Mwenyekiti wa kijiji auawa, atupwa mtaroni Dodoma

Muktasari:

  • Wakazi wa Kijiji cha Kisokwe wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wamekumbwa na sintofahamu baada ya mwenyekiti wa kijiji hicho kuuawa na kutupwa katika mtaro.

Dodoma. Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisokwe wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, Patrick Nyangauya amekutwa amefariki dunia na mwili wake kutupwa kwenye mtaro na kufunikwa na majani.

Akizungumza leo Jumatano Januari 17, 2024 kijijini hapo, Mtendaji wa Kijiji cha Kisokwe, Anna Fundichuma amesema alipigiwa simu na mwalimu kuwa kuna maiti imeonekana pale shuleni.

“Nikawasiliana na viongozi (bila kuwataja) ambao walikuja na baada ya kufunua mwili tukagundua ni mwenyekiti wa kijiji chetu. Ni huzuni kubwa imetukumba,” amesema.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Patrick Msumba amesema hawawezi kufahamu sababu hasa ya mauaji hayo na kwamba si mara ya kwanza kitokea mauaji kama hayo.

“Kama ni sababu za mazingira hatujui, kama ni sababu ya kutembea kwa wake za watu pia hatujui, walimua kwa sababu gani ama kwa mazingira gani,” amesema.

Girbert Chalula ameiomba Serikali kufanya uchunguzi wa mauaji yanayojirudia katika kijiji hicho ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

“Ni sehemu hiyohiyo inayokutwa watu wamekufa. Tunaomba waweze kuja kufanya uchunguzi wa kina kijijini kwetu,”amesema.

Mdogo wa marehemu, Baraka Nyangauya amesema madaktari wamepima mwili wa marehemu na kubaini hakuna sehemu yoyote aliyopigwa.

“Hatujui sababu nini. Tuliukuta mwili katika mtaro. Watu wengi wanalia kwa sababu hakuwa mtu mwenye tabu na yeyote,”amesema.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno ameahidi kumrudia mwandishi baada ya dakika moja, lakini baada muda simu yake iliita bila majibu.