Mzumbe kuleta suluhu tatizo la ajira kwa wahitimu

Muktasari:
- Tatizo la ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu huwenda likapata suluhisho kupitia na mradi unaotekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe unaolenga kuwajengea uwezo wahitimu vyuo vya elimu ya juu na kati, kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Dar es Salaam. Chuo Kikuu Mzumbe kimeingia katika ushirikiano na sekta ya Viwanda nchini katika kupata suluhisho la tatizo la ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu, linalotokana na kukosa ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Ushirikiano huo baina ya chuo hicho na sekta ya viwanda ni sehemu ya utekelezaji wa mradi unaosimamiwa na chuo hicho wa Elimu ya Juu katika Mageuzi ya Kiuchumi, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.
Katika kutekeleza jukumu hilo imeundwa kamati ya watalaamu inayojumisha wajumbe kutoka pande zote mbili ya ushauri kuhusiana na mahitaji ya soko kwa wahitimu hususan katika sekta ya viwanda.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Mwegoha amesema kuwa wahitimu wengi wanapata ugumu kuingia katika soko la ajira kutokana na kukosa ujuzi wa kiutendaji unaohitajika.
"Ili kutatua changamoto ya ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko na uchumi wa sasa kwa wahitimu wetu, sisi Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi kichumi tumedhamiria kujenga muunganiko imara kati ya elimu ya juu na sekta ya viwanda.", amesema Prof Mwegoha.
Amesema kupitia muunganiko huo wanafunzi watanufaika na fursa za mafunzo kwa vitendo kwa baadhi ya kozi na utaalamu kutoka viwandani ambavyo vitawapatia ujuzi wa moja kwa moja kutoka kwenye soko la ajira.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, amesema kuwa kumekuwa na kilio cha malalamiko kutoka Sekta binafsi kwamba wanapochukua waajiri wapya kutoka vyuoni walazimika kuwapeleka nje kuwafundisha tena ili wawe vizuri kwenye maeneo yao ya kazi.
Amesema kuwa hata tafifi zilizofanywa na umoja wa waajiri mwaka 2004, 2012 na 2014 zote zilitoa matokeo kwamba wahitimu hao hawaendani na mahitaji ya soko.
Hivyo amesema kupitia kamati hiyo itajibu changamoto hiyo kwani kama tatizo liko kwenye mitaala watashughulika nayo ili wahitimu waweze kukidhi mahitaji ya soko katika sekta hiyo ya viwanda kitaifa, Afrika na Dunia kwa jumla.
Mratibu wa mradi huo wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitalamu, Elizabeth Mwakasungula alisema kuwa mradi huo umetengewa Dola za Marekani 21 milioni.
Amesema kuwa mradi huo pamoja na mambo mengine unahusisha kuboresha mitaala na kuanzisha mbinu bunifu za kufundishia, kukuza utafiti na uwezo wa uchunguzi, kununua vifaa vya kisasa vya Tehama, kujifunza kupitia mtandao na kujenga mahusiano mazuri kati ya chuo na Sekta ya Viwanda.
Alisema malengo ya kamati hiyo ni kujenga muunganiko mzuri kati ya chuo na sekta ya ajira katika kutoa ushauri na kushirikisha uzoefu juu ya maendeleo, mchango wa viwanda na ukuaji wa uchumi, fursa za ajira na mafunzo kwa vitendo.