Mwenyekiti wa bodi MCL aonyesha njia ya wanawake kushika nyadhifa za juu

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Leonard Mususa amesema lengo la kuwa na wanawake kwenye nafasi za juu za uongozi litawezekana endapo kutakuwa na dhamira ya dhati.
Mususa ameyasema hayo leo jioni wakati wa jukwaa la The Citizen Rising Woman lililofanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Mususa amesema kama nchi imeweza kuanza kupiga hatua kwa kuwa na viongozi wa juu upande wa serikali lakini bado kuna ombwe kwenye taasisi na kampuni.
Amesema ili kukabiliana na hali hiyo ni muhimu kuwepo kwa mikakati ya kuhakikisha wanawake wengi wanapata nafasi ya kuongoza taasisi na kampuni.
“Tunaona kati ya maofisa watendaji wakuu wa Marekani 5% ni wanawake. Sisemi tuwe kama Marekani ila tunaweza kuangalia namna yetu ya kuongeza wanawake kwenye ngazi za juu.
Akieleza sababu ya kuandaa kongamano hilo, Mususa amesema The Citizen kama chombo cha habari kazi yake ni kuelimisha umma, hivyo suala la kuhamasisha nafasi ya mwanamke ni ajenda waliyoamua kuifanyia kazi.
“Tunahitaji kuwa na usawa kwenye vyumba vya habari angalau 50% wawe wanawake. Hivyo wanawake mlipo Mwananchi na The Citizen hakikisheni mfanye kazi nzuri ili kuhamasisha walioko nje kushiriki kwenye mchakato huu,” amesema.