Profesa Kitila arejea baraza la mawaziri

Profesa Kitila Mkumbo
Muktasari:
- Mabadiliko hayo yamekuja miezi mitano, tangu Rais Samia alipoeleza nia ya kuunda Tume ya Mipango alipokuwa akiwaapisha viongozi aliowateua Ikulu ya Chamwino Dodoma Februari 27 mwaka huu.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameunda Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na amemteua Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo kuiongoza wizara hiyo.
Profesa Kitila amewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Wizara ya Viwanda na Biashara na Katibu Mkuu Wizara ya Maji.
Kutokana na mabadiliko hayo, Rais Samia ameivunja Wizara ya Fedha na Mipango na kuunda Wizara ya Fedha ambayo Dk Mwigulu Nchemba ataiongoza.
Kabla ya hapo Dk Mwigulu alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Uteuzi huo uliotangazwa leo Julai 5 na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, umekuja kufuatia kutungwa kwa Sheria ya Mipango ya Taifa ya Mwaka 2023 pamoja na uamuzi wa kuhamishia masuala ya uwekezaji Ofisi ya Rais.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa Rais ameunda Wizara ya Viwanda na Biashara na amemteua aliyekuwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa wizara hiyo.
“Amemteua Laurence Mafuru kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa. Kabla ya uteuzi huo, Mafuru alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango (usimamizi wa uchumi).
“Amemteua pia Elijah Mwandumbya kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha (usimamizi wa uchumi), kabla ya uteuzi huo Mwandumbya alikuwa Kamishna, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha na Mipango.
Mabadiliko hayo yamekuja miezi mitano, tangu Rais Samia alipoeleza nia ya kuunda Tume ya Mipango.
Februari 27 mwaka huu, akiwaapisha viongozi aliowateua Ikulu ya Chamwino Dodoma, Rais Samia alisema, "Kwa sasa tunaleta, Msajili wa Hazina, Tume ya Mipango na Uwekezaji zinakuja chini ya Rais.
“Tutakuwa na waziri wake na naibu waziri wake, tukimaliza mchakato wa sheria itakuwa wizara kamili. Kwa sasa tumetanguliza katibu mkuu atusaidie kupanga, tunafanyaje wanakaaje, mambo ya uchumi, uchumi mkubwa na mdogo tunafanyaje atusaidie kupanga.”
Aprili 20, wabunge walitaka irejeshwe tume ya Taifa ya Mipango.
Juni 8 Serikali Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene aliwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango wa mwaka 2023 na ulipitishwa siku hiyo hiyo.
Pamoja na mambo mengine, tume hiyo itakuwa na jukumu la kubuni, kupanga, kuratibu na kusimamia mipango ya maendeleo ili kuwa na mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathimini ya utekelzaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.