Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyumba milioni 10 zawekwa anwani za makazi

Muktasari:

  • Kazi ya uwekaji anwani za makazi nchini imefikia wastani wa asilimia 75, huku nyumba 10,751,123 tayari zikiwa zimewekewa anwani hizo ikiwa ni mkakati wa Serikali kuyatambua makazi yote nchini.

Dar es Salaam. Kazi ya uwekaji anwani za makazi nchini imefikia wastani wa asilimia 75, huku nyumba 10,751,123 tayari zikiwa zimewekewa anwani hizo ikiwa ni mkakati wa Serikali kuyatambua makazi yote nchini.

Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan alibainisha kwamba Tanzania ina jumla ya makazi 14,348,372, kwa mujibu wa sensa ya makazi iliyofanyika Agosti 23. Kati ya hayo, Tanzania Bara ina makazi 13,907,951 na Zanzibar ina makazi 440,421.

Kwa mujibu wa ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia 25 ya nyumba za makazi bado hazijawekewa anwani hizo ambayo ni nyumba 3,597,249, hivyo kazi hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Mikoa mitano inayoongoza kwenye uwekaji wa anwani za makazi kwa viwango vya asilimia ni pamoja na Kaskazini Pemba ambao umefikia asilimia 90, Mtwara (asilimia 88), Njombe (asilimia 88), Kusini Pemba (asilimia 85) na Kagera (asilimia 84).

Mikoa mitano yenye viwango vya chini ni Dodoma (asilimia 63), Rukwa (66), Songwe (asilimia 66), Shinyanga (asilimia 67), Pwani na Dar es Salaa ambayo imefungana kwa kuwa na asilimia 70.

Kwa upande wa idadi kubwa ya nyumba zilizowekea anwani za makazi, Dar es Salaam inaongoza kwa kuzitambua nyumba 638,673, ikifuatiwa na Mwanza 637,231, Kagera 598,332, Morogoro 536,095 na Dodoma 531,072.

Mikoa ya Tanzania Bara yenye idadi ndogo ya makazi yaliyopatiwa anwani ni pamoja na Katavi 141,988, Rukwa 198,424, Songwe 239,587, Njombe 244,920 na Lindi 275,573. Kwa upande wa Zanzibar ni Kusini Unguja 49,243 na Kaskazini Pemba 50,939.

Licha ya kwamba idadi ndogo ya makazi yamepatiwa anwani katika mikoa hiyo, hakuna mkoa ulio chini ya asilimia 50, hiyo maana yake uwekaji wa anwani za makazi umefanikiwa kwa wastani wa asilimia 75.

Uwekaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi nchini, licha ya kuwa ni utekelezaji wa sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 inayotaka nchi kuwa na anwani za kitaifa zitakazowezesha ufikishaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi, pia ni maelekezo ya kimataifa ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umoja wa Posta Duniani (UPU).

Baadhi ya faida za matumizi ya mfumo wa anwani za makazi na postikodi ni kurahisisha ufanyikaji wa biashara mtandao kwa kuuza au kununua bidhaa kwa njia ya mtandao na kuletewa mpaka mlangoni.

Faida nyingine ni kurahisisha ufanyikaji wa huduma za posta na usafirishaji wa bidhaa na abiria mfano uber, bolt; unarahisisha ufikishaji wa huduma za Serikali kwa wananchi kama vile huduma za zimamoto, polisi, gari ya kubebea wagonjwa, sensa ya watu na makazi.

Pia, mfumo huo unasaidia kurahisisha makusanyo ya kodi za Serikali na shughuli zote za kiutawala, kijamii na kiuchumi.

Juzi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hadi Mei mwaka huu, kazi ya uwekaji wa anuani za makazi ilikuwa imefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 95 na kwamba kazi hiyo ni endelevu.

“Shughuli hii ni endelevu kwa kuwa halmashauri zetu zinapima maeneo mapya ya makazi na watu bado wanajenga na wote hao lazima wapate anwani za makazi yao. Kukamilika kwa utoaji wa anwani hizo kutachochea ukuaji na kuimarisha biashara mtandao na kuweka mazingira ya kunufaika na fursa za uchumi wa kidijitali,” alisema.

Akizungumzia mafanikio ambayo mkoa wake umeyapata, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Ahmed alisema siri kubwa ni ushirikishwaji wa wananchi.

“Tulitoa elimu ya kutosha kwa wananchi na kila mtu akaimiliki ile project (mradi), hivyo kupitia hiyo basi ikawa kila mtu anatekeleza wajibu wake bila kutumwa,” alisema Kanali Ahmed.

Alisisitiza wanaendelea kuhimizana, ili kuhakikisha wanakamilisha asilimia 12 iliyosalia katika mradi huo.

Mtaalamu wa uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, “kama hizo ramani zipo ni vizuri kwa sababu siku hizi teknolojia imekuwa nzuri na rahisi zaidi na asilimia 25 iliyobakia kasi yake iongezeke ikamilishwe haraka, ili ramani ikamilike.”

Profesa Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema asilimia 75 si ndogo, lakini wakati mwingine ukienda kwenye tovuti ya ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) pamoja na halmashauri, unakuta wametaja idadi bila vijiji kuorodheshwa.