Nondo tano za Profesa Janabi

Muktasari:
- Masihara na utani wa jamii kuhusu mafundisho ya mtaalamu mbobezi wa magonjwa ya moyo nchini, Profesa Mohamed Janabi mitandaoni, yanaashiria elimu imefika. Hilo linaonekana pale linapotokea jambo ambalo aliwahi kulionya kwenye maandiko yake na watu kukumbushana kuwa mtaalamu huyo alionya kuhusu suala hilo.
Dar es Salaam. Miongoni mwa wataalamu ambao wamekuwa wakiibua mijadala ya kiafya ndani ya jamii ikiwemo mitandaoni, ni mtaalamu mbobezi wa magonjwa ya moyo nchini, Profesa Mohamed Janabi.
Profesa Janabi ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), amewahi kutoa kauli kadhaa za ushauri wa kiafya ambazo kwa namna moja ama nyingine, Watanzania baadhi yao wamekuwa wakikosoa kwa kuwa zinagusa kile wanachokipenda.
Hapa tunakuletea kauli zake tano za kitaalamu zenye uhalisia wa maisha na afya ambazo amewahi kuzitoa, ijapokuwa zinakosolewa lakini zimegusa maisha ya watu.
Novemba 25, 2021 Profesa Janabi alisema matumizi makubwa ya pombe zote husababisha matatizo makubwa kwenye moyo.
Alieleza kuwa kitaalamu inashauriwa mtu atumie kati ya bia moja hadi mbili tu kwa siku na ziwe na mpishano wa saa moja na kwa wanaotumia vinywaji vikali wanashauriwa kunywa ‘shoti’ moja tu ili kulinda moyo.
“Ukienda baa saa moja hadi saa mbili ya usiku chupa moja, Chupa ya pili unaanza kunywa saa mbili hadi saa tatu baada ya hapo tazama mpira Liverpool inavyozifunga timu zingine au Simba inavyozifunga timu zingine,” alisema.
Alitaja matumizi ya pombe yaliyokithiri na ya muda mrefu husababisha misuli ya moyo kulegea na kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu vizuri.
“Hii husababisha kiwango fulani cha damu kubaki kwenye moyo nyakati zote na kufanya misuli yake kuzidiwa na uzito na kulegea Zaidi, na matokeo yake kuuacha moyo utanuke,”alisema.
Agosti 10, 2023 Profesa Janabi alisema ni muhimu kupima afya kabla ya kufanya mazoezi ili kusaidia katika kuboresha kinga ya mwili, pamoja na kujua hali ya afya ya moyo.
Akiongea na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24 alisema kupima afya kunasaidia kujua uwezo wa mwili katika kukabiliana na mazoezi, ambayo hufanywa kama vile mpira na kukimbia.
“Mazoezi ni kitu kizuri ila kapimeni afya zenu kabla ya kuanza, hii itawasaidia katika kuimarisha afya na kujiepusha na magonjwa ambayo yanaweza kuepukika.
“Nakumbuka nilipokuwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ile Afcon iliyofanyika timu ya Taifa ilileta wachezaji kupima, siwezi kutaja majina lakini Rais Karia kama ananiona anakumbuka tuliondoa wachezaji wawili pale tukasema hawa watakuja kuanguka uwanjani kama Yanga mtasema Simba karoga na kama Simba mtasema Yanga karoga…
“Wana tatizo mioyo yao ni mikubwa, ukishakuwa na hilo tatizo utakuja kuanguka kiwanjani ghafla na bahati mbaya unaweza kupoteza maisha, nikiwa mdogo Hussein Tindwa wa Simba alifariki uwanjani, wakati huo sikuwa daktari lakini nakumbuka kilichosemwa,” alisema Profesa Janabi.
Mei 6, 2021 Wakati wa mwezi wa Ramadhan, Profesa Janabi alinukuliwa akisema kula futari nyingi kipindi cha magharibi sio tu kutafanya wafungaji na waalikwa wengine kuongezeka uzito, bali kwa wale walaji ambao wana matatizo mbalimbali ya moyo kama shinikizo la damu la juu, moyo dhaifu, uliopanuka, mishipa au mirija ya moyo iliyoziba wanaweza kupata matatizo ya kiafya .
