Mwenyekiti wa mtaa auawa kwa kukatwa mapanga Geita

Aliyekua mwenyekiti wa Mtaa wa Mwatulole katavya Buhalahala  mjini Geita Noel  Ndasa aliyeuawa kwa kukatwa mapanga akiwa nyumbani kwake enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Wauaji wanadaiwa walifika nyumbani kwake kutaka huduma za kupewa kibali cha kusafirisha mifugo.

Geita. Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwatulole, Kata ya Buhalahala Mjini Geita, Noel Ndasa ameuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali mwilini na watu wasiojulikana.

Tukio hilo limetokea jana Juni 23, 2024 saa moja usiku, baada ya wanaume wawili kufika nyumbani kwake, wakidai wanataka huduma ya kupewa kibali cha kusafirisha mifugo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea na mpaka sasa hakuna aliyekamatwa kuhusishwa na tukio hilo, huku akiahidi baadaye taarifa rasmi itatolewa.

Akisimulia tukio hilo, Ofisa Mtendaji  Mtaa wa Mwatulole,  Emanuel Bomani amesema mauaji hayo yalifanyika saa moja usiku na mwenyekiti huyo alifikwa na mauti baada ya kutoka kwenye mkutano wa mkuu wa wilaya alirudi nyumbani kwake na kukuta ugeni wa watu waliokuwa wakimsubiri.

“Watu hao walikuja kupata huduma nyumbani kwake na walieleza shida yao wakati akiwahudumia ndio walianza kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili na watoto walikuwa nyumbani na ndio waliowakaribisha.

Mjane wa marehemu Noel Ndasa, Ester Daud (kushoto) akiomboleza wakati akiwa ndani ya nyumba yao katika mtaa wa Mwatulole mkoani Geita.

“Wakati tukio linatokea watoto walikuwa wanaona, lakini kwa udogo wao hawakuweza kufanya chochote,” amesema Bomani.

Amesema hawakuwahi kusikia kama mwenyekiti huyo ana mgogoro, kwani na alikuwa akiishi vyema. Pia alikuwa mtu wa watu bila kuchagua na wakati wote hutoa huduma kwa jamii bila kujali muda.

Unice Noel, mtoto wa marehemu amesema jana jioni wakati akianua nguo nje waliingia wanaume wawili waliosukuma geti na kuhoji iwapo mwenyekiti yupo na walipoambiwa hayupo, walieleza kuwa wanamsubiri. Walipewa viti na kukaa.

 “Baada ya muda baba alifika na kuingiza pikipiki na hao wageni wakasema wana shida ya kibali cha kusafirisha ng’ombe, baba akaingia ndani kuchukua karatasi na kalamu. Mmoja aliyekuwa amevaa suti akaingia bafuni akatoka na panga, baba alivyokuwa anatoka ndio wakaanza kumkata baada ya yule mwingine kumpiga na rungu kichwani,” amesema Unice

Ndugu na waombolezaji wakiwa nyumbani kwa marehemu Noel Ndasa katika mtaa wa Mwatulole Geita.

Amesema walipoona tukio hilo walikimbia na kujifungia ndani na kupiga kelele kuomba msaada, bila mafanikio na baadaye watu walijitokeza wao wakiwa wamejifungia chumbani.

Ester Daud, mke wa marehemu amesema waliachana na mumewe saa tisa alasiri kuwa anakwenda kwenye kikao, huku naye akawa anakwenda kwa dada yake.

Baadaye alipompigia simu mumewe, ili amweleze kuwa yuko njiani anarudi, simu haikupokelewa.

Amesema hakuwahi kusikia kuwa mumewe kuwa na mgogoro na mtu na amekuwa akiwahudumia wananchi muda wowote.