Aliyedaiwa kuua mke, mkwe naye auawa

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Mama mkwe alienda kumsalimia mwanaye kabla kukumbwa na mauti hayo yaliyosababishwa na mkwewe ambaye aliuawa na wananchi pia.

Dodoma. Mkazi wa Seguchini, Kata ya Nala, Wilaya ya Dodoma Mjini, Festo Maganga anadaiwa kumuua mkewe na mama mkwe wake, kisha yeye kuuawa na wananchi.

Tukio hilo limetokea jana Jumapili Januari 28, 2024 saa 10.30 jioni katika Mtaa wa Seguchini.

Akizungumza na Mwananchi Digital, mmoja wa ndugu za marehemu hao, Samwel Lengole amesema wiki iliyopita mama mkwe, ambaye ni mama wa mke wa mtuhumiwa, Anna Ngalai alikwenda kwa mwanaye Maria Joseph kusalimia.

Hata hivyo, amesema jana saa 10.30 kuelekea saa 12 jioni pasipo kufahamu ni nini kilitokea, ilikutwa miili ya mama na mtoto wake jikoni ikiwa imechomwa na kitu chenye ncha kali shingoni.

"Hatufahamu kilitokea nini maana hapa nyumbani hapakuwa na mtu mwingine zaidi yao. Jikoni kulikutwa wakipika makande," amesema Lengole.

Amesema baada ya wananchi kukuta miili hiyo, walianza kumsaka mwanamume huyo, ambaye alikutwa kwa mwenyekiti wa mtaa anakodaiwa alienda kujisalimisha baada ya tukio hilo.

Lengole amesema baada ya kuwaona watu wamevamia, mwenyekiti alijaribu kuzuia wasimdhuru mtuhumiwa lakini hakufanikiwa baada ya wananchi kusukuma geti na kuungia ndani.

Amesema wananchi baada ya kuingia ndani, walimweleza mwenyekiti kuwa salama yake ni aache wafanye shughuli yao na kwamba asipofanya hivyo watamchanganya na mhalifu huyo.

Lengole amesema wananchi hao walimvamia mtuhumiwa na kumuua kwa kumpiga kisha wakaondoka.

Amesema wawili hao walikuwa na ugomvi unaohisiwa unatokana na wivu wa kimapenzi, lakini kuuawa kwa mama mkwe ndiko kunaacha maswali ya nini kilitokea hadi akafikia uamuzi huo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amethibitisha tukio hilo akisema taarifa atazitoa baadaye.