Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Changamoto, fursa mpya za ongezeko la watu

Muktasari:

  • Ongezeko la watu lililotangazwa jana na Rais Samia Suluhu Hassan limeelezwa kuwa na fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo wananchi wanatakiwa kukuna kichwa kuzifikia huku Serikali yao ikiweka mikakati wa kutatua changamoto zinazotokana na hali hiyo.

Dar/Dodoma. Ongezeko la watu lililotangazwa jana na Rais Samia Suluhu Hassan limeelezwa kuwa na fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo wananchi wanatakiwa kukuna kichwa kuzifikia huku Serikali yao ikiweka mikakati wa kutatua changamoto zinazotokana na hali hiyo.

Miongoni mwa fursa zilizopo ni kutumia idadi hiyo katika usalishaji na soko la bidhaa huku changamoto zikiwa ni athari zinazotokana na ukosefu wa ajira na ongezeko la mahitaji ya huduma za jamii.

Juzi jijini Dodoma, Rais Samia alitangaza Tanzania ina jumla ya watu 61,741,120 ambapo kati yao, wanawake ni 31,687,990 sawa na asilimia 51 na wanaume ni 30,053,130 sawa na asilimia 49.

Shughuli ya sensa iliyofanyika kwa wiki moja ilianza Agosti 23 na jana Rais alihitimisha shughuli hiyo kwa kutangaza matokeo yake ambayo yatatumika kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo.

Sensa ambayo hapa nchini hufanyika kila baada ya miaka 10, mwaka 2012 ilibaini kuwa Watanzania walikuwa 44,928,923, hivyo watu walioongezeka katika kipindi hicho ni 16,812,197, ikiwa ni wastani ongezeko la asilimia 3.2 kila mwaka.

Kutokana na idadi hiyo, wachumi wamebainisha fursa zilizopo kwa idadi hiyo ni watu ikiwa ni pamoja na soko la uhakika na nguvu kazi ya kutosha.

Wamebainisha pia changamoto kwamba idadi hiyo inaongeza mzigo kwa Serikali kutoa huduma za kijamii pamoja na kuongeza changamoto ya ajira.


Takwimu zenyewe

Akitangaza matokeo hayo, Rais Samia alibainisha kuwa kati ya Watanzania 61,741,120, waliopo Bara ni 59,851,347 na Zanzibar 1,889,773.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, sura ya 352 ya mwaka 2015 na kwa kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020, ibara ya 206, na kwa mamlaka niliyopewa na Katiba...ninawatangazia rasmi Tanzania ina idadi ya watu wapatao 61,741,120,” alitamka Rais Samia.

Kuhusu takwimu za mikoa, Rais Samia alisema matokeo ya sensa yanaonyesha mkoa wenye idadi kubwa ya watu ni Dar es Salaam ambao una watu 5,383,728 sawa na asilimia 8.7 ya watu wote nchini, ukifuatiwa na Mwanza ambao una watu 3,699,872 sawa na asilimia 6 ya watu wote hapa nchini.

Kuhusu majengo, alibainisha kwamba matokeo yameonyesha kuwa Tanzania ina jumla ya majengo milioni 14,348,372, kati yake 13,907,951 yakiwa bara na Zanzibar 440,421.

Katika huduma za jamii, Rais alisema vituo vya kutolea huduma za afya vipo 10,067, kati yake, zahanati zipo 8,789, vituo vya afya 1,490 na hospitali 688.

Kwa upande wa elimu, Rais Samia alisema kwa sasa Tanzania ina jumla ya shule 25,626 -- za msingi 19,769 na sekondari 5,857.

“Wito wangu kwenu, viongozi, wadau wote na wananchi kwa ujumla, ni kutumia taarifa hii kwa madhumuni yaliyokusudiwa, kuboresha maisha ya kila Mtanzania,” alisema Rais Samia.


Soko limepanuka

Akizungumzia takwimu hizo, mchambuzi wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo alisema ongezeko hilo la watu ni fursa kwa wafanyabiashara, wenye viwanda na wenye nyumba za kupangisha.

“Watu wakiwepo duniani, wanahitaji kula, wanahitaji kuvaa, wanahitaji kulala, wanahitaji kutembea. Na ili kufanya hayo yote, inabidi miamala ifanyike, kwa hiyo ni fursa kwa wafanyabiashara, wenye viwanda na watu wenye nyumba za kupangisha,” alisema.

