Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nafasi ya vyombo vya habari kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Muktasari:

  • Wadau wa habari nchini wameeleza mchango wa vyombo vya habari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, huku wakisisitiza kipimo cha demokrasia kwa nchi yeyote ni nafasi ya vyombo hivyo na uhuru wa kufanya kazi bila kuingiliwa.

Dar es Salaam. Wadau wa habari nchini wameeleza mchango wa vyombo vya habari kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, huku wakisisitiza kipimo muhimu cha demokrasia katika nchi yoyote duniani ni nafasi ya uhuru wa vyombo vya habari kufanya kazi bila kuingiliwa.

Hata hivyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi leo Julai 9, 2025 akizungumza kwenye kikao cha wadau wa habari kilicholenga kujadili jinsi ya kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 unafanyika kwa amani, haki na utulivu, amesema vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika mchakato huo.

Amesema sekta ya habari ina mchango mkubwa katika kulinda amani, kudumisha usawa na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi, hasa katika ulimwengu wa sasa ambapo taarifa potofu, kauli za chuki na unyanyasaji zimeongezeka.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa vyombo vya habari kuzingatia weledi na viwango vya maadili ili kulisaidia Taifa kupita katika kipindi hiki nyeti bila migogoro.

Wakizungumza kwenye mjadala wa Mwananchi X Space, ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) uliofanyika leo Jumatano Julai 9, 2025 wenye mada isemayo: Nafasi ya vyombo vya habari katika kukuza demokrasia wakati wa uchaguzi.

Wamesema vyombo vya habari  vinapaswa kuwa huru, kutoingiliwa, kuihabarisha jamii bila upendeleo sambamba na kutoegemea eneo moja.

Akichangia mjadala huo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan) Edwin Soko amesema kipimo cha demokrasia kwa nchi yeyote ni vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa.

"Vyombo vya Habari vinatumika kama jukwaa la majadiliano ya umma, lazima umma uchague majukwaa mbalimbali kikubwa zaidi jukwaa la vyombo vya habari ndilo linaaminika zaidi, watu wanaamini zaidi vyombo vya habari mtu anaweza kusema usibishane na chombo cha habari nimesikia redioni taarifa fulani," amesema.

Pia, Soko amesema vyombo vya habari vinapaswa kutumika kufichua uovu kwenye uchaguzi ikiwemo vitendo vya kutishiana amani, rushwa hivyo vitu vya namna hiyo vinavyoweza kuathiri uchaguzi lazima vifichuliwe.

"Serikali inaweza kutumia njia zingine lakini vyombo vya habari vikiamua kuweka mikakati uchaguzi utafanikiwa kwa kiasi kikubwa," amesema.

Mchangiaji wa mjadala huo, Tuwa Sauti ya Haki, amesema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kukuza demokrasia kwa kutoa taarifa zinazohitajika na jamii, bila kusubiri taarifa kutoka serikalini au kwa watu binafsi.

Aidha, amesema vyombo hivyo vinapaswa pia kuwa na ujasiri wa kuikosoa Serikali kistaarabu na kuonesha upungufu ili iweze kujirekebisha. Haki amesema endapo vyombo hivyo vitasimamia misingi ya kutoa habari kwa uwazi bila upendeleo, vitajijengea uaminifu kwa umma na vitafuatiliwa na watu wengi zaidi.

“Vyombo vyetu mara nyingi hushindwa kuripoti baadhi ya mambo yanayotokea nchini, jambo linalochangia kuleta hali ya kutokuwa na usawa,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa vyombo vya habari Tanzania, Seleman Msuya amesema vyombo vya habari vinapaswa kuripoti kwa usawa ili kila mtu apate kile kinachostahiki.

Katika kufanya hivyo lazima viwe na mtaji wa kuripoti bila ya kutegemea wadau akitolea mfano vyama vya siasa hasa katika kampeni. Amesema ni matamanio yao kuona vyombo vikienda kuripoti kwenye kampeni viwe na magari yao, nauli na vyakula bila kutegemea chama husika.

“Lazima tujikite kwenye uwekezaji na kuonesha mipango kazi yetu kabla ya kuanzisha vyombo hivyo. Wanahabari hawapaswi kuleta changamoto bali kama kikwazo kitokee kwa chama husika,” amesema.

Naye Mhariri wa Gazeti la Nipashe, Salome Kitomari amesema vyombo vya habari vinao wajibu wa kutoa elimu kwa umma ili wananchi washiriki shughuli za kisiasa nchini.

Salome amesema vyombo vya habari vinapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu uboreshaji wa taarifa za mpiga kura, michakato ya mabadiliko ndani ya vyama vya siasa, mabadiliko ya sheria mbalimbali za uchaguzi, shughuli za kampeni hadi wagombea wanapotangazwa.

"Tuna wajibu wa msingi wa kutoa habari kwa uwazi kwa maana tunahakikisha taarifa zipo kwenye mizani ya kila sauti kusikika iwe ya pembezoni na vyama tofautitofauti,

“Kuna vyama takribani 18 vimesaini kanuni za maadili kushiriki uchaguzi mkuu hivyo tuna wajibu wa kuhakikisha sauti za vyama vyote zinasikika," amesema Salome.

Mbali na hayo, Salome amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kukuza uhuru wa mawazo na demokrasia kwa ujumla nchini kupitia radio, luninga, mitandao ya kijamii kwa kuruhusu watu kutoa maoni yao.

Akizungumzia suala la uchaguzi huru na haki, Salome amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina wajibu wa kuwaeleza wananchi mabadiliko ya sheria ya uchaguzi yaliyofanyika na vipengele gani wanapaswa kuvizingatia.

"Wakati mwingine tunapaswa kuripoti ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi, sheria na kanuni zipo, yapo mambo hayaonekani kuendana na sheria zilizopo tunapaswa kuziandika na kuzitangaza,” amesema.