Mzee wa miaka 74 adakwa kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa miaka 10

Mtoto (10) wa darasa la tatu aliyebakwa na mzee wa miaka 74 Mtaa wa Rwelu Manispaa ya Mtwara mikindani. Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Mzee wa miaka 74 mkazi wa Mtwara ashikiliwa kwa kosa la kubaka mtoto wa darasa la tatu (10) baada ya kumona mtoto huyo akiwa na usingizi hivyo kumuelekeza kwenda kulala ndani kwake ambapo alitekeleza tukio hilo.
Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia Hemed Mshamu (74), Mkazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 10, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Rwelu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 16, 2023; Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mtaki Kurwijila amesema kuwa mtoto huyo alikuwa na kawaida ya kucheza jirani na nyumba yao anayoishi mzee huyo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, tukio hili limetokeo Novemba 10, 2023; saa 10 jioni, baada ya mtoto kwenda kucheza jirani na nyumbani kwa mtuhumiwa, baada ya babu na bibi yake kwenda shambani.
Imeelezwa kuwa baada ya kucheza, mtoto huyo alihisi usingizi ambapo inadaiwa Mshamu alimwelekeza kwenda kulala chumbani kwake, na kwamba mtuhumiwa alitumia nafasi hiyo kutekeleza azma yake ya kumuingilia kimwili, jambo lililomsababisha mtoto huyo kupata maumivu sehemu za siri.
“Baada ya bibi kurudi alibaini kuwa mjukuu wake hatembei vizuri na baada ya kumuhoji ndipo alipomweleza kuwa alikuwa amebakwa na mtuhumiwa huyo hivyo alimuwahisha Kituo cha Polisi kisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula kwa ajili ya vipimo ambapo ilibainika kuwa ameingiliwa,” amesema.
Upelelezi wa tukio hilo umekamilika na muda wowote jalada hilo litafikishwa ofisi ya Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Mtwara kwa hatua zaidi.
Kwa upande wa bibi wa mtoto huyo, jina linahifadhiwa), amesema kuwa alimuandaa mtoto aende shule lakini alikataa maana alikuwa anaumwa mguu.
“Nikatoka, niliporudi nilimkuta mtoto amekaa kwenye kona ya nyumba analia nikamuuliza unalia nini au unaumwa akasema hapana lakini akasimulia kisa chote kilichotokea mpaka kubakwa tukashangaa tukaenda kwake mzee Mshamu kumuuliza lakini alikataa,” amesema na kuongeza;
“Tulipo mpeleka hospitali watalaamu wakadhibitisha kuwa ni kweli amefanyiwa vitendo hivyo babu amemdharirisha mtoto na amemuharibu.”
Mtoto huyo amesema kuwa alikuwa anacheza na watoto wenzie nje ya nyumba ya mzee huyo ambapo akiwa amejilaza nje aliambiwa na mzee huyo akalale ndani.
“Nilikuwa nacheza wengine wakatandika mimi nikalala yeye alinikuta akaniambia niende kulala nikaenda kulala nilipolala akaja akanifunua akanibana mdomo na mkono kisha akanibaka naogopa hata kutembea ilikuwa ni mara ya nne alikuwa akinifanyia lakini niliogopa kusema kwakuwa aliniambia kuwa atanichinja nikisema kwa watu,” amesema.
Mtoto huyo ameongeza kusema kuwa: “Nyumbani kwa mzee huyo jirani na nyumba yake kuna udongo watoto wengi huwa tunaenda kukuchukua watoto wengi huwa wanapenda kwenda pale lakini mimi ndio alikuwa akinionea na kunitisha.”
“Unajua wakati ananibaka aliniziba mdomo na aliniumiza miguu mpaka sasa siendi shule yaani miguu inauma,” amesema mtoto huyo.