Prime
Mwili uliookotwa Coco Beach wabainika wa Dk Hashimu aliyepotea

Muktasari:
- Aprili 24, 2025 Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kwa umma kuhusu mwili wa mwanamume ambaye hajafahamika jina wala makazi yake kukutwa kwenye mchanga wa ufukwe wa bahari, eneo la Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Mwili wa mwanamume uliopatika kwenye ufukwe wa Coco, jijini Dar es Salaam, Aprili 24, 2025 umebainika ni wa mwanafunzi wa udaktari bingwa wa upasuaji Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Hashimu Tito.
Dk Tito pia alikuwa daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mtwara.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jambo hilo alishalizungumza.
“Rudini kwenye ile taarifa yangu ya mwanzo mtaliona,” amesema.
Katika taarifa kwa umma ya Aprili 24, 2025, Polisi katika kanda hiyo ilieleza kuhusu mwanamume kukutwa eneo la ufukwe wa Coco, Oysterbay na baadaye kubainika kuwa amefariki dunia.
Taarifa hiyo ilisema Aprili 24, 2025 saa tano asubuhi katika eneo hilo lililopo wilayani Kinondoni, mtu mmoja mwanamume ambaye hajafahamika jina wala makazi yake, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35 alikutwa akiwa kwenye mchanga wa ufukwe wa bahari, hajitambui.
Ilielezwa kuwa alikuwa amefungwa bandeji ngumu ya muda mrefu (PoP) kwenye mkono wa kulia.
“Taarifa hiyo ilifikishwa Polisi na watu wanne wafanyabiashara ndogondogo wa eneo hilo, ambao pia hawamtambui mtu huyo ambaye alipelekwa Hospitali ya Mwananyamala ambako ilithibitika kuwa alikuwa ameshafariki dunia na maiti imehifadhiwa Hospitali ya Polisi Kilwa Road kutokana na matatizo ya nafasi ya kuhifadhi hospitali ya awali. Uchunguzi juu ya chanzo cha kifo hicho unaendelea,” ilieleza taarifa hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji katika idara ya Upasuaji Muhas, Dk Ali Mwanga akizungumza na Mwananchi leo Juni 6, amesema taarifa za kupotea kwa daktari huyo zilitolewa awali na familia, baada ya kushindwa kumpata nyumbani na kwenye maeneo yake ya kazi.
“Tulianza kumtafuta kwa kushirikiana na ndugu zake baada ya kugundua hayupo kazini wala nyumbani, juhudi hizo zilihusisha vyombo vya usalama na matumizi ya mitandao ya kijamii,” amesema Dk Mwanga.
Katika harakati hizo za utafutaji, amesema walikumbushwa kuhusu tangazo lililotolewa na Kamanda Muliro, Aprili 24, 2025 kuhusu kuokotwa mwili wa mtu asiyefahamika kando mwa bahari akiwa katika hali mbaya.
Taarifa hiyo aliyosema hawakuipa uzito mkubwa wakati huo, ilielezea mtu aliyekuwa na jeraha mkononi, maelezo yaliyofanana na hali ya Dk Hashimu aliyekuwa amefanyiwa upasuaji kabla ya kutoweka kwake.
Amesema kwa kushirikiana na familia walikwenda polisi kufuatilia suala hilo ambako walielezwa mwili ulipelekwa Hospitali ya Polisi Kilwa Road.
Dk Mwanga amesema familia na vyombo vya usalama walifuatilia na hatimaye kutambua mwili huo kuwa ni wa daktari aliyepotea, kupitia picha na alama za mwili.
“Tulishirikiana na baba yake mzazi pamoja na kaka zake ambao walithibitisha kwa macho yao kuwa mwili ni wa Hashimu baada ya kuonyeshwa picha,” amesema Dk Mwanga.
Kuhusu hatua zinazofuata, Dk Mwanga amesema taratibu za kitaalamu, zikiwamo uchunguzi wa vinasaba (DNA) zinaendelea kwa kushirikiana na vyombo vya dola ili kuhakikisha uthibitisho kamili wa utambulisho wa marehemu.
Amesema mpaka sasa chanzo cha kifo hakijajulikana na uchunguzi wa kina unaendelea kufanywa na vyombo vya usalama.
Mwananchi lilipomtafuta Tito Mwatowine, baba mzazi wa Dk Hashimu amesema mambo ni mengi hawezi kuelezea lolote kwa sababu mwili bado upo kwenye uchunguzi.
“Kwa hiyo siwezi kukwambia lolote yaani hatujamaliza, leo bado tunaendelea tutahabarishana,” amesema.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema kunahitajika uchunguzi zaidi, kwani kifo hakizoeleki kinakuja na maumivu yasiyoelezeka.
Amesema daktari kufariki ni maumivu makali, ni hasara kwa uwekezaji uliofanyika, kumpata mwingine itachukua muda hasa anapofariki akiwa mdogo.
“Tunaziita mamlaka husika zifanye uchunguzi wa kina kubaini sababu za kifo cha aina hii, kwa daktari huyu kijana na mwanafunzi wa shahada ya upasuaji wa Muhas, ili tuwalinde na kuzuia vijana hawa kufa mapema," amesema.