Profesa Ndakidemi alia na askari wa Kinapa

Muktasari:
Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amesema askari wa hifadhi ya mlima Kilimanjaro (KINAPA) wamekuwa wakikiuka haki za kibinadamu kwa kuwafanyia matendo maovu wananchi pindi wanapowakuta katika eneo hilo kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo kukata majani ya mifugo au kuokota kuni kavu.
Moshi. Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amedai kuwa askari wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) wamekuwa wakikiuka haki za kibinadamu kwa kuwafanyia matendo maovu wananchi pindi wanapowakuta katika eneo hilo kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo kukata majani ya mifugo au kuokota kuni kavu.
Akichangia kwenye kikao cha baraza la madiwani Ndekidemi amesema Kinapa wamekabidhiwa kusimamia eneo la Nusu maili na kwamba makubaliano yalikuwa wakinamama wataruhusiwa kuingia eneo hilo kukata majani ya mifugo pamoja na kuokota kavu lakini kwa sasa askari hao wanapowakuta wakinamama hao wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya ukatili.
"Kitendo cha askari wa Kinapa kuwapiga, kuwatesa huku wangine wakifariki dunia kutokana na mateso wanayoyapata sio jambo nzuri hivyo serikali inatakiwa kuangalia kwa jicho la pili ikiwa ni pamoja na kuruhusu wananchi kufanya shuguli za kawaida kama kuokota kuni na kukata majani katika hifadhi hiyo" amesema Prof. Ndakidemi.
Akisoma mapendekezo ya madiwani, diwani wa kata ya Uru Shimbwe, Bertin Mkami amesema kuwa, kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi ya mlima Kilimanjaro.
Mkami amesema kuwa, eneo hilo la Nusu maili wananchi walikuwa wakilitumia kwa ajili ya ukataji majani ya mifugo, kuokota kuni kavu, kusafisha mifereji ya maji, bomba, dawa za asili pamoja na mawasiliano ya njia za kutoka kijiji kimoja kwenda kingine.
"Kumekuwepo pia na migogoro kuhusiana na mpaka mpya katika baadhi ya vijiji na wananchi ndio walinzi wazuri wa kutunza kuendeleza kulinda na kutumia rasilimali za misitu bila kuathiri mazingira" amesema Mkami.
Amesema kuwa, wananchi wakipewa haki ya kusimamia eneo la nusu maili watalitunza vema kwa sababu watathamini umuhimu wa eneo hilo kwani kinyume na hapo watalazimika kuingia ndani ya hifadhi kutafuta mahitaji ya msingi kwa kuwa hawana eneo mbadala la kukimbilia.
"Dhana ya ujirani mwema imeingia hitilafu baada ya wananchi kukatazwa kuingia katika eneo la nusu maili hali ambayo inaweza kupelekea wananchi kususia kushiriki baadhi ya shughuli zikiwemo uzimaji wa moto hifadhini ama kuficha taarifa muhimu za wahalifu na wahujumu wa maliasili" amsesema
Akijibu hoja za madiwani Mhifadhi Mwandamizi hifadhi ya Kinapa, Charles Ngendo amesema kuwa wao wanasimamia eneo la nusu maili kwa mujibu wa maelekezo kutoka serikalini.
Ngendo amesema kuwa askari wa Kinapa wamekuwa wakiwasisitiza kufuata sheria na kanuni hali ambayo kwa sasa imepelekea kupungua kwa malalamiko ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu kutoka kwa wananchi.
"Katika kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) mwaka 2014 kulikuwa na makubaliano ya kuwaruhusu wakinamama kulitumia eneo la nusu maili kukata majani ya mifugo pamoja na kuokota kuni kavu lakini kwa sasa shughuli hizo haziruhusiwi tena" amesema Ngendo.