Mwanza. Mwenge wa Uhuru umetoa siku tano Jiji la Mwanza lirekebishe dosari zilizoonekana kwenye miradi mitatu ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni wakati ukikagua, kuweka mawe ya msingi na kuizindua.
Miradi hiyo ambayo ni ujenzi wa Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mabatini unaogharimu Sh142 milioni, ujenzi wa barabara ya mita 372 katika kata ya Isamilo inayogharimu Sh348 milioni na ujenzi wa ghorofa lenye vyumba 12 vya madarasa katika Shule ya Sekondari Mirongo linalojengwa kwa Sh513 milioni ni miongoni mwa miradi saba yenye thamani ya Sh4.5 bilioni iliyokaguliwa na Mwenge wa Uhuru.
Akizungumza Julai 15, 2023 wakati wa kukagua miradi hiyo, Kiongozi wa Mbio hizo Kitaifa, Abdalla Shaibu Kaim ingawa alilidhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo amewataka viongozi wa jiji hilo kufanyia kazi mapungufu madogo yaliyobainika hadi itakapofika Julai 20 mwaka huu kisha kuambatanisha picha za ushahidi za kuonyesha kabla na baada ya marekebisho.
“Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 zimefika katika mradi huu ya ujenzi wa ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mabatini, tumekagua na kupitia kwa kina nyaraka hazina shida kwa kiwango kikubwa isipokuwa tumekuta baadhi ya kasoro ambazo tunatoa siku tano kuanzia leo zifanyiwe kazi kwa kuzingatia yale mapungufu tuliyowaambia na baada ya hapo mtatutumia picha zitakazokuwa zinaonyesha kabla na baada ya marekebisho,”amesema Kaim
Katika mbio hizo za Mwenge uliopokelewa Shule ya Msingi Igoma ukitokea Manispaa ya Ilemela zaidi ya miti ya matunda 3,000 imepandwa, mifuko ya saruji 300 imekabidhiwa Shule ya Msingi Samia, umezindua dawati la kuzuia rushwa na madawa ya kulevya kwenye Shule ya Sekondari Kasese, kukagua mradi wa uwekezaji wananchi kiuchumi na ufunguzi wa Kituo cha Afya cha Bulale.
Akizungumza mara baada mbio hizo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema Sh1.5 bilioni kati ya Sh4.5 bilioni iliyotumika kwenye ujenzi wa miradi hiyo imetokana na nguvu ya wananchi huku Sh6 milioni ya maandalizi ya ujio wa Mwenge huo zimetokana pia na michango ya wakazi wa Jiji hilo.
“Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Nyamagana umekimbizwa kilomita 37.7 katika kata 13 za Kishiri, Igoma, Mabatini, Mbugani, Pamba, Isamilo, Igogo, Mkuyuni, Butimba, Nyegezi, Mkolani, Bulale na Buhongwa ambapo umezindua mradi mmoja, umefungua miradi miwili na umeweka mawe ya msingi kwenye miradi mitatu, yote kwa pamoja inagharimu Sh4.5 bilioni,”amesema Makilagi
Mwenge huo umepokelewa Julai 13 mwaka huu mkoani Mwanza na utakimbizwa kwa siku nane hadi Julai 20, 2023 huku ukiwa umebeba kauli mbiu ‘Tunza mazingira, okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai kwa uchumi wa Taifa’