Fahamu mambo tisa uamuzi kesi kupinga ushindi wa Ruto kesho

Muktasari:
- Uamuzi wa kesi ya kupinga matokeo ya kura za urais utajikita kwenye mambo tisa yaliyotambuliwa kuzua utata.
Nairobi. Kesho Jumatatu Septemba 5, 2022 majaji saba wa Mahakama ya Juu ya Milimani nchini Kenya wanatarajiwa kutoa uamuzi wa kesi ya kupinga matokeo ya urais yaliyompa ushindi Rais mteule wa Kenya, William Ruto iliyofunguliwa na Raila Odinga.
Shauku ya uamuzi huo wa kesho haishii kwa wanasiasa hao wawili bali inawahusu wafuasi, mashabiki wao na watu wa mataifa mbalimbali wanaotaka kujua hatima ya kisiasa ya Kenya iliyofanya iliyofanya Uchaguzi Mkuu Agosti 9, 2022 na matokeo yake kutangazwa Agosti 15 na Mwenyekiti wa Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, Wafula Chebukati.
Kupitia uamuzi utakaotolewa na Jaji Mkuu Martha Koome na majaji Philomena Mbete Mwilu, Mohamed Ibrahim, Dk Smokin Wanjala, Njoki Susanna Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko utatoa uelekeo kama Ruto ataapishwa Septemba 13, 2022 kuwa Rais wa Kenya au kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga atapata fursa nyingine ya kuwania urais kama matokeo yatabatilishwa au atakwenda kustaafu siasa.

Majaji saba wa Mahakama ya Juu ya Milimani nchini Kenya wanaotarajiwa kutoa uamuzi wa kesi ya kupinga matokeo ya urais yaliyompa ushindi Rais mteule wa Kenya, William Ruto iliyofunguliwa na Raila Odinga.
Uamuzi wa kesi hiyo ya kupinga matokeo ya kura za urais utajikita kwenye mambo tisa yaliyotambuliwa kuzua utata;
1. Ikiwa mitambo ya kiteknolojia almaarufu Kiems, iliyotumika kuwatambua wapiga kura na kupeperusha matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 ilifikia ubora unaohitajika.
2. Ikiwa mtandao wa Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ulivurugwa.
3. Ikiwa Fomu 34A zilizotumwa katika mtandao wa IEBC zilikuwa tofauti na walizopewa maofisa wa kusimamia uchaguzi katika vituo vya kupigia kura pamoja na zile walizopewa maajenti wa wawaniaji urais vituoni.
4. Ikiwa kuahirishwa kwa uchaguzi wa magavana Kakamega na Mombasa, pamoja na maeneo mengine sita kuliwanyima wapiga kura fursa ya kupiga kura za urais.
5. Ikiwa kulikuwa na tofauti za kura zilizopigiwa wawaniaji urais na nyadhifa kama Ugavana, Useneta, Ubunge na Udiwani.
6. Ikiwa IEBC ilikagua, kutathmini na kutangaza matokeo ya kura za urais kwa mujibu wa Katiba.
7. Ikiwa Rais Mteule Dk William Ruto aliyetangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alipata asilimia 50 + 1 ya kura zilizopigwa kulingana na Kifungu nambari 138 cha Katiba.
8. Ikiwa kulikuwa na makosa ambayo yatachangia kubatilishwa kwa matokeo ya kura za urais.
9. Maagizo yanayofaa kutolewa