Nauli ya Dar- Morogoro na Dodoma kwa reli ya SGR pasua kichwa

Behewa za Reli ya Kisasa (SGR) zilizotengenezwa na kampuni ya SSRST (Sung Shin Rolling Stock Technology) ya nchini Korea zilizowasili nchini jana Novemba 23,2022 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Muktasari:
Mapendekezo ya viwango vya nauli za abiria kwa treni ya njia ya Reli ya Kisasa (SGR) iliyotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Dodoma ni mwiba mchungu, nauli kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ni marambili ya nauli za basi.
Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limependekeza viwango mbalimbali vya nauli za abiria kwa treni ya njia ya Reli ya Kisasa (SGR) huku Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) ikiitisha maoni ya wadau.
Latra inapaswa kukusanya maoni ya wadau Desemba 19, 2022, kabla ya kufikia uamuzi wa kuridhia viwango vya nauli kwa huduma zinazodhibitiwa na mamlaka ikiwemo treni, hiyo ikiwa ni utekelezaji wa kifungu Na 21 cha Sheria Na 3 ya Latra ya mwaka 2019.
Kulingana na mapendekezo ya TRC, nauli kutoka Dar es Salaam kwenda Soga daraja la kawaida kwa mtu mzima ni Sh9,494 na mtoto wa miaka kati ya 4-12 ni Sh4,747 na kwa daraja la kati mtu mzima atapaswa kulipia Sh11,392 na mtoto ni Sh5,696.
Pia, kutoka Dar es Salaam kwenda Ruvu kupitia SGR nauli pendekezwa ni Sh14,394 na mtoto ni Sh 7,197 kwa daraja la kawaida huku daraja la kati ni Sh17,272 na Sh8,636 kwa mtoto.
Kwa upande wa Dar es Salaam hadi Ngerengere abiria atapaswa kulipia Sh19,494 na Sh9,747 kwa mtoto na daraja la kati ni Sh23,392 kwa mtu mzima na mtoto Sh11,696.
Kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro abiria atapaswa kulipia Sh24,794 na Sh12,397 na kawa daraja la kati kwa mtoto na Sh29,752 na Sh14,876 kwa mtoto.
Dar es Salaam hadi Mkata abiria daraja la kawaida atalipia Sh 30,194 na Sh17,847 kwa mtoto na mtoto.
Kwa Dar es Salaam hadi Kilosa kwa daraja la kawaida abiria atalazimika kulipia Sh35,694 na mtoto ni Sh17847 na daraja la kati ni Sh42,832 na Sh21,416 kwa mtoto
Kufika Kidete kutokea Dar es Salaam TRC wamependekeza Sh41,394 na mtoto Sh20,697 na daraja la kati ni Sh49,672 na Sh24836 kwa mtoto, pia kutoka Dar es Salaam hadi Gulwe ni Sh47,294 na Sh23,647 kwa daraja la kati ni Sh56,752 na Sh28,376 kwa mtoto.
Maeneo mengine ni kutoka Dar es Salaam hadi Igandu Sh53,294 na Sh26,647 kwa mtoto na daraja la kati ni Sh63,952 na kwa mtoto ni Sh31,976, kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ni Sh59,494 na Sh29,747 kwa mtoto na kwa daraja la kati ni Sh71,392 na mtoto Sh35,696.
Eneo la mwisho ni Dar es Salaam hadi Bahi Sh65,894 na kwa mtoto ni Sh32,947 na kwa daraja la kati ni Sh79,072 na Sh39,536 kwa mtoto.