“Ulaji wa chakula kingi kunaweza kuchochea mshtuko wa ghafla wa moyo ambao unasababisha mamilioni ya watu kupoteza maisha kila mwaka duniani. Kila mwaka vifo hivi vinaongezeka zaidi duniani kipindi hiki cha RamadhanI na wakati wa sherehe mbalimbali kama vile Krismasi, Pasaka na Mwaka mpya,” alisema Profesa Janabi.
Alitaja sababu za vifo hivyo kuongezeka kipindi cha Ramadhani kuwa unapokula chakula kingi mpaka kuvimbiwa wakati wa kufuturu/iftar au wakati wa daku ,tumbo la chakula linapanuka ili kukipokea.
Hiyo itasababisha damu mwilini kujipanga upya kwa kutoa damu nyingi kutoka kwenye moyo kupeleka kwenye njia ya chakula, ili kusaidia kukisaga wakati wa futari/daku.
“Hali hii ikimkuta mlaji ambaye ana tatizo lake la moyo au presha la muda mrefu itasababisha mstuko wa moyo na athari zake,”alisema.
“Tumbo lililojaa kutokana na ulaji wa chakula kingi husababisha moyo kwenda mbio au mapigo kutokwenda sawasawa, hii pia huchochea mstuko wa moyo na wengine kupata kiharusi,” alisema.
Oktoba 6, 2018 alisema watu wenye miili ya wastani bila magonjwa, kulea mwili katika mazingira hayo ni gharama kubwa sana.
“Kabla hujaondoka kwenda sehemu jiulize kwanza huko nitakula nini? Mimi mpaka huwa nabeba chakula changu mwenyewe ambao nishawahi kuwa nao semina wanajua. Kwa sababu kula chochote ulicholetewa sio ishara ya upendo, afya ikishabomoka ni gharama sana kuijenga,” alisema.
Profesa Janabi alisema Watanzania hawajui kitambi kinatengenezwa na vyakula vya bei poa, kama ubwabwa, tambi, ngano, soda, juisi, mafuta mabaya.
“Watanzania hawajui athari za kula kupindukia vyakula vya sukari na wanga. Wanadhani ni mafuta yanayoonekana, sayansi inasema huwezi kula mafuta na kurundika mafuta, ila unaweza kula wanga na sukari ukarundika mafuta na hayo ndio yanaitwa mafuta mabaya,” alisema.
Alitoa mfano rahisi ili uweze kupata glasi moja ya juisi ya asilimia 100 ya machungwa unahitaji machungwa manne mpaka matano, ina maana nikinywa glasi tano kwa siku nimekula machungwa 20 kwa siku 10 machungwa 200, mwezi 600 ni ngumu kula idadi hiyo.
“Chukua tunda lolote lile ili uweze kupata glasi ambayo hujaongeza kitu kingine chochote na ndiyo maana upande wa afya tunashauri zaidi kula matunda badala ya juisi,” alisisitiza.
Desemba 11, 2023 aliweka wazi kuwa kwa mtoto kuzaliwa akiwa na uzito wa zaidi ya kilogramu nne ni kiashiria cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Alisema mtoto aliyezaliwa na uzito mkubwa yuko hatarini, hivyo jamii haipaswi kufurahi mama anapojifungua mtoto mwenye uzito mkubwa kwa kuwa ni hatari kiafya.
"Pale wodi ya wazazi unaona mtu amejifungua mtoto mwenye kilogramu 4 ndugu wanasema mashallah, hapo hamna mashallah mtoto ni ana uzito uliopitiliza si jambo kufurahia ni tatizo. Si sahihi kwa mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mkubwa kupita kiasi, tujitahidi kupunguza uzito. Ukiwa mzazi mnene hii unaiambukiza kwa mtoto, sasa hivi tunashuhudia watoto wadogo wanakuja Muhimbili figo zimeharibika tunalazimika kuwapandikiza,” alisema Profesa Janabi.
Daktari huyu bingwa wa magonjwa ya moyo alisema mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa kupita kiasi ni matokeo ya mfumo usiofaa wa maisha ya mama aliyebeba ujauzito, hasa anaporuhusu mwili wake upokee sukari nyingi.
Kuna umuhimu wa kuzingatia haya kwa maana wengi wamekuwa wakipata madhara yatokanayo na tabia bwete ambazo Profesa Janabi amekuwa akiziainisha kwenye mikutano, semina na maandiko yake kwa lengo la kubadili mtazamo wa jamii, ili iishi katika afya bora na salama.