Raia wa kigeni 7,000 wanaofanya biashara ndogondogo wakamatwa

Muktasari:
- Hatua ya kukamatwa kwa raia hao, imetokana na uchunguzi wa miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu, katika mikoa yote nchini.
Dar es Salaam. Baada ya kilio cha wafanyabiashara kuhusu kuwepo kwa raia wa kigeni wanaofanya biashara ndogondogo nchini Tanzania, Idara ya Uhamiaji limewakamata raia 7,069 wanaofanya shughuli hizo.
Hatua ya kukamatwa kwao, kwa mujibu wa idara hiyo, imetokana na uchunguzi wa miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili 2025, katika mikoa yote nchini.
Hata hivyo, uchunguzi wa idara hiyo ulitanguliwa na ripoti ya kamati ya kufuatilia na kuhakikisha raia wa kigeni hawajihusishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa maeneo ya Kariakoo iliyoongozwa na Profesa Edda Lwoga.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika eneo la Kariakoo pekee, maduka 75 yalikutwa na raia wa kigeni 152 walioajiriwa, huku asilimia 97 wakijihusisha na biashara za rejareja.
Hadi kamati hiyo inaundwa, Februari 5, 2025 kulikuwa na malalamiko kutoka wa wafanyabiashara katika soko hilo na maeneo mengine kuhusu kuwepo kwa raia hao.
Mjadala kuhusu hilo, uliibukia hadi bungeni na msisitizo uliwekwa katika kufanya uchunguzi na kuwabaini raia hao ili kuhakikisha biashara nchini zinafanywa kwa ushindani.
Taarifa ya kukamatwa kwa raia hao, imetolewa leo, Alhamisi Aprili 24, 2025 na Msemaji wa Uhamiaji, Paul Msele.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kati ya waliokamatwa 1,008 wamefikisha mahakamani, huku 703 wamehukumiwa kifungo gerezani na 257 wamehalalisha ukazi wao.
Taarifa hiyo, inaeleza wengine 4,796 wameondoshwa nchini na watuhumiwa 305 uchunguzi bado unaendelea.
"Sambamba na hilo, Idara ya Uhamiaji kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama wamefanya ukaguzi maalumu katika eneo la Kariakoo," imeeleza.
Imesema katika ukaguzi huo, jumla ya raia wa kigeni 62 kutoka katika mataifa mbalimbali wamekamatwa na kuondoshwa nchini kwa kosa la kuishi na kufanya biashara bila ya vibali na baadhi yao kukiuka masharti yaliyoanishwa katika vibali vyao vya biashara.
"Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa raia wa kigeni kuzingatia matakwa ya masharti ya vibali vyao ili kuepuka hatua za kisheria au usumbufu unaoweza kujitokeza wakati huu ambapo zoezi la ukaguzi linaendelea," inasomeka taarifa hiyo.