Padri Mbahulira afariki dunia

Bukoba. Padri Ireneus Mbahulira (80) wa jimbo Katoliki Bukoba amefariki dunia katika hospitali ya Mugana wilaya ya Misenyi akipatiwa matibabu.
Akizungumza jana Jumamosi Januari 23, 2021 Askofu msaidizi wa jimbo hilo, Methodius Kilaini ameieleza Mwananchi Digital kuwa kifo cha Mbahulira kimetokea Januari 22, 2021 katika hospitali ya Mugana Wilaya ya Misenyi alikokuwa amelazwa wiki moja iliyopita.
Amesema katika matibabu mbali na kuwekewa dripu kadhaa, padri huyo aliwekewa mashine za kumsaidia kupumua.
Amesema padri huyo alizaliwa mwaka 1942 na mwaka 1969 alipata daraja la upadri na alihudumu kama paroko Jimbo la Bukoba Parokia ya Buyango Wilaya ya Misenyi.
"Mwaka 2018 aliamua kurudi nyumbani ambapo alipangiwa Parokia ya Rukindo wilaya ya Muleba baadaye alihamishiwa Minziro wilaya ya Misenyi, " amesema Kilaini
Amesema mazishi yatafanyika Jumatatu Januari 25, 2021.