Mume adaiwa kumchinja mkewe, atupa viungo mtoni

Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Njombe, Joseph Malongo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Dombwela wilayani Makete mkoani Njombe baada ya kutokea mauaji ambapo inadaiwa mume kumuua mkewe.

Muktasari:

  •  Alimmcharanga mapanga mkewe  kisha kutupa sehemu ya viungo vyake mtoni katika Wilaya ya Makete mkoani Njombe.

Njombe. Polisi Wilayani Makete, Mkoa wa Njombe, inamshikilia mkazi wa wilaya hiyo Juma Kyando (36), kwa tuhuma za za mauaji ya mkewe Tumaini Luvanda (35), ambapo inadaiwa mtuhumiwa alimchinja na kutenganisha kichwa na kiwiliwili.

Kama hiyo haitoshi, inadaiwa kuwa baada ya kumchinja, mtuhumiwa aliukata mwili huo vipande vipande na kisha kutupa baadhi ya viungo kwenye mto, huku vingine akivitupa jirani na nyumba yake eneo la Kabinda lililopo wilayani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kudai kuwa kesho atatolea ufafanuzi zaidi.

"Tukio kweli limetokea lakini kesho nitalitolea ufafanuzi nitakapozungumza na wanahabari," amesema Kamnda Banga.

Kwa upande mwingine, akizungumza na wananchi wilayani Makete, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Njombe, Joseph Malongo amesema jeshi hilo limepokea tukio hilo kwa masikitiko kutokana na mtuhumiwa huyo kufanya kitendo cha kikatili na kujichukulia sheria mkononi.

Amesema Polisi linamshikilia mtuhumiwa huyo na kwamba litahakikisha hatua za kisheria zinachuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakama mara tu upelelezi utakapokamilika.

"Watu wanasumbuliwa na msongo wa mawazo, nawatakeni na nawaombeni msiyarundike matatizo yenu, mshirikishe watu pengine inaweza kusaidia,” amesema Malongo.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Iwawa Joseph Mbilinyi amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Januari 8, 2024 katika Kijiji cha Dombwela.

Kwa mujibu wa Mbilinyi ambaye pia ni na Mwenyekiti wa Mtaa wa Dombwela, alipigiwa simu na jirani yake kuwa kuna mtu anamshambulia mke wake ndipo akaelekea eneo la tukio na alipofika pale alikuta mtuhumiwa kashika panga na anatisha kiasi cha kushindwa hata kumsogelea.

Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kumkatakata mapanga mkewe ambaye kwa sasa ni marehemu, alichukua baadhi ya viungo vya mwili huo na kwenda kuvitupa kwenye mto.

"Baada ya kumuuma kwa kumkata mapanga alimuweka kwenye mfuko kisha kwenda kumtupa kwenye mto, ila uwanjani jirani na nyumbani kwake, tulikuta moyo wa mtu ambao aliumtoa baada ya kumuua,” amesema Mbilinyi.

Naye ndugu wa mtuhumiwa wa mauaji hayo, Medrick Kyando amesema ndugu yake hana historia ya kuwa na matatizo ya akili, hata hivyo, ameshangaa kuona ametekeleza tukio hilo la kikatili kwa mke wake huyo na kusababisha sintofahamu kwa majirani.

"Ndugu yetu hana historia ya tatizo la akili ni fundi ujenzi, alikuwa hana makundi na hata tulipopigiwa simu kuhusu tukio hilo tulishtuka sana," amesema Kyando.

Baadhi ya majirani akiwemo Jeita Nkwama amesema jirani yao alikuwa anaishi vizuri na mke wake na hajawahi kusikia matukio yoyote ya ajabu lakini wameshanngaa kuona ametekeleza tukio la kikatili kwa mke wake.

"Hatuwezi kujua shida ni nini na hatuamini kama kuna binadamu anaweza kutenganisha kila sehemu ya viungo vya mkewe kama mnyama," amesema  Nkwama.