Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyumba zabomolewa Mbagala kupisha ujenzi wa stendi

Muktasari:

  • Stendi hiyo inajengwa ikiwa tayari kuna stendi nyingine ya aina hiyo imejengwa maeneo ya Kijichi na kushindwa kufanya kazi. Wananchi wadai hawakutaarifiwa wala kupewa muda wa kutosha kuondoka.

Dar es Salaam. Zaidi ya nyumba 20 zimebomolewa katika Mtaa wa Rangi Tatu na Mtaa Mianzini kwa kile kilichoelezwa ni kupisha ujenzi wa stendi ya daladala na mabasi ya mikoa ya kusini.

Nyumba hizo zilianza kubomolewa tangu jana (Jumapili, Mei 3, 2026), huku wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo wakisema hawajaridhika na namna walivyoondolewa na kutaka viongozi wa juu kuingilia kati.

Mwananchi iliyofika eneo hilo leo, Jumatatu, Mei 4, 2026, ambalo ni jirani na stendi ya Mbagala Rangi Tatu, ilikuta kazi ya ubomoaji ikiendelea ambayo wamepewa kampuni ya udalali ya Yono Action Mart.

Wananchi wa Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam wakiangalia mabaki ya nyumba zilizobomolewa na Kampuni ya Udalali ya Yono kwa amri ya Manispaa ya Temeke, leo. Picha na Said Powa.

Baadhi ya wananchi walioathirika wamesema wameambiwa ubomoaji huo unafanyika kwa kuwa wanatakiwa kupisha ujenzi wa stendi, jambo ambalo limethibitishwa pia na Msemaji wa Halmashauri ya Temeke, Joanita Joseph, alipizungumza na Mwananchi.

“Lile ni eneo la wazi lililokuwa chini ya halmashauri, ambapo baada ya kuachwa wazi kwa muda mrefu, watu walilivamia na baadhi kujimilikisha kama lao.

“Sasa halmashauri imetaka eneo lake kwa ajili ya matumizi ya kujenga stendi, ndiyo maana imewabomolea, na uzuri wananchi waliokuwa wanaishi hapo wanalijua hilo kwamba walikuwa wavamizi na walishapewa notisi, ikiwemo kuongezewa muda wa kuhama,” amesema.

Joanita amesema: “Hivyo, kama kuna wanaosema hawajui au hawakupewa taarifa ya kutakiwa kuondoka, watakuwa waongo, ukizingatia waliomba kuongezewa muda zaidi na halmashauri ikafanya hivyo.”

Wakati Joanita akisema hivyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mianzini, Abdallah Ndengaya, amesema hana taarifa ya ubomoaji huo wala hajui ni matumizi gani yanatarajiwa kufanywa, na suala la ujenzi wa stendi ameliskia kama wananchi wa kawaida walivyolisikia na si katika vikao halali.


Walichosema wananchi

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi waliobomolewa nyumba zao, akiwemo Riziki Robert, ambaye ni mmiliki wa nyumba na mfanyabiashara katika eneo hilo, amesema siku ya tukio hawakuwa wanajua chochote, kwani hawakuwahi kupewa notisi kuwa eneo hilo linatakiwa kubomolewa.

Badala yake, amesema walichokuwa wanafahamu ni kwamba eneo lililotakiwa kubomolewa ni kitalu namba 23 kilichopo jirani na eneo lao, ambalo ni kitalu namba 22.

“Tunashangaa, Jumapili walipita watu wa Yono, saa tano asubuhi, na kutuambia tunatakiwa kutoa vitu vyetu kwenye nyumba. Tulipowauliza kwa nini, wakati tunachojua ni kitalu namba 23 ndicho kinatakiwa kubomolewa, wakatujibu tumeambiwa hata kitalu namba 22 kivunjwe,” amesema Riziki.

Naye Rosemary Kimario, maarufu Mama Mchaga, amesema katika tukio hilo amefanikiwa kutoa vitu vichache katika eneo lake la biashara, huku vingi vikichukuliwa na wahuni.

“Hawakutupa notisi wala muda wa kutosha wa kuhamisha vitu tulivyokuwa navyo ndani, hivyo tumepata athari kubwa,” amesema.

Kwa upande wake, Fatuma Pazi amesema katika ubomoaji huo familia yao imeathirika, ukizingatia baba yao ni mgonjwa na mlemavu wa kutoona, na ni mwezi mmoja tu umepita tangu afanyiwe upasuaji wa tezi dume.

“Nilipigiwa simu na majirani nikiwa kazini, wakaniambia niende kumtoa mzee wangu kwa kuwa nyumba zinavunjwa. Tunaomba viongozi wa juu mje mtusaidie, kwa kuwa hatujui sakata hili limeanzia wapi, wananchi tunanyanyasika huku,” amesema.

Kwa mujibu wa Fatuma, nyumba yao ilikuwa na fremu tatu za biashara ambazo baba yake alikuwa akizitegemea kuendesha maisha yake baada ya kustaafu.


Stendi ya aina hiyo ilishajengwa

Hatua ya kujengwa kwa stendi nyingine inakuja wakati tayari kuna stendi nyingine ya aina hiyo iliyojengwa maeneo ya Kijichi, lakini ikashindwa kufanya kazi.

Baadhi ya wananchi wa Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam wakishuhudia greda likiondoa mabaki ya nyumba zilizobomolewa na Kampuni ya Udalali ya Yono kwa amri ya Manispaa ya Temeke, leo. Picha na Said Powa.

Stendi ya Kijichi inatarajiwa kubadilishwa matumizi yake baada ya kushindwa kutumika kama ilivyokusudiwa kwa mabasi ya mikoa ya kusini.

Hivi karibuni, akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke, Jomary Satura, alisema wameamua kuweka vivutio vitakavyowashawishi watu kwenda eneo hilo, ikiwemo michezo ya watoto.

Stendi hiyo ilianza kufanya kazi Oktoba 17, 2022, huku ujenzi wake ukigharimu zaidi ya Sh3 bilioni tatu, ikiwa ni moja ya miradi ya Uboreshaji wa Miundombinu Dar es Salaam (DMDP).

Hata hivyo, baada ya siku mbili tangu kuzinduliwa, kulizuka malalamiko kutoka kwa madereva wakidai eneo hilo si rafiki kutokana na kuwa na mchanga mwingi uliosababisha magari kunasa.

Changamoto nyingine iliyotajwa ni barabara za kuingia kuwa nyembamba, hali inayosababisha magari kusubiri kupishana.

Kwa upande wa abiria, walisema eneo hilo ni mbali kufikika, na hivyo kupendekeza kuendelea kutumia stendi ya Mbagala Rangi Tatu, jambo lililosababisha mamlaka kuiruhusu kuendelea kutumika hadi sasa, licha ya sintofahamu ya ubomoaji wa nyumba.

Hata hivyo, mara ya mwisho alipozungumza na Mwananchi kuhusu stendi ya Kijichi baada ya wananchi kuitosa Satura, alisema wana mpango wa kubadilisha matumizi yake.

Satura alisema wanatarajia kuweka vivutio mbalimbali katika stendi hiyo, ikiwemo michezo ya watoto na maduka makubwa (supermarket).