswali ni kuwa sasa anakwenda wapi?

Mwanasheria Jebra Kambole alisema kiutaratibu mtendaji huyo anarudi kutekeleza majukumu yake kwa mwajiri wake wa zamani (polisi) kwa sababu hakustaafu wala kufukuzwa.

“Kama alikuwa askari au jeshi anarudi katika nafasi yake ya mwanzo huko ndiko atakapopangiwa, si kwamba anakuwa jobless (anakosa kazi) hapana. Mwajiri wake wa kwanza ndiye anajua aendelee katika nafasi ipi ni kama vile mtu alikuwa ameazimwa kufanya shughuli katika idara nyingine.

“Angekuwa amefukuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu ingekuwa mambo tofauti,” alisema Kambole.


Wapo wenzake

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kutengua uteuzi muda mfupi baada ya kuteua, kwani Julai 31 mwaka jana ikiwa siku tatu tangu alipomteua Dk Raphael Chegeni kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, alitengua uteuzi huo.

Pia, Aprili 5, 2022 alitengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Thobias Richard ikiwa ni chini ya saa 12 tangu amteue kushika wadhifa huo.


Imeandikwa na Bakari Kiango, Peter Elias (Dar) na Mainda Mhando (Dodoma)