Hata hivyo, alisema ukuaji wa miji mikubwa ya Dar es Salaam na Mwanza unakwenda kuongeza msukumo kwenye huduma za kijamii kwa sababu watu ni wengi, hivyo watahitaji huduma ya maji, elimu na matibabu.

Pia, alibainisha kwamba ongezeko hilo litaongeza tatizo la ajira kwenye miji kwa sababu watu wanapohama kutoka vijijini kwenye mijini, wanakuwa na matumaini ya kupata fursa za ajira lakini wanakuta hali tofauti.

“Unapokuwa na tatizo la ajira wakati nguvu kazi ipo, unatengeneza jamii ya watu ambao “wanaweza wakawa watu ambao si wazuri sana”, ndiyo unakuta panyarodi…kwa sababu unakuta mtu lazima ale, lazima aishi, kama fursa hazipo hapo anapoishi ni rahisi sana kufanya mambo ambayo hayaendani na sheria zetu,” alisema Profesa Kinyondo.

Profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Humphrey Moshi alisema endapo idadi ya vijana ni kubwa katika jumla iliyotangazwa itakuwa ni fursa kwa sababu taifa litakuwa na nguvu kazi ya kutosha.

Alisema kukiwa na nguvu kazi ya kutosha, wataweza kuzalisha kwa wingi lakini pia kuwahudumia makundi tegemezi kama vile watoto na wazee.

Hata hivyo aliweka angalizo kuwa ikiwa vijana hao hawatakuwa na ajira, hiyo haitakuwa neema, itakuwa laana.

“Cha muhimu kufanya ni kuhakikisha kwamba hawa vijana wanakuwa na kitu cha kufanya ili waweze kuchochea zaidi uchumi kukua kwa haraka,” alisema Profesa Moshi wakati alizungumza na Mwananchi.

Mtaalamu mwingine wa uchumi, Oscar Mkude alisema changamoto anayoiona ni kukosekana kwa fursa na mazingira yatakayowawezesha vijana kupata ajira au kujiajiri, jambo ambalo linaongeza mzigo kwa kaya na Serikali.

“Eneo ambalo naona ni fursa ni kilimo lakini hatujawekeza vya kutosha. Kilimo kinachukuliwa kama kazi ya mtu masikini, aliyechoka na kweli wakulima wengi wamchoka. Lakini kwa wenzetu Ulaya, kilimo ni kazi ambayo ina manufaa makubwa,” alisema.

Mkude aliongeza kwamba kuwa na watu wengi ambao hawaweza kuchangia maendeleo ya Taifa, kutawafanya wengine wachangie kwa niaba yao. Alitolea mfano wa tozo kwenye miamala ya simu kama moja ya njia ya kutanua wigo wa mapato kwa kuwa wachangiaji ni wachache.

Mkazi wa Isanga, mkoani Dodoma, Elizabeth Daudi alimwomba Rais Samia baada ya kujua takwimu halisi, aweke nguvu katika uwezeshaji kiuchumi wanawake ambao wameonekana ndio wengi nchini.

“Nawataka wanawake wenzangu kuweka bidii kwenye uzalishaji kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu baada ya kufahamu idadi yetu,” alisema.


Matokeo mengine bado

Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara 2022, Anne Makinda alisema matokeo ya sensa yaliyozinduliwa ni ya mwanzo yanayotokana na uchambuzi wa maswali machache kati ya 100 yaliyokuwapo katika dodoso.

Makinda alisema kadri uchambuzi utakavyokuwa unakamilika, ndivyo matokeo yatakavyoendelea kutolewa kwa mujibu wa kalenda ya kuchapisha matokeo ya Sensa.

“Kwa hiyo haya leo ni matokeo ya mwanzo, mengine yatakavyozidi kuchambuliwa yataendelea kutolewa, kuna mambo ya ustawi wa jamii, hali halisi na mazingira, yataendelea kutolewa kwa mujibu wa kalenda,” alisema.

Alisema awamu hiyo ni muhimu kwani walipokuwa wakielimisha na kuhamasisha watu kushiriki sensa walizungumzia umuhimu wa kujenga mustakabali wa maendeleo ya nchi.