Pacha walioungana watenganishwa Muhimbili

Muktasari:
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikisha upasuaji wa kuwatenganisha watoto pacha walioungana kifuani Rehema na Neema.
Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikisha upasuaji wa kuwatenganisha watoto pacha walioungana kifuani Rehema na Neema.
Upasuaji huo uliodumu kwa saa 7, ulioanza saa 3 asubuhi na kumalizika saa 9 alasiri, umefanikiwa licha ya ugumu na changamoto kubwa kwa watoto hao kuungana ini, moyo na baadhi ya tishu za ndani.
Upasuaji huo uliofanyika kwa mafanikio umefanyika leo Ijumaa Julai Mosi 2022 kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa afya 31 kutoka Tanzania na Ireland ambao wanatokea Shirika la Operation Child Life.
Akizungumza na vyombo vya habari, Daktari bingwa wa upasuaji watoto hospitalini hapo, Zaitun Bokhari amesema upasuaji huo umefanywa na madaktari bingwa wa upasuaji watoto wadogo 12.
“Madaktari wa usingizi sita, madaktari wa kutengeneza ngozi ‘plastic surgery’ wanne, madaktari ambao kazi yao kuangalia mfumo mzima wa watoto unakwenda vizuri wawili na wauguzi 6,” amesema.
Upasuaji wa kutenganisha pacha walioungana ulifanyika kwa mara ya kwanza nchini mwaka 1994 na wa pili ni mwaka 2018.
Kufanyika kwa upasuaji huu leo unaandika historia nyingine kwa kuwa Tanzania inakua nchi ya tatu baada ya Misri na Afrika Kusini katika bara la Afrika kufanya upasuaji mgumu zaidi kwa pacha walioungana.
Serikali ingelazimika kutumia hadi Sh120 milioni endapo pacha hao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu, lakini kwa kuwa upasuaji huu unafanyika nchini inakadiriwa kutumia hadi Sh50 milioni.