Mwanamke atuhumiwa kumuua mumewe kwa nyengo

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia Tressfolina Nkolongo (33) mkazi wa Viziwi mtaa wa Mji Mwema uliopo halmashauri ya mji wa Njombe kwa tuhuma za kumuua mume wake Bosco Mhagama (53) kwa kumpiga na nyengo kichwani na kusababisha kifo chake.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.

Amesema tukio hilo la mauaji lililofanywa na mtuhumiwa huyo limetokea Oktoba 16, mwaka huu mnamo saa tano ya usiku hapa halmashauri ya mji wa Njombe.

Amesema chanzo cha mwanamke huyo kumpiga mume wake kwa nyengo kichwani inadaiwa kuwa alikuwa anazuia asiendelee kumpiga mtoto wake ambaye alikuwa akimuadhibu.

Amesema jeshi hilo litamfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo wakati wowote baada ya taratibu za uchunguzi kukamilika ili taratibu za  kisheria ziweze kufuatwa.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linaendelea kutoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani inasababisha madhara mengi ikiwemo mauaji," amesema Banga.

Amesema katika kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili jeshi hilo litaendelea na mkakati wa kuwakamata wahusika wa matukio hayo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Amesema jeshi hilo limejipanga kuimarisha ulinzi kwenye maonyesho ya biashara ambayo yanatarajia kuanza Oktoba 21 na kumalizika Oktoba 26, 2023.

Mmoja ya wakazi wa Mkoa wa Njombe, Winfrida Batwel ameshauri kunapotokea migogoro kwenye familia ni vizuri wakatoa taarifa katika uongozi wa mtaa ili mwafaka uweze kupatikana kuliko kujichukulia sheria mkononi.

"Panapotokea migogoro ndani ya familia waliona imeshindikana kabisa ni bora wakaripoti katika uongozi wa mtaa kuliko kujichukulia sheria mkononi mwisho wake huwa mbaya," amesema Batwel.