Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwili wa mtoto aliyejinyonga Mirerani waagwa

Ndugu, jamaa na marafiki wakazi wa kitongoji cha Kilimahewa kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wakiwa mbele ya jeneza lenye mwili wa marehemu Vaileth Soka (13) aliyefariki dunia kwa kudaiwa kujinyonga. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Mtoto Vaileth Innocent Soka (13) alifariki dunia kwa kudaiwa kujinyonga Julai 18, 2026 katika kitongoji cha Kilimahewa kata ya Endiamtu, mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Mirerani. Mwili wa mtoto Vaileth Soka (13) aliyefariki dunia kwa kudaiwa kujinyonga umeagwa katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Kibosho Umbwe wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro kwa maziko.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Innocent Soka, akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Julai 23, 2026 amesema tukio hilo limempa pigo kubwa, lakini anamwachia Mungu. Amesema alikuwa akiishi na watoto wake wawili wa kike baada ya kutengana na mama yao, lakini sasa amebaki na mmoja.

"Binti yangu alikuwa mcheshi na asiyependa kuweka vitu moyoni, ila nimesikitishwa na sikutegemea kuchukua uamuzi mgumu kama huu," amesema Soka.

Amesema tukio hilo lilitokea Jumamosi Julai 18, 2026, siku ambayo hakukuwa na masomo kwa kuwa Vaileth alikuwa akisoma darasa la sita katika Shule ya mchepuo wa Kiingereza Mirerani.

Betha Shayo (katikati) mama mzazi wa mtoto Vaileth Soka (13) aliyekuwa mkazi wa kitongoji cha Kilimahewa kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, aliyefariki dunia kwa kudaiwa kujinyonga, kulia mwenye picha ni dada wa marehemu Vicky Soka. Picha na Joseph Lyimo

Soka amesema chanzo cha tukio hilo kilikuwa kumkuta mtoto huyo akiangalia maudhui yasiyofaa kwenye luninga kupitia flashi ambayo hakujua ilipotoka na kuanza kumuhoji.

Amesema alimwelekeza aoshe vyombo akiwa dukani, lakini baadaye alisikia ukimya ndani na kuingia kuona kilichokuwa kinaendelea. Alipomkuta akiangalia maudhui hayo alimkemea bila kumpiga na kumwambia wasubiri dada yake arudi kutoka masomo ya ziada ili wazungumze.

Amesema dada yake, Vicky Innocent, aliporudi na kuingia ndani alipiga ukunga na kutoka nje. Alipoulizwa alieleza kuwa Vaileth amejinyonga. Majirani walifika na kusaidia kumshusha baada ya kujinyonga sebuleni kwa kutumia kanga.

"Niliweka mapajani, nikamkandamiza kifuani na kumpulizia hewa kwa mdomo, lakini sikuweza kumsaidia kwani alikuwa ameshafariki," amesema Soka.

Amesema walitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mirerani na kuandika maelezo yeye na binti yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Ahmed Makarani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi walifanya uchunguzi kisha kuukabidhi mwili kwa ndugu kwa ajili ya maziko.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kilimahewa Kata ya Endiamtu, Andrew Nyambo, amesema Soka alikuwa baba bora aliyewalea watoto wake kwa upendo na hajawahi kupata malalamiko ya manyanyaso.

Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Kilimahewa kata ya Endiamtu mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wakibeba jeneza lenye mwili wa marehemu Vaileth Soka (13) aliyefariki dunia kwa kudaiwa kujinyonga. Picha na Joseph Lyimo

Jirani na balozi wa nyumba 10, Mwantumu Abdalah, amesema Soka amejitahidi kuwalea watoto wake wawili wa kike na ni mtu anayeshirikiana vizuri na jamii.

Mkazi wa eneo hilo, Samwel Kaaya, amemwelezea Vaileth kuwa wakati wa uhai wake alikuwa binti mcheshi na mwenye busara.