Pensheni yaliza wazee

Muktasari:
Wazanzibari kuanza kulipwa Sh20,000 kila mwezi
Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikitarajia kuanza kutoa pensheni kwa wazee wa miaka 70 na kuendelea visiwani humo mwishoni mwa mwezi ujao, wazee wa Bara wameiangukia Serikali wakiiomba itafute njia bora ya kuwalipa.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti kwenye mkutano wa kujadili changamoto zinazowakabili wazee nchini ulioandaliwa na shirika la kimataifa la kusaidia wazee la HelpAge International, baadhi ya wazee hao walisema suala la pensheni limepigiwa kelele kwa muda mrefu, lakini halijafanyiwa kazi.
Mmoja wa wazee hao, Theresia Minja (76) alisema Serikali iliahidi kutoa pensheni kwa wazee wa miaka 70 tangu 2011, lakini bado wanapigwa danadana.
Minja ambaye alistaafu mwaka 1993, alisema ni asilimia nne tu ya wastaafu wa Serikali ambao wanapata pensheni huku asilimia 96 kutoka sekta zisizo rasmi na wale waliokuwa wamejiari wakiambulia patupu.
Alisema umefika wakati Serikali iwafirikie pia wazee ili kuwakomboa kutoka katika umaskini uliokithiri na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi kwa kuwapatia pensheni.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mstaafu mwingine, Abdallah Majumba ambaye alisema, wazee wengi waliotoa mchango katika Taifa hili miaka ya nyuma wamesahaulika.
Hata hivyo, wakati wazee hao wakilamikia hilo, Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi za Jamii kutoka Zanzibar, Salum Rashid alisema kuanzia mwisho wa mwezi ujao, wazee 24,000 wenye miaka 70 wataanza kupokea pensheni zao.
Rashid ambaye ni mkuu wa kitengo hicho kilicho chini ya Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Zanzibar, alisema SMZ imetenga Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kutoa pensheni kwa wazee wote bila kujali aina ya ajira aliyokuwa nayo kabla ya kustaafu.
Alisema kila mzee atalipwa pensheni ya Sh20,000 kila mwisho wa mwezi kwa muda wa miezi mitatu kabla ya bajeti ya mwaka huu wa fedha haijafikia ukomo.
Mbali na changamoto ya pensheni, Naibu mwenyekiti wa HelpAge International, Smart Daniel alisema changamoto nyingine inayowakabili wazee ni kukosekana kwa sheria ya wazee.
Alisema kwa sasa ipo Sera ya Wazee ya Mwaka 2003 ambayo haitoshi kusimamia masuala hasa ya haki za wazee.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Stephen Gumbo alisema sera hiyo inafanyiwa kazi na iko kwenye hatua nzuri za kufanywa sheria.
Gumbo ambaye alimwakilisha Naibu Waziri wa Afya, Dk Khamis Kingwangalla, alisema hata suala la pensheni linafanyiwa kazi na mchakato wake unaendelea vizuri.