Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nape amkaribisha Chande wizarani

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akifurahia jambo na Mkurugenzi Mkuu mpya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Maharage Chande (wa kwanza kulia).

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amekaribisha Mkurugenzi mpya wa TTCL Maharage Chande aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amekaribisha Mkurugenzi Mkuu mpya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Maharage Chande aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo hivi karibuni.

“Kipekee kabisa nikukaribishe ndugu yangu, kaka yangu, rafiki yangu, Maharage Chande. Karibu rasmi kwenye familia ya wanamawasiliano, najua umetokea huku, ni mshale umerudi nyumbani. Namshukuru Rais kwa uteuzi wako, karibu sana,” amesema.

Hayo yalisemwa leo Jumatatu Septemba 25, 2023 katika hafla ya utiaji saini hati ya maridhiano na hati ya mkataba wa nyongeza kwenye miundombinu ya mkongo wa mawasiliano kati ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na umoja wa watoa huduma za mawasiliano nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo Nnauye, amesema tukio hilo ni uthibitisho wa utayari wa Serikali kuungana na sekta binafsi katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana nchini.

Aidha amesema hatua hiyo imefikiwa kufuatia maelekezo Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza kutatuliwa kwa mgogoro uliokuwepo kati ya umoja huo na Serikali jambo lililosababisha kukwama kwa shughuli za uwekezaji.

Ameeleza kuwa baada ya kutatuliwa kwa mgogoro huo mahusiano yamerejea na tayari umoja huo umeahidi kukabidhi kwa Serikali miundombinu ya mkongo wa mawasiliano wenye urefu wa takribani kilomita 3,000.

“Kwa kutambua umuhimu wa Tehama Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watoa huduma na wawekezaji kujenga miundombinu ya mawasiliano kote nchini, nawahakikishia tutaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha,” amesema Nnauye.

Akieleza miongoni wa juhudi za Serikali katika mawasiliano amesema imepunguza gharama za kuweka miundombinu ya mkongo kutoka Sh2.5 milioni hadi Sh250,000 lakini pia inaendelea na ujenzi wa mkongo wa Taifa ambao unatarajia  kuzifikia wilaya 99 kati ya 139 ifikapo Machi 2024 huku lengo likiwa ni kufikia wilaya zote ifikapo mwishoni mwa mwaka ujao.

Ameongeza kuwa kuimarisha Tehama na mawasiliano kutasaidia kuleta maendeleo ya uchumi, kukuza biashara na kuongeza matumizi ya kidijitali katika kuimarisha sekta za kijamii.

“Ni matumaini yetu kuona Tanzania inapiga hatua katika kuongeza kasi ya matumizi ya mifumo ya kidijitali kwani kuna miundombinu ya kisasa ya Tehama na mawasiliano inayofanya kazi kwa kasi na ubora unaostahili,” amesema Nnauye.

Pia amewataka watendaji wa wizara hiyo kuhakikisha mikataba inafanyiwa kazi kwa wakati ili kuepuka ucheleweshaji wa utekelezaji wa mikataba huku akitoa rai kwa watoa huduma za mawasiliano kuendelea kuwekeza katika miundombinu inayowezesha kufikisha huduma kwa wananchi.

Katika tukio hilo, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom ilikaribishwa rasmi katika umoja huo kwani haikuwa sehemu ya umoja huo ambao mwaka 2011 wizara hiyo iliingia makubaliano na umoja huo kwa lengo la kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo ambayo mkongo wa Taifa haujafika.