Mwanafunzi IFM azikwa bila kichwa kijijini kwao, mama mzazi atoa ujumbe
Muktasari:
- Mwili wa mwanafunzi huyo wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) umezikwa leo Mei 7, 2026 katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Mande, Kata ya Old Moshi Magharibi, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro ukiwa hauna kichwa.
Moshi. Aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), James Temba aliyeuawa na mwili wake kukutwa ukielea katika Mto Msimbani, eneo la Baracuda jijini Dar es Salaam, umezikwa katika makaburi ya familia kijijini kwao Mande, Moshi mkoani Kilimanjaro, huku mama mzazi akitoa ujumbe kutoka Zaburi ya 35 kwa yeyote aliyehusika na tukio hilo.
Mwili wa mwanafunzi James Temba (24) aliyeuawa kwa kukatwa shingo na mwili wake kukutwa unaelea katika Mto Msimbazi, jiijini Dar es Salaam James Temba ukiwa umewasili leo Alhamisi Mei 7, 2026 katika Kijiji cha Mande, Kata ya Old Moshi Magharibi, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
"James nakuachia Zaburi ya 35 inene nawe huko kaburini! Usinyamaze huko kaburini! James wamekuwa vibaya," haya ni baadhi ya maneno ya Eugenia Temba, mama mzazi wa marehemu mwanafunzi huyo.
Mwili wa mwanafunzi James Temba (24) aliyeuawa kwa kukatwa shingo na mwili wake kukutwa unaelea katika Mto Msimbazi, jiijini Dar es Salaam James Temba ukiwa umewasili leo Alhamisi Mei 7, 2026 katika Kijiji cha Mande, Kata ya Old Moshi Magharibi, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Maneno ya mama huyo aliyokuwa akiyatamka wakati mwili wa mwanaye ukiingizwa kaburini yaliwaumiza na kuwaliza waombolezaji waliokuwa kwenye mazishi hayo, huku baadhi yao wakiangua vilio.
Eugenia Temba, Mama mzazi wa aliyekuwa mwanafunzi wa chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) aliyeuawa kwa kukatwa kichwa na mwili wake kukutwa ukiwa unaelea ndani ya maji mto msimbazi Jijini Dar es salaam ukiwa hauna kichwa akimuaga mwanaye wakati mwili wake ukishushwa kaburini katika Kijiji cha Mande, kata ya Old Moshi Magharibi, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Mwili wa mwanafunzi huyo wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) umezikwa leo Mei 7, 2026 katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kijiji cha Mande, Kata ya Old Moshi Magharibi, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, mwili wake ukiwa hauna kichwa, hivyo waombolezaji waliokuwepo kwenye mazishi hayo wakilazimika kuaga picha iliyowekwa kwenye jeneza lake.
Temba, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha IFM, aliondoka nyumbani kwao Aprili 29 mwaka huu na baadaye mwili wake kukutwa katika mto huo, ukielea ndani ya maji huku ukiwa umekatwa kichwa.
Mei 3 mwaka huu, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilithibitisha kifo cha Temba na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho, na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Eugenia Temba, Mama mzazi wa aliyekuwa mwanafunzi wa chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM)aliyeuawa kwa kukatwa kichwa na mwili wake kukutwa ukiwa unaelea ndani ya maji mto msimbazi Jijini Dar es salaam ukiwa hauna kichwa akimuaga mwanaye wakati mwili wake ukishushwa kaburini katika Kijiji cha Mande, kata ya Old Moshi Magharibi, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Akihubiri katika ibada ya mazishi ya mwanafunzi huyo, Mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kanda ya Kaskazini, Anorld Swai, ameitaka jamii kuwa na hofu na kumrudia Mungu kutokana na matukio ya ukatili yanayoendelea hivi sasa.
"Tunaishi katika wakati ambao chuki, mioyo yenye mambo mengi mabaya yenye siri nyingi katika jamii, imefika mahali kuliko ukutane na binadamu bora ukutane na mnyama," amesema mwinjilisti huyo.
Amesema katika kipindi hiki ambacho watu wamekuwa na roho ya ukatili, chuki na roho mbaya, ni kipindi ambacho jamii inapaswa kumrudia Mungu.
"Tunamhitaji sana Mungu kuishi katika majira haya ambayo watu wamekuwa na roho mbaya. Imefika mahali binadamu hana huruma tena, tumekuwa na roho ambazo zimejaa hila mbaya. Mtu wa leo kuua imekuwa ni kitu cha kawaida. Watanzania tumevamiwa na roho ambayo siyo ya kawaida, Mungu atusaidie tubadilike," amesema Mwinjilisti huyo.
Akitoa salamu za rambirambi, Diwani wa Kata ya Old Moshi Magharibi, Rayson Massawe, amesema tukio hilo ni la kuumiza na lenye kuacha majeraha katika jamii.
"Tulipokea msiba wa ndugu yetu huyu kwa masikitiko na majonzi makubwa kwa kuondokewa na mtoto wetu mpendwa. Nimekuja hapa kuwafikishia salamu za pole kwani hapa kwenye kijiji chetu kuna misiba mingine minne," amesema diwani huyo.
Wanafunzi IFM walaani mauaji ya mwenzao
Akitoa salamu za chuo hicho, mwanafunzi Justine Masanja amelaani vikali tukio hilo na kusema ni tukio ambalo limeacha majeraha waomboleza na chuo hicho kwa ujumla.
Waombolezaji, ndugu na marafiki wakiendelea na ibada ya kuaga mwili wa James Temba.
"Tunatoa pole sana kwa familia ya James, kama chuo tulihuzunishwa na tukio hili kutokea katika nchi yetu, hasa kwa kijana ambaye alikuwa na ndoto nyingi za hapo baadaye, tutamkumbuka kwa mazuri yake," amesema mwanafunzi huyo.
Amesema, "Tumefika kumsindikiza mwenzetu katika safari yake ya mwisho lakini mpaka sasa hatuamini kama ni kweli, tukio kama hili siyo zuri kwa nchi yetu kutokea."
Mwanafunzi mwingine, Martine Shoo amesema watamkumbuka kwa kuwa alikuwa ni mwenzao na alikuwa na mahusiano mazuri na wenzake.
Waombolezaji, ndugu na marafiki wakiendelea na ibada ya kuaga mwili wa James Temba.
"Alikuwa ni rafiki yetu sana, na hata alichelewa chuoni alikuwa anatuomba tumuwekee nafasi ya kiti. Tutamkumbuka sana James, nakumbuka mara ya mwisho alinieleza taarifa za kufiwa na shangazi yake huko kijijini akionyesha masikitiko makubwa," amesema mwanafunzi huyo.
Akisoma historia ya marehemu, kaka wa marehemu, Jackson Temba amesema ndugu yao alikuwa mcheshi, mwenye maono makubwa na aliyeaminika katika jamii kutokana na kujituma kwake.
"Katika kipindi cha uhai wake, alikuwa kijana msikivu, mnyenyekevu na aliyeaminiwa kwa vitu vikubwa. Alikuwa na akili nyingi na uwezo wake wa kuchanganyika na watu, lakini alikuwa mshauri mkubwa kwa vijana," amesema kaka wa marehemu.
Aidha, amesema Aprili 29 mwaka huu ndugu yao huyo alikatishwa uhai na watu wasio wema na hivyo kuwaachia familia jeraha kubwa lisilofutika.
Amewaomba waombolezaji waliokuwa msibani hapo kuiombea familia hiyo kutokana na kipindi kigumu wanachopitia.