Polisi, NEC wacharurana kuelekea uchaguzi wa marudio

Muktasari:
- Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) ilisema katika taarifa yake Jumatano kwamba polisi "waliingia kwenye majengo ya NEC bila kibali wala kutangazwa na waliwahoji wafanyakazi wa NEC; na kuwazuia kufanya kazi zao.
Freetown, Sierra Leone. Jeshi la Polisi limetupilia mbali shutuma zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba maofisa wake wanaharibu shughuli zao kipindi hiki cha kuelekea marudio ya uchaguzi mkuu wa rais Machi 27, hali inayosababisha uadilifu wa jeshi kuhojiwa.
Mvutano uko juu huku kampeni zikitawaliwa na vurugu, kushambuliana na vitisho dhidi ya wanasiasa na wafuasi wao pamoja na ongezeko la uhasama wa kikabila.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilisema katika taarifa yake Jumatano kwamba polisi "waliingia kwenye majengo ya NEC bila kibali wala kutangazwa na waliwahoji wafanyakazi wa NEC; na kuwazuia kufanya kazi zao."
Vitendo vyao "vilitumikia kutisha wafanyakazi fulani", Nec iliongeza.
Polisi walijibu Alhamisi kwa kudai kuwa ilikuwa inachunguza makosa 200 ya uhalifu unaohusiana na uchaguzi nchini kote, na baadhi yaliwahusu wafanyakazi wa NEC.
Msemaji wa jeshi hilo alisema maofisa walilazimika kusubiri "muda wa mwisho" ili kuwahoji katibu mkuu wa tume Jumatano na akaongeza kuwa tamko la Nec kwao lilikuja kwa "mshangao".
Jukumu la polisi lilikuwa "kuwaondoa kutoka ndani ya safu yake" mfanyakazi yeyote wa NEC anayeweza kudhoofisha mchakato wa uchaguzi wa marudio Sierra Leone, msemaji huyo aliongeza.
Taarifa ya tume hiyo inaweza kuchochea shutuma zaidi kutoka upinzani kwamba polisi wako wamewekwa mfukoni na chama tawala cha All Peoples 'Congress (APC), ambacho mgombea wake alishika nafasi ya pili katika duru ya kwanza ya kupiga kura mnamo Machi 7.
Nyumba ya kiongozi wa upinzani Julius Maada Bio ilizungukwa baada ya uchaguzi kufungwa siku hiyo na kusababisha mvutano, ingawa hakukamatwa na polisi walitawanyika baadaye.
Bio, kutoka Chama cha Watu wa Sierra Leone (SLPP), aliongoza kwa asilimia 43.3 ya kura, wakati Samura Kamara wa APC alipata asilimia 42.7, matokeo yaliyosababisha kuandaliwa duru ya pili.
APC na SLPP wote wamelalamikia kuwepo udanganyifu katika uchaguzi huo uliotangazwa na waangalizi wa kimataifa na wa ndani kwamba ulikuwa huru na haki.
Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi na Sahel (UNOWAS), Mohamed Ibn Chambas, alisema Alhamisi kuwa tume hiyo ilikuwa "inafanya kazi chini ya changamoto maalum kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ndani ya vikwazo vikali vya wakati".
Aliziasa pande zote "kujizuia na zisiingilie au kuathiri uhuru na uadilifu wa NEC".