Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndege ya kwanza yatua Sumbawanga baada ya uwanja kukamilika

Uzinduzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga mkoani Rukwa.

Muktasari:

  • Uzinduzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga kutafungua fursa ya uwekezaji, biashara, ajira, utalii na vivutio vya asili vinavyopatikana katika Mkoa wa Rukwa.

Rukwa. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amewataka wananchi kutumia vyema fursa zinazotokana na maboresho ya sekta ya uchukuzi kujikwamua kiuchumi kwa kuibua na kuendeleza miradi ya kimkakati.

Kihenzile ametoa kauli hiyo leo Aprili 24, 2026, alipomwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, katika uzinduzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga mkoani Rukwa.

Amesema uwanja huo ni kichocheo muhimu cha maendeleo kwa wananchi wa Rukwa na maeneo jirani, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha sekta ya uchukuzi ili kuinua maisha ya Watanzania.

Katika tukio hilo, ndege ya abiria ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ilitua kwa mara ya kwanza na kupokewa kwa “water salute”, kuashiria kuanza rasmi kwa huduma za usafiri katika kiwanja hicho.

Katikati ni Naibu waziri wa uchukuzi David Kihenzile katika uzinduzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga.

“Ninazindua uwanja huu kwa kuwa umejengwa kwa kiwango kinachokubalika, chenye ubora wa hali ya juu wa kimataifa,” amesema Kihenzile.

Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Msalika Makungu, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Makongoro Nyerere, amesema uzinduzi wa kiwanja hicho utafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa mkoa huo.

Baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo, akiwemo Mikidadi Machesha, msafiri wa kwanza kutoka Sumbawanga kwenda Dar es Salaam, aliyesema usafiri wa anga utarahisisha safari na kupanua wigo wa ajira.

“Zamani tulisafiri zaidi ya kilomita 1,148 hadi Dar es Salaam, lakini sasa ni saa moja na dakika 40 tu,” amesema Machesha.

Ameiomba mamlaka ya usafiri kuhakikisha kunakuwa na safari za kila siku, akibainisha kuwa uwanja huo ni lango muhimu la usafiri kwa mikoa ya jirani na nchi kama Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Abdul Mwondokaleo amesema uwanja huo una uwezo wa kuhudumia zaidi ya abiria 150,000, huku akibainisha kuwa katika kipindi cha mwanzo kutakuwa na nauli nafuu ili kuwavutia wasafiri.

Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga umegharimu zaidi ya Sh60 bilioni hadi kukamilika kwake.

Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aesh Hilary wakati akizungumza katika uzinduzi huo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aesh Hilary amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa zitakazotokana na uwanja huo, ikiwemo ajira, biashara na utalii, ili kuongeza kipato cha mkoa na Taifa kwa ujumla.

Aidha, ameiomba Serikali kuharakisha ukarabati wa meli ya MV Liemba katika Ziwa Tanganyika ili kufungua zaidi fursa za uchumi kwa wakazi wa Rukwa.

Viongozi mbalimbali walioshiriki katika uzinduzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga.

“Nimeupigania uwanja huu kwa zaidi ya miaka kumi. Kuzinduliwa kwake kutarahisisha kwa kiasi kikubwa huduma za usafiri na usafirishaji kwa wakazi wa Sumbawanga,” amesema Aesh.