Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Kenyatta: Makabidhiano madaraka yatakuwa ya amani

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Muktasari:

  • Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa mchakato wa makabidhiano ya madaraka kwa utawala mpya yanaendelea huku akisisitiza kuwa yatakuwa ya amani.

Dar es Salaam. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema mchakato wa makabidhiano ya madaraka kwa utawala mpya yanaendelea huku akisisitiza kuwa yatakuwa ya amani.

Katika hotuba yake ambayo ameitoa leo Jumatatu Septemba 5, 2022 jioni baada ya Mahakama ya Juu kuthibitisha matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais mteule William Ruto, Rais Kenyatta amesema maagizo yote ya kuwezesha mchakato huo wa kukabidhiana madaraka yameshatolewa.

"Nia yangu ni kusimamia makabidhiano ya amani kwa utawala ujao na maagizo yote muhimu ya kuwezesha mchakato huu tayari yametolewa" amesema Kenyatta wakati akitoa hutuba yake ya kwanza hadharani tangu uchaguzi ufanyike.

Rais huyo ambaye wakati wa kampeni za uchaguzi huo uliofanyika Agosti 9 mwaka huu alikuwa anamuunga mkono Odinga, amesema anaheshimu uamuzi wa Mahakama ya Juu wa kuidhinisha ushindi wa Ruto kama Rais mteule.

 “Nilipoapishwa kuwa Rais, niliahidi kuheshimu sheria. Leo Jumatatu Mahakama ya Juuu imeidhinisha matokeo ya urais kama yalivyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Ninaheshimu uamuzi wa Mahakama” amesema

Wakati wa hotuba yake, Rais Kenyatta hakumtaja kwa jina Rais mteule William Ruto wala kumpongeza kwa ushindi wake lakini aliwapongeza Wakenya kwa kudumisha amani wakati wote wa mchakato wa uchaguzi na wakati matokeo yalipopingwa mahakamani.

Katika matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati Agosti 15, 2022, Dk William Ruto alishinda kwa kura 7,176,142 (asilimia 50.49 ya kura) na Raila Odinga akafuatia kwa kura 6, 942, 930 (asilimia 48.85). wangombea wengine wawili hawakufikisha asilimia moja ambapo David Waihiga alipata asilimia 0.23 % huku George Wajackoyah akipata asilimia 0. 44.

Baada ya Chebukati kutangaza matokeo hayo yaliyompa ushindi Ruto, Odinga aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja na mgombea mwenza wake, Martha Karua walifungua kesi katika Mahakama ya Juu kupinga ushindi wa Ruto.

Leo mchana akitoa uamuzi wa hukumu hiyo ya kesi ya kupinga matokeo hayo, Jaji Mkuu Martha Koome alisema Raila na waleta maombi wenzake wameshindwa kuthibitisha kuwa kulikuwa na udanganyifu na uchakachuaji wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi, siku na baada ya kupiga kura.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, Ruto akizungumza na waandishi wa habari aliweka wazi kuwa kuwa hajazungumza na Kenyatta kwa miezi sasa huku akiahidi kuwa atampigia simu wazungumze.

“Nina miezi sasa sijazungumza naye lakini nitampigia rafiki yangu Rais Uhuru Kenyatta tuzungumze” alisema Ruto huku akicheka

Kwa upande wa timu ya mawakili wa Ondinga walisema wameupokea lakini hawaukubali uamuzi wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo iliyotupilia mbali maombi yao ya kupinga matokeo ya uchanguzi uliompa ushindi William Ruto.

Kiongozi wa jopo la mawakili Ondinga, wakili mwandamizi James Orengo aliwaambia waandishi wa habari muda mfupi baada ya uamuzi huo kuwa uamuzi wa mahakama hiyo ulikuwa wa kiitikadi zaidi kuliko kisheria.

“Kwa mujibu wa sheria tunalazimika kuupokea huu uamuzi lakini nadhani ulikuwa wa kiitikadi zaidi. Tunaupokea lakini hatukubaliani nao,” alisema Orengo.