Sakata la Mpina, Mwinyi kupewa miaka saba kuibukia vikao vya CCM?

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chana cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan ataongoza vikao vya vya juu vya chama hicho Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) Juni 29 na 30, 2024.

Dar es Salaam. Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) inatarajiwa kuketi Juni 30, 2024, pamoja na mambo mengine masuala sita yakitajwa kuwa na uwezekano wa kuibuka.

Msimamo wa CCM kuhusu mgomo wa wafanyabiashara nchini, chokochoko za kumwongezea muda wa kukaa madarakani Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na hatua za chama hicho dhidi ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina yanatajwa kuwa huenda yakaibuka.

Ajenda nyingine ni tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali iliyopitishwa jana Juni 26, 2024, ripoti ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho, uchaguzi wa serikali za mitaa na tathmini ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi katika mikoa 11.

Hata hivyo, taarifa kwa umma iliyotolewa leo Alhamisi Juni 27, 2024 na Katibu wa Itikadi na Uenezi na CCM, Amos Makalla imeelezea tu kuwa vikao hivyo, vitafanyikia jijini Dar es Salaam, chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan bila kuweka wazi agenda zake.


Mgomo wafanyabiashara

NEC hiyo inaketi katika kipindi ambacho, wafanyabiashara katika mikoazaidi ya saba nchini wanaendesha mgomo kwa kufunga maduka, kushinikiza utekelezaji wa mapendekezo yao baada ya mgomo wa Mei mwaka jana, kadhalika kutatuliwa kero zao.

Vuguvugu la mgomo huo lilianza Juni 22, mwaka huu katika eneo la Kariakoo baada ya kusambazwa vipeperushi vikiwataka wafanyabiashara wafunge maduka yao.

Hali iliendelea hivyo kwa siku tatu, mikoa iliendelea kuongezeka na hadi imefikia 10 – Dar es Salaam, Iringa, Arusha, Dodoma, Mbeya, Kagera, Kigoma, Morogoro, Ruvuma na Mtwara.

Serikali iliwaita wafanyabiashara mkoani Dodoma kuketi nao na uamuzi ulifanyika wa kusitisha ukaguzi wa risiti za EFD.

Kutokana na mazingira hayo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema NEC haina budi kujadili mgomo huo.

Umuhimu wa NEC kulijadili hilo unatokana na waandamanaji nchini Kenya kuwapa nguvu na matumaini wafanyabiashara katika kushinikiza Serikali kushughulikia mambo yao.

“Hili linatokana na ukweli kwamba maamuzi ya Rais William Ruto wa Kenya kutotia saini Muswada wa Fedha wa 2024, ni uthibitisho tosha kuwa kiongozi wa nchi anayo fursa ya kubadili kilichopitishwa na Bunge, endapo atakuwa ameona haja ya kufanya hivyo.

“Lazima NEC ijadili kwa sababu wafanyabiashara wanaweza kushikilia msimamo wao kwa sababu wameona wenzao Wakenya wameshikilia hadi Serikali ikabadili uamuzi wa kuacha kusaini muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2024,” anasema.

Kwa namna yoyote ile, anaeleza CCM itakuwa na hofu kwamba pengine wafanyabiashara wakawa na shinikizo zaidi kama njia ya kufanikiwa.

Mtazamo wa Dk Masabo hautofautiani na Profesa Ambrose Kessy, makamu mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), aliyesema kikao mgomo huo unaonyesha kuna namna Serikali haikusimama vema katika kuitekeleza ilani ya chama hicho inayotaka kuwekwa mazingira rafiki ya biashara.

“Wafanyabiashara kuna mahali wanaona mambo hayaendi vizuri na pengine kwa sababu kuna kodi kubwa wanazotozwa au namna wanavyotozwa ndiyo tatizo,” ameeleza.

Kwa hiyo, anasema kikao kama hicho lazima kilijadili jambo hilo na kuamua mbinu nzuri za kuhakikisha walipakodi hao wanatendewa haki na kusikilizwa.

“Kikao hicho kitatoa maelekezo kwa Serikali kuwasikiliza, si kuwakimbia au kuwatolea maneno ya kuwakatisha tamaa wafanyabiashara,” amesisitiza.


Chokochoko Zanzibar

Kikao cha NEC pia kinafanyika wiki moja tangu Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Dimwa apendekeze kumwongezea muda wa kukaa madarakani Rais Mwinyi.

Dk Dimwa alitoa kauli hiyo Juni 23, 2024 katika hotuba yake alipofunga Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), akisema sekretarieti imetathmini na kujiridhisha kuwa kiongozi huyo anapaswa kuongezewa muda madarakani.

"Wajumbe wa sektetarieti tumejadili na kutathmini kwa kina juu ya utendaji wa Rais Mwinyi, tukajiridhisha hakuna mbadala wake na anastahili aongoze nchi kwa kipindi cha miaka saba, ili apate muda mzuri wa kufanya mapinduzi ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii,” alisema.

Baada ya kauli hiyo kupingwa na kila kona, CCM na Rais Mwinyi mwenyewe walitoa ufafanuzi kuwa kiongozi huyo ataheshimu Katiba.

