Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi yaonya watoto chini ya miaka 12 kupandishwa bodaboda

Kamanda wa Usalama Barabarani Wilaya ya Kipolisi Kawe/Mbweni, Adriano Kamarai, akitoa elimu kuhusu usalama barabarani kwa maofisa usafirishaji leo Julai 25, 2026, jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Onyo hilo limetolewa kutokana na kuendelea kushuhudiwa kwa madereva wa bodaboda wakiwasafirisha watoto wadogo wasiokuwa na uwezo wa kujishikilia vizuri wanapokuwa kwenye pikipiki, hali inayowaweka katika hatari ya kuanguka na kupata majeraha.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limewataka madereva wa bodaboda kuacha kuwapakiza watoto wenye umri chini ya miaka 12 kwa kuwa hatua hiyo ni hatari na inakiuka misingi ya usalama barabarani, huku likionya kuwa tabia hiyo imekuwa ikichangia ajali zinazohusisha watoto.

Onyo hilo limetolewa kutokana na kuendelea kushuhudiwa kwa madereva wa bodaboda wakiwasafirisha watoto wadogo wasiokuwa na uwezo wa kujishikilia vizuri wanapokuwa kwenye pikipiki, hali inayowaweka katika hatari ya kuanguka na kupata majeraha.

Akizungumza leo Jumamosi, Julai 25, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa semina ya elimu ya usalama barabarani iliyoandaliwa na Chama cha Usalama na Afya Mahala pa Kazi Tanzania (Tohasa) kwa maofisa usafirishaji wa bodaboda eneo la Tangibovu jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Usalama Barabarani wa Wilaya ya Kipolisi Kawe/Mbweni, ASP Adriano Kamarai amesema kisheria, mtoto anayepaswa kupanda bodaboda ni mwenye miaka 12 na kuendelea.

“Kwa umri huo (12) mtoto huwa na uwezo wa kujimudu akiwa kwenye pikipiki kwa kujishikilia vizuri, anaweza kuvaa vifaa kinga kama kofia ngumu, tofauti na watoto wadogo ambao uwezo wao wa kujikinga huwa mdogo,” amesema.

Maofisa usafirishaji, wawakilishi wa Tohasa na Kamanda wa Usalama Barabarani Wilaya ya Kipolisi Kawe/Mbweni, Adriano Kamarai, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya semina ya elimu ya usalama barabarani iliyofanyika leo Julai 25, 2026, jijini Dar es Salaam.

Mbali na kutoa elimu hiyo, Kamarai amewataka madereva bodaboda kuzingatia sheria zote za usalama barabarani sambamba na matumizi ya vifaa vya kinga kama reflector, miwani ya kuzuia upepo, kofia ngumu na viatu vinavyofaa wanapokuwa kazini.

Pia, amewataka kuheshimu alama za wavuka kwa miguu (zebra), akisema ajali nyingi hutokea pale madereva bodaboda wanapovunja sheria kwa kupita wakati magari mengine yamesimama kupisha watembea kwa miguu.

"Maafisa usafirishaji zingatieni sheria za usalama barabarani, hususan alama za wavuka kwa miguu. Msipite katikati ya vyombo vingine vya usafiri, baki katika njia yako. Pia pikipiki inatakiwa kubeba abiria mmoja tu, si wawili, na vaeni viatu mnapoendesha," amesema Kamarai.

Katika semina hiyo, washiriki wamekabidhiwa vifaa vya kujikinga wakiwa barabarani, sambamba na stika zenye ujumbe wa usomekao 'Kuwa Makini, Okoa Maisha.'

Kwa upande wake, Rais wa Tohasa, Caroline Baraza amesema takwimu kutoka hospitalini zinaonesha ongezeko la majeruhi wanaotokana na ajali za bodaboda, huku nyingi zikichangiwa na uzembe wa madereva.

Amesema kutokana na hali hiyo, chama hicho kimeamua kutoa elimu ya usalama barabarani kwa maofisa usafirishaji ili kuwajengea uwezo wa kuendesha kwa kufuata sheria na hivyo kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika.

"Ajali nyingi za barabarani kwa sasa zinahusisha bodaboda. Matokeo yake ni vifo, ulemavu wa kudumu na kupungua kwa nguvu kazi ya taifa. Ndiyo maana tumetoa elimu pamoja na vifaa vya kinga vitakavyowasaidia wanapokuwa barabarani," amesema Caroline.

Naye Mwenyekiti wa Kituo cha Bodaboda Tangibovu, Athuman Kitunguru amesema baadhi ya madereva hulazimika kuvuka alama za zebra bila kusimama kwa kuhofia kugongwa na magari yanayokuwa nyuma yao wanaposimama ghafla, ingawa amekiri kuwa kitendo hicho ni ukiukaji wa sheria za usalama barabarani.

Amesema madereva wa bodaboda hukumbana na changamoto ya kunyanyaswa na baadhi ya madereva wa magari makubwa na daladala, hali inayochangia kutokea kwa ajali.

Hata hivyo, amesema elimu wanayoendelea kuipata kutoka kwa maofisa wa usalama barabarani, imechangia kupunguza matukio ya madereva wa bodaboda kujichukulia sheria mkononi baada ya wenzao kupata ajali.

Hivyo, amewahakikishia waandaaji wa semina hiyo kuwa madereva wa bodaboda wataitumia elimu waliyoipata kuboresha uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani na kulinda usalama wao pamoja na wa watumiaji wengine wa barabara.