Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NGIZWE MCHUNU: Kuchoma nyumba hakutazuia harakati kupinga wahamiaji - 3

Muktasari:

  • Asisitiza matatizo ya muda mrefu hayawezi kutatuliwa kwa usiku mmoja na hivyo kampeni yake ya kupinga uhamiaji haitasimama, haitasitishwa, wala kurudi nyuma.




Kuna picha moja ambayo imekuwa ikisambaa katika mitandao ya kijamii ya Afrika Kusini tangu Mei 10, 2026 inayobeba taswira ya jambo la msingi lakini la kutisha kuhusu wakati huu katika historia ya nchi hiyo.

Katika picha hiyo, Ngizwe Mchunu anaonekana amesimama katikati ya magofu ya nyumba zake (rondavels) zilizochomwa moto huko Mbumbulu. Mbali na picha hiyo, Afrika Kusini yenyewe inaendelea kuchemka.

Kuchomwa kwa makazi ya Mchunu kama tulivyoona kwenye makala ya kwanza,  hakukuwa tukio lililotokea pasipo sababu. Ilikuwa ni shambulio la pili baada ya lile la kiongozi wa harakati za ‘March and March’ ndani ya kipindi cha wiki mbili.

Felemntwnini Gumede, kiongozi wa ‘March and March’ aliyeko Mzimkhulu, nyumba yake ilivunjwa na kuharibiwa na kundi lililokuwa likimtafuta siku chache kabla ya tukio hilo.

Watoto wake nao walinusurika. Wanaharakati wanaohusishwa na harakati za kupinga wahamiaji walikuwa wakilengwa majumbani mwao, katika maeneo yao ya kifamilia. Ni watu wasiojulikana lakini wanaodhaniwa kuchochewa na hasira dhidi ya maandamano ya wanaharakati hao.

“Watu waliochoma nyumba yetu wanataka vita,” alisema Sbani Mchunu, mtoto wa Ngizwe Mchunu. Baba yake pia hakuwa na mtazamo tofauti.

“Matatizo ya muda mrefu hayawezi kutatuliwa kwa usiku mmoja,” Ngizwe alieleza, huku akisisitiza kuwa kampeni yake ya kupinga wahamiaji haitasimama, haitasitishwa wala kurudi nyuma hata hatua moja.

Anaposema ‘tuko vitani’, Mchunu anaamini kwa dhati kwamba Afrika Kusini ipo katika vita vya kimaadili na kiustaarabu kati ya wanaotaka kusimamia mipaka na sheria zake na wale wanaonufaika kiuchumi au kisiasa na kutokuwapo kwa usimamizi huo.

Hoja zake ingawa zina utata na mara nyingine ukali, zinagusa hisia za mamilioni ya raia wa Afrika Kusini wanaokabiliwa na ukosefu wa ajira karibia asilimia 40, wanaowaona watoto wao wakishindania nafasi chache za fursa na watu waliovuka mipaka na kuingia kwenye nchi yao bila nyaraka.

Haya ni malalamiko halisi. Hayajatengenezwa na Mchunu, hata kama mbinu zake za kuyakuza mara nyingi huwa za kiholela na wakati mwingine hatarishi.

Lakini kati ya malalamiko halali na njia zinazotumika kuyashughulikia kuna pengo kubwa ambalo wachambuzi wanasema ndiyo kiini cha mgogoro wa kimaadili ndani ya harakati za ‘March and March’.

Uchunguzi wa kina wa gazeti la ‘Daily Maverick’ kuhusu harakati hizo umeielezea ‘March and March’ kama harakati inayotumia alama za jadi za upinzani wa kiraia wa Afrika Kusini (fulana, maandamano na nembo za bendera ya taifa), huku ikiendeleza ajenda ya umaarufu wa kisiasa inayofanana na harakati za mrengo mkali wa kulia, dhidi ya wahamiaji barani Ulaya na Amerika Kaskazini.

Maandamano yake yanayodai uhalali, sera ngumu za ukimbizi na hatua dhidi ya wafanyabiashara wanaoajiri watu wasio na vibali, yanaweza kusikika ya kawaida yanapotazamwa kwa mbali.

Lakini uwanjani, wanahabari wameripoti hali tofauti, yaani kuwako vurugu, vitisho na kulengwa kwa watu kwa misingi isiyo ya kisheria bali kwa sura, lafudhi au hata ishara za biashara zao.

Historia ya Mchunu inafanya ukosoaji huu usiwe rahisi kupuuzwa kama ambavyo angependa. Amewahi kukumbwa na malalamiko kadhaa mbele ya Tume ya Haki za Binadamu ya Afrika Kusini, si tu kutokana na kauli zake dhidi ya wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (LGBTQIA+ ) zilizomletea onyo rasmi Oktoba 2025, bali pia kauli zake kuhusu jamii ya Wahindi.

Jumuiya ya Wahindi nchini humo, iliwasilisha malalamiko yake ikimtuhumu kutoa kauli za kibaguzi zilizojaa chuki wakati wa kipindi cha chake ‘Bhinca Nation’.