Kwa kuwa suala hilo lilionekana kama kuna mpasuko ndani ya CCM na wengine wakidhani Dk Dimwa hakuzungumza hilo kwa bahati mbaya, ndiyo sababu Dk Masabo anaamini ajenda hiyo inaweza kujitokeza kwenye NEC.

Mwanazuoni huyo amesema suala hilo linaipaka matope CCM na kutikisa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Katika jambo hilo kunaweza kujitokeza taswira kwamba CCM Zanzibar ikiamua mambo yake hayaweza kwenda, bila CCM bara kuamua. Ni jambo zito lazima walijadili,” amesema.


Sakata la Mpina

Si hayo tu, kikao hicho cha NEC kinafanyika katika kipindi ambacho Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina yupo nje ya Bunge kwa vikao 15, baada ya kuhukumiwa kwa kosa la kudharau mamlaka ya muhimili huo na Spika, Dk Tulia Ackson.

Kwa sababu amekumbana na hukumu ya kudharau mamlaka ya Bunge, matarajio ya wengi ni kwamba adhabu hiyo itafuatiwa na rungu lingine kutoka katika chama chake, hasa baada ya wabunge wenzake kueleza nia ya kulipeleka huko.

“Tukiweka 15 (vikao) wabunge wengine hawawezi kurudia kufanya makosa ya wazi kama yaliyofanywa na mheshimiwa Mpina. Na mimi ni Mjumbe wa NEC nikitoka hapa nitakwenda kumshtaki kwenye NEC,” alisema Livingston Lusinde, mbunge wa Mvumi (CCM).

Kauli ya kumshitaki Mpina NEC, pia ilitolewa na Joseph Musukuma, mbunge wa Geita Vijijini, aliyesema: “Na mimi ni MNEC kesi ni ileile, nikitoka hapa Juni 30 tunaye tena.”

Kuhusu hilo, Dk Masabo anasema linaweza kujadiliwa lakini si kwa mtazamo wa mbunge huyo kuadhibiwa na chama hicho kama wengi wanavyodhani.

Kinachoweza kujadiliwa ni namna alivyoadhibiwa kwa kurejea mchakato wote wa kamati na hoja alizoziibua.

Alipoulizwa kwanini hadhani mbunge huyo hataadhibiwa na chama chake, amesema si wa kwanza kuadhibiwa na kamati hiyo ya Bunge, ilitokea kwa Jerry Silaa (Ukonga), Josephat Gwajima (Kawe) na CCM haikuwaadhibu.

Sababu ya kujadiliwa kwa jambo hilo, amesema ni hatua ya Mpina kuueleza umma kupitia vyombo vya habari, akirejea sheria ya sukari huku kamati hiyo ikimuadhibu kwa kutumia sheria ya NFRA.


Tathmini ya bajeti

Kikao hicho kinafanyika siku chache baada ya wabunge kupitisha bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/25 ambayo pamoja na mambo mengine, ina mzigo mkubwa wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kulipa deni la Serikali.

Kwa mtazamo wa Dk Masabo, NEC hiyo haitaacha kutathmini utekelezaji wa bajeti iliyopitishwa na hasa changamoto zake, likiwemo deni la taifa.


Utekelezaji wa ilani

Hii ni moja kati ya ajenda ambazo kila kikao cha NEC lazima zijadiliwe kwa kuwa zinahusu kutathmini namna Serikali ilivyotekeleza ahadi zilizotolewa na mgombea urais.

Katika ajenda hiyo, aghalabu inaelezwa miradi iliyotekelezwa na shughuli mbalimbali kama zilivyoainishwa katika ilani hiyo.

Kwenye vikao hivyo, Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Sulaiman ndio hukukabidhi taarifa hizo.


Uchaguzi

Pengine kikao hicho, kikawa cha mwisho kikatiba kukutana kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, kama kitafanyika kingine kitakuwa cha dharura.

Na kwa sababu chama hicho na vingine, vinatarajia kushiriki uchaguzi huo, bila shaka ajenda ya mipango kuelekea uchaguzi huo ikajadiliwa.

Katika hilo, mwanazuoni wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Matrona Kabyemela amesema kutokana na mwenendo wa Serikali kwa sasa, bila shaka kikao kitafikiri namna ya kuwa na uchaguzi huru na haki.

“Nisingependa kuona wagombea wa vyama vingine wanaenguliwa katika hatua za awali, eti wamejaza fomu vibaya, nafikiri watalijadili pia hilo,” anasema.

Mbali na hayo, kikao hicho kinatarajiwa kutathmini ziara katika mikoa 11 ya Dk Nchimbi. Mikoa hiyo ni Singida, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma yote mwaka huu.

Mambo mengine yatakayojadiliwa kwa mujibu wa Dk Kabyemela ni suala la uchumi wa nchi na wa mtu mmoja mmoja.

 “Lakini kipato cha watu kiko chini kwa maoni yangu, watajadili yote lakini haya ni mambo mengine muhimu yatakayojadiliwa kwa undani,” ameeleza.