Panda, shuka bei za mafuta, wadau wakitaja njia mbadala kukabili

Muktasari:
- Dizeli inakayopokewa katika Bandari ya Tanga imeongezeka bei kutoka Sh3,124 Julai hadi Sh3,138 na Bandari ya Mtwara imeongezeka kutoka Sh3,124 hadi Sh3,140 Agosti kwa lita.
Dar es Salaam. Wadau wa usafirishaji wametaka njia mbadala za kuzuia kupanda na kushuka kwa bei ya mafuta ya dizeli na petrol nchini Tanzania, huku bomba la mafuta la Uganda hadi Tanga na matumizi ya nishati mbadala vikitajwa.
Maoni ya wadau hao, yametokana na taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha bei za mafuta kuanzia jana Jumatano Agosti 7, 2024 imepanda katika mikoa inayochukua mafuta hayo kwenye bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Mafuta yanayochukuliwa Bandari ya Dar es Salaam, petroli imepanda kwa Sh21 kwa lita moja na kuwa Sh3,231, wakati petroli inayochukuliwa katika Bandari ya Tanga, kwa lita moja imepanda kutoka Sh3,210 Julai hadi Sh3,229 huku kwa Bandari ya Mtwara imepanda hadi Sh3,304 kutoka Sh3,212 Julai.
Kwa upande wa bei ya dizeli, taarifa ya Ewura imesema bidhaa hiyo inayopokewa Bandari ya Dar es Salaam bei yake imeongezeka kutoka Sh3,115 Julai hadi Sh3,131 Agosti.
Na dizeli inakayopokewa katika Bandari ya Tanga imeongezeka kutoka Sh3,124 Julai hadi Sh3,138 na Bandari ya Mtwara imeongezeka kutoka Sh3,124 hadi Sh3,140 Agosti kwa lita.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule, amesema mwenendo wa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia kuongezeka kuwa ni miongoni mwa sababu ya kupaa kwa bidhaa hizo muhimu katika uchumi.
Maoni ya wadau
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti wadau wa usafirishaji, akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam(Darcoboa), Sabri Mabrouk, amesema kuna haja ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kugeuzwa kama fursa ya kuondokana na tatizo hilo.
Mradi huo kutoka Kabaale – Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga ni matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni za kimataifa za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi za Total, Tullow na CNOOC.
Katika utafiti huo ilibainika uwepo wa mafuta ghafi takribani mapipa bilioni 6.5 na kutokana na ugunduzi huo imebainika uwezekano wa kuvuna mapipa kati ya bilioni 1.2 hadi 1.7.
Ni kutokana na hilo, Mabrouk amesema anaona ni vema badala ya kusafirisha mafuta ghafi, yangetengenezwa mafuta kabisa.
“Ninaamini mafuta kama yatazalishwa kwa wenzetu Uganda, itakuwa ni rahisi kwa kuwa Tanzania na nchi hiyo sio mbali, badala ya kusubiri yaende kusafishwa huko nje, halafu turudishiwe,” amesema Mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania(Taomac), Raphael Mgaya, alikuwa tofauti na kauli ya Mabrouk na kusema uzalishaji mafuta unahitaji kuwa na teknolojia kubwa, maji mengi na umeme mwingi, vitu ambavyo kwa nchi hizi za Afrika Mashariki bado ni tatizo kubwa.
“Katika biashara hii kadri unavyokuwa na kiwanda kikubwa ndipo na gharama za uzalishaji zinapungua, lakini kama utakuwa na kiwanda kidogo, basi ujue gharama zitakuwa juu na matokeo yake utauza mafuta kwa bei ya juu kuliko yale yanayotoka nje ya nchi.
Pia, amesema inahitaji kuwekeza ukiwa na uhakika wa soko kubwa na ndio maana biashara hizi zipo India, China na Singapore ambako kuna soko kubwa na mahitaji makubwa kutokana na uwepo wa viwanda lakini urahisi wa kusafirisha kwenda nchi nyingine,” amesema Mgaya.
Katika maoni yake amesema zipo njia kuu mbili za kukabiliana na panda shuka ya mafuta, ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya mafuta ambayo ni njia ya muda mfupi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Rahim Dossa, amesema kuna haja ya Serikali kubadili mfumo wa upandishaji bei za mafuta kwa kuzitoa kila baada ya miezi mitatu au minne.
Amesema kwa kufanya hivyo itawasaidia hata wasafisrishaji ambao wamekuwa wakipata oda za mizigo mwezi mmoja na kusafirisha mwezi unaokuja kupambana na gharama za usafirishaji.
‘Hata wananchi wanaumia’
Mwenyekiti wa Chama cha Malori madogo na ya kati (Tamstoa), Chuki Shabani amesema gharama ya kupanda kwa mafuta haiwagharimu tu wasafirishaji bali na wananchi kwa jumla kwa kuwa mafuta yakipanda kila kitu kinapanda huku anayeumia akiwa ni mwananchi wa kipato cha chini.
Katika ushauri wake, Shaban ameiomba Serikali kuendelea kutoa kodi zilizopo katika mafuta na kuhamishia maeneo mengine ili kuleta ahueni kwa wananchi.
Kauli ya Shabani haitofautiani na ya Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo ambaye amesema utoaji wa baadhi ya kodi utaleta afueni kwao ukizingatia biashara hiyo kwa sasa imekuwa ni ya kusuasua.
Pia, Mwalongo amesema kupanda huko kwa bei ya mafuta, hakuwezi kusababisha kupandisha nauli kufidia gharama kwa kuwa kufanya hivyo ni mchakato wa muda mrefu ambao pia unahitaji gharama za kuwakodi wahasibu wenye vigezo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Said Chenja amesema kupanda mafuta kuna athari kubwa ukizingatia bei wanazotoza abiria ni kati ya Sh1,000 hadi Sh2,000, hivyo leo haiwezi kuwa rahisi kumwambia unambeba kwa Sh3,000 kisa mafuta yamepanda.
Ushauri wa mtaalamu
Mtaalamu wa Uchumi na Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo, amesema kuna namna mbili ya kukabiliana na hali ya kupanda na kushuka kwa bei za mafuta duniani, fupi ikiwa ni kuwa na maghala makubwa ya kuhifadhi bidhaa hizo.
“Kuna nchi zinatengeneza maghala makubwa, wakinunua ni stock inayokaa zaidi ya miezi mitatu, hivyo bei ikipanda hapo katikati wao haiwahusu, utakuta wanayo ya kuanzia Januari hadi Desemba,” amesema Profesa Kinyondo.
Amefafanua kuwa na maghala haya yanaweza kutengenezwa kwa ubia wa Serikali na sekta binafsi kwa kuwa Serikali haiwezi kufanya kila kitu na pia biashara hiyo huwezi kuiachia sekta binafsi peke yake kwa kuwa sio tabia yao kukataa faida.
Mtaalamu huyo pia ametaka nchi kutoka kuwa tegemezi wa mafuta hayo na kwenda kwenye nishati safi ya magari kutumia gesi, umeme, sola, upepo, nishati ambazo amesema zote hapa nchini Mungu kajalia zipo.
“Wenzetu sasa hivi wanatengeneza magari yanayotumia umeme, ambao betri zake zinatengenezwa kwa madini adimu ambayo hapa nchini yapo.
“Kwa nini magari yetu yasitumie umeme tumeng’ang’ana na mafuta na kila uchwao Serikali inazidi kuagiza magari makubwa yanayotumia nishati hiyo,” amehoji Profesa Kinyondo.