Polisi yawaonya wanasiasa uchaguzi wa kesho

Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya
Muktasari:
Uchaguzi wa udiwani katika kata 77 na jimbo la Buyungu, Kakonko utafanyika kesho nchini.
Mtwara. Jeshi la polisi mkoani Mtwara limewaonya wanasiasa wanaofanya mikusanyiko isiyo halali kwa madai ya kulinda kura katika uchaguzi mdogo unaotegemewa kufanyika kesho Jumapili.
Uchaguzi wa udiwani katika kata 77 na jimbo la Buyungu, Kakonko utafanyika kesho nchini.
Akizungumza leo Agosti 8 Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya amesema jeshi hilo limejipanga na lina askari wa kutosha kutuliza ghasia.
Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya kidemokrasia na kumchagua kiongozi wanayemtaka.
“Tunazo taarifa baadhi ya vyama vya siasa wamejipanga kufanya mikusanyiko isiyo halali katika vituo vya kupiga kura kwa kile wenyewe wanachokiita kulinda kura zao zisiibiwe, tunawakumbusha kazi ya kulinda usalama wa raia na mali zao ni jukumu la jeshi la polisi na sio mtu mwingine,” amesema
Amesema hata kazi ya kulinda wananchi wakati wakipiga kura ni kazi ya jeshi hilo na si vinginevyo.
Pia amewaomba wananchi kurudi nyumbani mara baada ya kumaliza kupiga kura na waendeleze utulivu wakisubiri matokeo.
“Tutatakuwa na askari wengi sana katika vituo vyote vinavyotarajiwa kupigwa kura, kwa hiyo mtu yeyote asijipe jukumu hilo, hivyo vyama vinavyojipanga kutekeleza jukumu la polisi hatujaomba msaada sisi,” amesema
Amesema polisi wana askari wa kutosha kuweza kusimamia uchaguzi.
Uchaguzi wa madiwani Mtwara, utafanyika katika kata tatu za Makonga, Nanguruwe na Nalingu.