Raia wa Kenya kortini kwa kuishi nchini bila kibali

Muktasari:
- Raia wa Kenya, Abdulkarim Makiadi (28) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kuwepo nchini Tanzania kinyume cha sheria.
Dar es Salaam. Raia wa Kenya, Abdulkarim Makiadi (28) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kuwepo nchini Tanzania kinyume cha sheria.
Hata hivyo, alipoulizwa na hakimu kuhusu uraia wake, amesema ni raia wa Musoma.
Mshtakiwa amefikishwa mahakamani hapo Alhamisi Septemba 21, 2023 na kusomewa shtaka lake na wakili wa Serikali Grace Nyalata, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya.
Akimsomea shtaka lake, wakili Nyalata amedai Septemba 16, 2023 katika eneo la Jangwani lililopo Wilaya ya Ubungo, mshtakiwa akiwa raia wa Kenya alipatikana akiishi nchini kinyume cha sheria.
Mshtakiwa anadaiwa kuwa alikutwa akiishii nchini bila kuwa na kibali Wala nyaraka inayoonyesha uhalali wa kuishi nchini.
Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake, alikana kutenda kosa lake.
"Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa kesi hii umekamilika hivyo, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali (PH) na kisha kuanza kusikiliza ushahidi" Amedai Wakili Nyalata.
Upande wa mashtaka baada ya kueleza hayo, hakimu Mbuya alimuuliza mshtakiwa baadhi ya maswali na ifuatayo ni sehemu ya mahojiano yao.
Hakimu: Wewe ni raia wa wapi?
Mshtakiwa: Raia wa Musoma.
Hakimu: Mhh Musoma?
Hakimu: Kwani Musoma ni nchi?
Mshtakiwa: Ndio
Hakimu: Unakaa mkoa gani?
Mshtakiwa: Mkoa wa Musoma.
Hakimu: Kijiji gani?
Mshtakiwa: Siani
Hakimu: Unakufahamu vizuri Musoma?
Mshtakiwa: Ndio
Hakimu: Musoma wanakaa kabila gani?
Mshtakiwa: Wapare na Wajaluo.
Hakimu: Wewe ni kabila gani?
Mshtakiwa: Mjaluo
Hakimu: Ukiwa unatoka Dar es Salaam kwenda Musoma unapita mikoa gani? Hebu nitajie
Mshtakiwa: Morogoro, Mkoa wa Chalinze, Dodoma, Singida, Shinyanga, Mwanza, unaenda upande wa Tarime halafu Mwanza, Musoma halafu mkoa mwingine wa Tarime.
Hakimu: Tarime? Hebu tuambie ukitoka Tarime unaenda wapi?
Mshtakiwa: Mheshimiwa hapo nimechanganya.
Hakimu: Halafu umekosea, ukitoka Dar unaenda mkoa wa Pwani, wewe Pwani hujaitaja.
Mshtakiwa: Niliitaja Chalinze.
Hakimu: Chalinze sio mkoa.
Hakimu: Halafu hakuna mkoa unaitwa Musoma.
Hakimu: Nitajie wilaya zinazopatikana mkoa wa Mara ni zipi?
Mshtakiwa: Tarime, Simiyu, Rorya.
Hakimu: Hivi hapa Dar es Salaam unaishi wapi na unaishi na nani?
Mshtakiwa: Naishi Kimara Baruti na ninaishi na mke wangu.
Hakimu: Mke yupo hapa mahakamani?
Mshgakiwa: Ndio
Mke wake anasimama mahakamani na kukiri kuwa Makiadi ni mume wake.
Hakimu: Wewe unaishi wapi (mke wa Makiadi)?
Mke wa Makiadi: Nakaa Kimara Baruti.
Hakimu: Wewe ni kabila gani?
Mke wa Makiadi: Mhehe
Hakimu: Mume wako yeye kabila gani?
Mke wa Makiadi: Mjaluo
Hakimu: Umeshafika kwao?
Mke wa Makiadi: Ndio nilifika mara moja kwa bibi yake anaishi Kisumu.
Hakimu: Wazazi wake wapo?
Mke wa Makiadi: Walishafariki, hivyo mume wangu alilelewa na bibi yake
Hakimu: Huyo bibi yake anakaa wapi Kisumu sehemu gani?
Mke wa Makiadi: Bibi yake aliolewa na Mjaluo tu, yeye ni mchaga wa Moshi
Hakimu: Moshi sehemu gani?
Mke wa Makiadi: Kimya
Hakimu: Eti Makiadi? bibi yako anakaa Moshi sehemu gani?
Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu mimi Moshi nilienda kufanya biashara.
Hakimu: Shule ya msingi ulisoma wapi?
Mshtakiwa: Manyati, ipo Kisumu.
Hakimu: Mama yako alikuambia umezaliwa wapi?
Mshtakiwa: Mimi nimelelewa na bibi tu, sijakaa na mama yangu.
Baada ya maswali hayo, Hakimu Mbuya alitaja masharti ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo, ambapo mshtakiwa ametakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayetambulika kisheria atakayesaini bondi ya Sh300,000.
Hata hivyo, mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kurudishwa rumande.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 2, 2023 kwa ajili ya maelezo ya awali.