Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi wasimulia kichwa cha mwanafunzi IFM kilivyopatikana

Muktasari:

  • James Temba, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha IFM, alizikwa Mei 7, 2026 katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Mande, Kata ya Old Moshi Magharibi, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro bila kichwa.

Dar es Salaam. Siku sita baada ya kuzikwa kwa kiwiliwili cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), James Temba, hatimaye kichwa chake kimepatikana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Mei 13, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ameeleza kuwa kichwa hicho kimepatikana katika eneo la Kitunda Kibeberu, Ilala jijini Dar es Salaam kikiwa kimefukiwa ardhini.

“Sehemu ya kichwa hiki kimekutwa kimefukiwa ardhini na waliotekeleza uhalifu ule, jumla ya watuhumiwa watano wanashikiliwa akiwemo mtu mwingine ukiacha wale niliowapa taarifa zao Mei 3, mwaka huu, ameongezeka mwingine aliyefahamika kama Said Ally mwenye umri wa miaka 31 maarufu Side ambaye ni mganga wa kienyeji,” amesema.

Kamanda huyo amesema taratibu za kisheria zinakamilishwa ili mamlaka zingine za kisheria ziweze kuendelea na hatua zingine.

Awali, akizungumza kwa njia ya simu, Rogers Temba ambaye ni baba mzazi wa marehemu amesema licha ya kuwa bado yuko Moshi, lakini amesikia tetesi za kupatikana kwa kichwa hicho na polisi bado wanamalizia kazi yao.

“Wamekipata kwa tetesi za awali katika eneo la Kitunda Kibeberu (Ilala jijini Dar es Salaam),” amesema mzee huyo kwa njia ya simu.

Mwili wa mwanafunzi huyo ulizikwa  Mei 7, 2026 katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Mande, Kata ya Old Moshi Magharibi, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, mwili wake ukiwa hauna kichwa, hivyo waombolezaji waliokuwepo kwenye mazishi hayo wakilazimika kuaga picha iliyowekwa kwenye jeneza lake.

Temba, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha IFM, aliondoka nyumbani kwao Aprili 29 mwaka huu na baadaye mwili wake kukutwa katika mto huo, ukielea ndani ya maji huku ukiwa umekatwa kichwa.

Mwili wa Temba ambaye ni mkazi wa Tabata Chang'ombe jijini Dar es Salaam ulikutwa ukielea kwenye maji yaliyokuwa yanatiririka Mto Msimbazi eneo la Kipawa Ilala Aprili 30, 2026 huku ukiwa hauna kichwa.

Amesema kwa sasa taratibu zinaendelea kufanyika za kipelelezi na kisheria na pindi zikikamilika na wakakabidhiwa kichwa hicho watarudisha Moshi sehemu ambapo mwili wa James ulipumzishwa bila kichwa.

Amesema watakapofika Moshi hawatalazimika kufukua kaburi kwani wakati wanazika waliacha sehemu ya dharula baada ya kuwaza nini kingefanyika baada ya kichwa kupatikana.

“Hivyo tuliacha eneo dogo kabla ya zege kumwagwa ambalo lingetumika ikiwa kichwa kingepatikana.

“Kiukweli, tunawashuruku ndugu jamaa na marafiki kwa kushirikiana nasi tangu mwanzo tulipopata taarifa hizi, hadi kumpumzisha kijana wetu kwani watu wengi walitukimbilia kutoka sehemu mbalimbali na tulipopata taarifa ya kupatikana kichwa hiki tumefarijika kwa sababu mtoto anapozikwa hana kichwa unakuwa na mawazo zaidi,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kulishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada waliowapatia sambamba na vyombo vya habari ambavyo vilisaidia upatikanaji wa taarifa hizo.

“Jambo hili lilituumiza siyo kidogo kwani si kitendo cha kawaida ni aghalabu kutokea ila vingine viko nje ya uwezo wako na hauna budi kupokea. Sasa tunasubiri Serikali wakamilishe taratibu zao ndiyo tukabidhiwe,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kuendelea kumuombea ili wapate nguvu katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.

Hili linatokea wakati ambao Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi huyo.

Taarifa ya Polisi iliwataja wanaoshikiliwa ni Steven Chaka (31), ofisa maabara Mkazi wa Bomang'ombe, Wilaya ya Hai, Kilimanjaro. Mwingine ni Anna Lema (30), Mkazi wa Mkazi wa Tabata Chang'ombe ambaye pia ni mfanyabiashara.

Wengine ni Twalibu Khamis (23), mkazi wa Kigogo Kati, Michael John (26), mkazi wa Kigogo Kati na Said Ally mwenye umri wa miaka 31 maarufu Side ambaye ni mganga wa kienyeji.