Taasisi ya Ahmed Kathrada Foundation baadaye ililaani kauli hizo, ikisema zinachochea mazingira ya uhasama wa kikabila. Mchunu alizipuuza shutuma hizo akisema ni njama za maadui anaowajua wazi na kuwa anao wengi.

Wafuasi waliofika katika nyumba yake iliyochomwa hawakuja kwa sababu wanakubaliana na kila anachosema, bali kwa sababu walitambua katika hali yake kitu wanachokielewa kwa hisia kali, yaani hisia ya kusema ukweli usiopendeza na kulipia gharama yake.

Kwa upande wake, Mchunu anajua ana maadui wengi na wenye nguvu. Aliwataja bila kificho baada ya tukio la moto: Julius Malema, jamii ya LGBTQIA+ na watu wasiojulikana anaowaita ‘wakazi wa ndani’ wanaopinga kampeni yake.

Alilinganisha kwa namna moja hali yake na ya Chris Hani, aliyeuawa akionyesha kuwa kama mauaji ya Hani hayakuzuia mabadiliko ya kidemokrasia, basi kuchomwa kwa nyumba yake pia hakutazuia harakati zake.

Kisichotabirika ni mwelekeo wa yote haya. Kesi ya Bonginkosi Khanyile iliyovurugwa na tukio la moto inaendelea mahakamani. Khanyile anakabiliwa na mashitaka ya kuchochea vurugu na kuvunja kanuni za Uviko-19 za mwaka 2021.

Mahakama Kuu ya Gauteng, Pretoria, imetoa amri ya kudumu inayomzuia Ngizwe Mchunu kuendelea kutoa au kurudia madai ya kashfa dhidi ya Julius Malema.

Awali aligoma kuomba radhi na alionekana kuendelea kumshambulia Malema hadharani hata baada ya kupokea amri ya mahakama.

“Nitawasiliana na ‘amadlozi’ (mizimu ya mababu) kuona ninachopaswa kurekebisha,” aliambia gazeti la Daily Sun, akirejea mizimu ya mababu katika utamaduni wa Kizulu.

“Kama hili lilikusudiwa kuondoa uhai wangu, basi iwe hivyo, lakini sitaacha kupambana,” alisema.

Katika nchi ambako chama tawala kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu na mamilioni ya watu bado wanahisi ahadi za demokrasia hazijatekelezwa, kuna mantiki hatari katika uimara wa Mchunu.

Anawakilisha wale wasiotaka kukubali hali ilivyo. Wakosoaji wake wanasema ni mchochezi anayetumia malalamiko halali kueneza chuki na kwamba, kampeni zake dhidi ya wahamiaji wasio na vibali mara nyingi hubadilika kutoka uanaharakati kwenda vitendo vya vurugu.

Lakini wafuasi wake wanasema serikali imeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa wananchi, kwamba wanasiasa wamegeuza suala la uhamiaji kuwa chombo cha siasa bila kulishughulikia kwa uhalisia. Pia, ni watu kama Mchunu pekee wanaoweza kulilazimisha liingie kwenye ajenda ya kitaifa.

Tarehe ya mwisho ya Juni 30, 2026 inayotolewa na harakati ya ‘March and March’ kwa wageni wasio halali kuondoka Afrika Kusini, kisheria haiwezi kutekelezeka. Lakini kama kauli ya kisiasa ya kuchochea hisia, ina nguvu kubwa.

Wakati huohuo, waliochoma nyumba Mbumbulu bado hawajulikani. Polisi wa KwaZulu-Natal (KZN) wamefungua jalada la uchunguzi ambao unaendelea.

Waliowasha moto huo watapatikana au hawatapatikana? Lakini moto wa ndani zaidi, ule uliokuwa ukijijenga kwa miaka mingi chini ya uso wa jamii ya Afrika Kusini, ambao Mchunu hakuuwasha lakini kwa hakika ameuchochea, unaendelea kuwaka bila kuzimika na hakuna amri ya mahakama, uamuzi wa tume inayoweza kuuzima.


Akiwa katikati ya mabaki ya kila alichokuwa nacho, Mchunu alisema: “Sina dhambi kwa mababu zangu zinazostahili kuniadhibu hivi.”

Kama mababu wanasikiliza au la, hilo ni suala la imani. Kile kisicho cha imani ni kile kitakachofuata.

Ngizwe Mchunu bado hajaisha. Afrika Kusini, inayotikiswa na hasira, wasiwasi na makovu ya historia yake tata pia bado haijaisha.

Swali si kama moto utaendelea kuwaka, bali ni utachoma nini na kuangamiza.

Caption: Ngizwe Mchunu akiwa na mashabiki wake baada ya Mahakama Kuu ya Pretoria kuhitimisha kesi ya madai ya kashfa dhidi ya Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema, ikimtaka kuacha kutoa matamshi ya kumchafulia jina.