Naibu Waziri ataka taasisi na mashirika kutoa kipaumbe kwa wanawake

Muktasari:
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah Ulega ametoa wito kwa taasisi na mashirika kutoa fursa kwa wanawake katika uongozi kwani kufanya hivyo kutaongeza mafanikio ya maeneo yao ya kazi.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah Ulega ametoa wito kwa taasisi na mashirika kutoa fursa kwa wanawake katika uongozi kwani kufanya hivyo kutaongeza mafanikio ya maeneo yao ya kazi.
Ameyasema hayo leo Machi 8, 2021 wakati akifungua jukwaa la The Citizen Rising Woman lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited.
Jukwaa hili limefanyika siku ambayo Tanzania inaungana na mataifa mengine katika kusherehekea siku ya wanawake duniani huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni `Mwanamke katika uongozi chachu ya kujenga usawa wa kijinsia.’
Ulega amesema anafurahi kuona baadhi ya taasisi na mashirika mbalimbali hivi sasa yakitoa fursa kwa wanawake kuongoza katika maeneo yao.
“Nitoe wito kwa taasisi na mashirika mengine ambayo bado hayajafanya kitu hiki yatoe fursa kwa wanawake kwani takwimu na uhalisia vinaonyesha kuwa wanawake wamekuwa na mafanikio makubwa wanapopewa nafasi za uongozi,” amesema Ulega, ambaye pia ni Mbunge wa Mkuranga.
Amesema jambo kama hilo pia limeshafanyika serikalini kwa kuweka viongozi wanawake katika ngazi za juu ikiwemo Makamu wa Rais na Naibu Spika kitu ambacho pia kimefanyika kwa upande wa Zanzibar.
Makamu wa Rais ni Samia Suluhu Hassan, Naibu Spika Dk Tulia Ackson na pia hivi karibuni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alimteua Zena Ahmed Said kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pia amesema hata idadi ya wabunge wanawake nao wameongezeka katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019 ikilinganishwa na zamani.
“Idadi ya wabunge wanawake waliongezeka kutoka 127 mwaka 2015 hadi 143, mwaka 2019 huku wale wa kuchaguliwa wakiongezeka kutoka 21 mwaka 2015 hadi 26 mwaka 2019,” aliongeza Ulega.
Kitu kama hicho pia kimefanyika katika ngazi za mahakama kwani idadi ya majaji wanawake wamefikia 40 kutoka 24 waliokuwapo kipindi kama hicho.
“Kwa idadi hii ya majaji mnaweza ukadhani ni jambo dogo isipokuwa kumpata huyo mmoja ni jambo kubwa,” amesema Ulega.