Ni hukumu ya kuitikisa katiba au wanasiasa Kenya

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alipotangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya katika ukumbi wa Bomas Agosti 15 na Dk William Ruto kutangazwa mshindi. Picha ya Maktaba
Muktasari:
Tofauti na hukumu iliyofuta ushindi wa Uhuru Kenyatta mwaka 2017, ya leo inaweza kutikisa Katiba ya Kenya kutokana na hoja za walalamikaji ambao ni Raila Odinga na Martha Karua.
Nairobi. Tofauti na hukumu iliyofuta ushindi wa Uhuru Kenyatta mwaka 2017, ya leo inaweza kutikisa Katiba ya Kenya kutokana na hoja za walalamikaji ambao ni Raila Odinga na Martha Karua.
Mbali na hayo, makamishna wanne kati ya saba wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) walijitenga na matokeo yaliyotangazwa hivyo kuongeza ugumu kama wataweza kuungana iwapo matokeo ya urais yaliyotangazwa yatafutwa.
Hukumu hiyo inatolewa baada ya Odinga aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya na mgombea mwenza wake, Martha Karua kupinga katika Mahakama ya Juu ushindi wa mgombea wa muungano wa UDA, Dk William Ruto.
Wawili hao mbali na kuiomba mahakama iwatangaze wao kuwa washindi wa uchaguzi huo uliofanyika Agosti 9, wameomba IEBC itangazwe kutokuwa na uwezo wa kusimamia uchaguzi na kumtangaza mwenyekiti wake, Wafula Chebukati kukosa sifa za kuongoza ofisi hiyo ya umma.
Tayari Jaji Mkuu Martha Koome na msaidizi wake Philomena Mwilu, wamewaomba Wakenya wawaombee ili leo watoe uamuzi wenye busara na unaoendeleza demokrasia nchini humo.
Majaji wengine kwenye kesi hiyo ni Mohamed Ibrahim, Dk Smokin Wanjala, Njoki Susanna Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko.
Wakati wa uamuzi wa kupinga ushindi wa Uhuru Kenyatta mwaka 2017 katika kesi iliyofunguliwa na Raila Odinga, Jaji Mkuu David Maranga alisema kati ya majaji sita waliosikiliza kesi hiyo wanne walijiridhisha kwamba uchaguzi huo haukufanyika kwa mujibu wa Katiba na sheria za uchaguzi nchini humo.
Hukumu ya leo ina majaji saba wakiongozwa na Martha Koome aliyezaliwa mwaka 1960 ambaye ni jaji mkuu wa 15 tangu Kenya ipate uhuru.
Wakati akifuta ushindi wa Uhuru Kenyatta, Jaji Mkuu Maranga alisema kwa mujibu wa majaji hao kulikuwa na udanganyifu mkubwa kwenye uchaguzi huo hivyo haukuwa huru wala kufanyika kwa haki.
Kauli ya Jaji Maranga iliungwa mkono na Chekubati ambaye baada ya hukumu hiyo alinukuliwa akisema waliohusika katika kuvuruga uchaguzi wanafaa kuwajibishwa.
Pia, alitangaza kumwalika Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kufanya uchunguzi ndani ya IEBC na kuwafungulia mashtaka watu wote waliohusika kuuvuruga uchaguzi.
Tangu hukumu hiyo ya Agosti 2017, Odinga ameendelea kuilalamikia IEBC na katika maombi yake kwenye kesi inayotolewa hukumu leo ni kwamba imeshindwa kusimamia uchaguzi na Chekubati hana uwezo wa kuongoza ofisi hiyo ya umma.
Mgongano wa kikatiba
Iwapo leo Mahakama ya Juu itaufuta ushindi wa Dk Ruto, kwa mujibu wa Katiba uchaguzi huo mkuu utatakiwa kurudiwa ndani ya siku 60.
Pia, kama mahakama itakubaliana na hoja za Odinga za kuitangaza IEBC kutokuwa na uwezo wa kusimamia uchaguzi au mwenyekiti wake Chekubati kwamba hana uwezo wa kuiongoza ofisi hiyo ya umma, Kenya itaingia kwenye mgogoro wa kikatiba kwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta anayeondoka madarakani hana madaraka ya kuteuwa kiongozi yeyote, anachosubiri ni kuapishwa kwa Rais mpya yeye aondoke.
Hata hivyo, Katiba inaelekeza kuwa kiongozi wa IEBC anaweza kuondolewa kwa mashitaka dhidi yake kuwasilishwa bungeni na tume maalumu itakayoundwa na Rais.
Mwanasheria mbobevu wa Katiba, Bobby Mkangi alisema hata kama Mahakama ya Juu itafuta matokeo ya urais, Rais Uhuru Kenyatta hawezi kuwa na mamlaka ya kufanya uteuzi wowote.
“Amebaki kwenye ofisi kusubiri kuapishwa kwa Rais mpya. Kufutwa matokeo ya urais hakumrejeshei mamlaka,” alisema Mkangi.
Hukumu kuigawa IEBC?
Pia, hukumu hiyo vyovyote itakavyokuwa inatishia kuwagawa makamishna saba wa IEBC kwa kuwa itakuwa vigumu kwao kuungana na kuandaa uchaguzi wa marudio kama mahakama itafuta matokeo ya awali ya urais yaliyotangazwa huku wajumbe wan ne kati yao wakisema hawayatambui wala kuyabariki.
Makamu Mwenyekiti wa IEBC, Juliana Cherera na makamishna wengine Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya walitangaza kutoyatambua matokeo hayo ya kura za urais yaliyotangazwa Chebukati ndani y amuda wa kikatiba wa kutangaza matokeo ya kura zilizopigwa na wananchi waliojitokeza siku ya uchaguzi mkuu.
Pia, makamishna hao walitangaza kuwa mchakato wa uchaguzi ulikiuka sheria na taratibu za uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, Chekubati na makamishna wawili kati ya saba waliobaki ambao ni Boya Molu na Abdi Yakub Guliye wanayatetea matokeo yaliyompa ushindi Dk Ruto.
Jaji Mkuu Martha Koome
Mwaka 2021, Rais Uhuru Kenyatta alimteua Martha Karambu Koome kuwa jaji mkuu wa kwanza mwanamke nchini Kenya ili kumrithi David Maraga aliyemaliza muda wake.
Baada ya uteuzi wa Rais, tume inayoshughulikia idara ya mahakama ilimpitisha Koome baada ya kuwahoji wagombea 10 waliokuwa wanaiwania nafasi hiyo na baadaye Bunge likamthibitisha.
Koome amewahi kuwa mwanaharakati wa haki za binadamu kabla ya kuwa jaji. Alikuwa mstari wa mbele kuwatete wanaharakati wa kisiasa wakati wa utawala wa Rais Daniel Arap Moi.
Alijiunga na idara ya mahakama mwaka 2003 na miaka minane baadaye, ataketeuliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa nchini Kenya.
Mwaka 2019, Koome alikuwa kati ya majaji watano waliotupilia mbali kesi ya kutaka kusajiliwa kwa shirikisho linalotetea masilahi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja nchini humo.