Polisi yaanika uchunguzi dhidi ya aliyekuwa RC Simiyu

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda.
Dar/Mwanza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema Jeshi hilo leo Julai 5, 2024 lilipokea taarifa za uchunguzi wa vielelezo kuhusu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda, anayedaiwa, kumlawiti mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Mwanza, Tumsime Ngemela.
Alisema taarifa hizo walizipokea kutoka maabara za uchunguzi wa kisayansi.
Kamanda Mutafugwa amesema hayo saa chache baada ya Tumsime mwenye miaka 21 akiwa ofisi za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), jijini Dar es Salaam, kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo, akiomba msaada wa Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ili haki itendeke.
Kamanda Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari amesema: “Kama ilivyo katika uchunguzi wa makosa ya jinai likiwamo na hili, jalada lazima lifike Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali.”
“Jalada hili lilishafikishwa katika Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali na taarifa hiyo ya uchunguzi wa vielelezo hivyo kutoka maabara ya uchunguzi wa kisayansi ambazo nimesema tumezipata leo na zenyewe zinafungashwa kumpelekea Mkuu wa Mashtaka wa Mkoa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria,” amesema.
Kamanda Mutafungwa aliyekiri kuona mahojiano ya binti huyo akieleza tukio zima lilivyotokea, amemtoa hofu akimuahidi uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa ukaribu, umakini na weledi mkubwa.
"Nipende kumtoa hofu binti huyo nakumhakikishia uchunguzi makini na wenye weledi unaendelea, na kupitia hayo atapata haki yake ambayo atastahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, uchunguzi wa matukio hayo hauhusishi polisi peke yake.
“Tunachunguza wengi... lakini katika hatua hizi tutarajie kuanzia Jumatatu Ofisi ya Mashtaka ya Mkoa itatoa mwongozo wa hatua zinazochukuliwa,” amesema.
Amesema kwa sasa Dk Nawanda yupo nje kwa dhamana, akieleza dhamana ni haki ya mtuhumiwa wa kosa kama lake kwa mujibu wa sheria na kwamba, anaripoti ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Mwanza.
Alichosema Tumsime
Katika mkutano na wanahabari, Tumsime ameeleza anapitia changamoto kadhaa, ikiwamo kulazimika kuhamahama makazi baada ya kuripoti polisi tukio hilo siku 34 zilizopita.
Kutokana na changamoto hizo, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo ili haki itendeke.
Msichana huyo, ambaye ni mwanafunzi wa chuo kimoja jijini Mwanza amedai baada ya tukio hilo la Juni 2, 2024 lililotokea kwenye gari dogo alilodai ni la Dk Nawanda alitoa taarifa polisi na baadaye akaenda hospitali.
“Nikapigiwa simu na mmoja wa viongozi wa Mkoa wa Mwanza akaniambia anahitaji kuniona, nikamwambia siwezi kuja nipo na polisi, akasema wape simu, akaongea nao na kuniamuru wanipeleke ofisini kwake,” amedai.
Amedai katika mazungumzo ofisini kwa kiongozi huyo alimtaka afute kesi, suala ambalo pia alidai Dk Nawanda alimtaka afanye hivyo ili limalizwe kifamilia.
Kutokana na kesi hiyo anadai askari wa ngazi ya juu, aliamuru atafutiwe eneo jingine la kuishi kwa ajili ya usalama wake kwa kuwa alikuwa akipigiwa simu akitakiwa kufuta kesi.
Akizungumzia barua ya kufuta kesi iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Tumsime alisema alipelekewa iliyoandikwa na kutakiwa kuandika upya kwa kunakili yaliyoandikwa.
Baada ya kunakili alidai aliweka saini ya kidole gumba na ikapelekwa polisi.
Tumsime ameoimba Serikali kulifikisha suala hilo mahakamani ili haki itendeke kwa kila mtu.
“Kama ninamsingizia, nipewe adhabu kwa hili, lakini kama Dk Nawanda amenifanyia makosa haki itendeke. Inavyocheleweshwa haifiki mahakamani, kila mtu atakuwa na tafsiri au maoni tofauti kuhusu tukio hili,” amesema.
Kwa nyakati tofauti Mwananchi limekuwa likiandika habari kuhusu sakata hili, huku wanasheria na wadau wa haki za binadamu waliohojiwa, wakiisihi Serikali kuharakisha upelelelezi ili jambo hilo lifikishwe mahakamani.
Kutokana na tukio hilo amedai amesitisha masomo.