Anayedaiwa kubaka mwanafunzi auawa na wananchi

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Gilles Muroto akizungumza kuhusu ongezeko la ubakaji Mkoa wa Dodoma

Muktasari:

Mtu mmoja amekufa mkoani Dodoma baada ya kushushiwa kipigo na wananchi akituhumiwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili mwenye umri wa miaka nane

Dodoma. Mtu mmoja amekufa mkoani Dodoma baada ya kushushiwa kipigo na wananchi akituhumiwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili mwenye umri wa miaka nane.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema leo Alhamisi Julai 4, 2019 kuwa mtu huyo ambaye jina lake halijafahamika, alikuwa akihusishwa na matukio mengine ya ubakaji katika mtaa wa Mailimbili mkoani humo.

Amesema alikuwa akiwakwepa polisi na jana alikutwa akifanya unyama huo katika jengo ambalo halijakamilika ‘pagale’.

Jeshi hilo pia linamshikilia Mazengo Chilatu (28) kwa tuhuma za  kumlawiti mama yake mzazi huku,  Donald Justin (25) akishikiliwa kwa kosa la kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 95.